NA WAANDISHI WETU
MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amesema kitendo cha wabunge wa CCM kuendelea na mkutano wa Bunge Maalum la Katiba ni matumizi mabaya ya wingi wao ndani ya Bunge hilo.
Pamoja na hayo, amesema haungi mkono hatua iliyofikiwa ya kitendo cha wajumbe wenzake wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba mpya kwa sababu swala la Katiba halina mshindi.
Alisema kitendo kilichofanywa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge ni kuendelea kuacha yanayoendelea kutokea.
Hayo aliyasema jana kupitia taarifa yake ailiyoitoa ambapo alisema kuwa pamoja na mchakato huo kupita katika misukosuko, lakini waamuzi wa mwisho ni wananchi ambao wataamua kwa kupigia kura Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa.
“Sisi tutafanya yote. Lakini waamuzi wa mwisho ni wananchi kwani wana nafasi ya kupiga kura ya ‘referendum’ ya kuikubali Katiba hiyo mpya au la. Kutumia wingi ndani ya Bunge ni matumizi mabaya, ni bahati mbaya sana kwamba tumeyaacha yale yanayotokea bungeni yaendelee kutokea.
“Kimsingi, Ukawa walipashwa kubaki bungeni na kujenga hoja zao ndani ya Bunge. Hoja za kwamba wanatukanwa na kubezwa hazina mashiko kwa sababu sisi wajumbe wa Bunge la Katiba siyo waamuzi wa mwisho.
“Lakini pia kwa hatua tuliyofikia mie siungi mkono. Katiba ni jambo la maafikiano. Katiba ni jambo la maridhiano. Washindi wanapaswa kuwa ni Watanzania. Na pia niwakumbushe wabunge wenzangu wa CCM kuwa kinachoandaliwa kwenye Bunge la Katiba ni Katiba ya Watanzania wote na siyo Katiba ya CCM.
“Ndiyo ni kweli kwamba mle bungeni CCM ina wabunge wengi. Na ni kweli pia kwenye demokrasia wengi wape. Lakini pia demokrasia pevu na yenye tija ni ile inayoheshimu na kuyafanyia kazi maoni ya wachache,” alisema Filikunjombe.
Katika hatua nyingine, watu wa kada mbalimbali, wamepinga kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ya kuitaka Serikali kuvibana vyombo vya habari vinavyorusha midahalo inayojadili mwenendo wa Bunge hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na gazeti hili, walisema Bunge hilo halina ubavu kisheria wa kuvibana vyombo vya habari, wajumbe waliokuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo iliongozwa na Jaji Joseph Warioba au wananchi wa kawaida kujadili suala hilo la Katiba.
Akizungumzia kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba alisema Bunge Maalumu halina uwezo wa kisheria wa kutunga sheria au kushauri kuzuia vyombo vya habari kwa sababu hiyo si kazi yao, bali kazi yao ni kujadili Rasimu ya Katiba.
Alisema kauli za aina hiyo zinazotolewa na Bunge hilo ndizo zinazoonyesha uhalali wa Ukawa kukataa kushiriki katika vikao vyao ambavyo vinaonyesha kuwa na nia ya kuchakachua maoni ya wananchi.
Prof. Lipumba alisema: “Tazama wanaanza kutafuta njia za kubana hoja nzito ambazo zimo ndani ya rasimu iliyopendekezwa na wananchi wakitaka Katiba isimamie uwazi, uwajibikaji na uadilifu, vifungu hivyo vyote vimewekwa kwa sababu wananchi wanataka uwepo wa uhuru wa vyombo vya habari, ili wapate haki ya kupata taarifa kwa mambo yanayowagusa,” alisema.
Profesa Lipumba alishangazwa na kauli ya Bunge hilo kufikiria kuwanyima wananchi haki ya kuchangia, kuhabarishwa au kutojadili maoni hayo, hali ambayo anaiona kama ni kuondoa maudhui ya katiba yenyewe.
“Hilo pekee linathibitisha kwamba kuanzia mwenyekiti hadi wajumbe hawaheshimu maoni ya wananchi, na ndiyo maana wanataka kufanya mambo yanayokwenda kinyume na mapendekezo ya wananchi na wanaonyesha wazi kabisa hawana nia ya kuheshimu maoni ya wananchi, lakini pia hawana nguvu za kisheria za kuzuia uhuru huo wa kikatiba,” alisema.
Akizungumzia kuhusu wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufungwa midomo ya kuzungumzia Katiba, alisema wanao wajibu wa kuwaeleza Watanzania walichokiandika ndani ya rasimu hiyo kwa sababu ndio wanaojua sababu za kuingiza maoni yaliyomo kwenye rasimu hiyo na pindi inapojitokeza Watanzania wakahitilafiana au rasimu kuchezewa, waweze kutoa tafsiri.
“Linalonisikitisha ni kwamba, Serikali tayari imeshafunga hata ile tovuti ambayo ilikuwa ikitoa taarifa kuhusiana na mchakato wa rasimu hiyo, hivyo inaonyesha kwamba hawana nia thabiti ya kuyatendea haki maoni ya wananchi na hawana haki kisheria ya kuwazuia wajumbe kutolea ufafanuzi nje ya Bunge hilo,” alisema.
Alisema anapata shaka kama kweli wajumbe hao wana nia thabiti ya kutengeneza katiba inayolenga maoni ya wananchi kama ilivyo sasa, walivyoanza kuzibana haki mbalimbali ikiwamo ya uhuru wa kupata habari.
Akizungumzia hoja ya wajumbe kutaka mabadiliko ya kanuni iliyotaka wajumbe wa kundi la 201 walioteuliwa na rais, inayosema kuwa kama wasipohudhuria mikutano kwa siku tano mfululizo bila taarifa wafutwe na wateuliwe wengine, Profesa Lipumba alisema: “Sheria ilivyo ni kwamba rais anayo mamlaka ya kuteua ila hana haki ya kufukuza.”
Profesa Kabudi
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema suala la kuzuia litakuwa linakwenda kinyume na Katiba ambayo inampatia kila Mtanzania uhuru wa kutoa maoni na mawazo.
“Kama wamesema hivyo, wakumbuke kuwa mchakato wa Katiba ni safari, na safari yoyote ina mabonde, milima, ina kona na nyingine ni kali sana, huku nyingine si kali sana, na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu sana, na haijengwi kwa kuzuia maoni ambayo unatofautiana nayo.
“Hapa tunahitaji tujifunze kwa mwanafalsafa mmoja aitwaye Voltea, aliwahi kusema kwamba ‘jambo la mwisho ambalo nitalifanya ni kumzuia mtu kutoa maoni yake, hata kama maoni hayo anayoyatoa yatakuwa ya kunitukana mimi, nitamwambia una uhuru, lakini umevuka mpaka’, akimaanisha una uhuru wako wa kutoa maoni, lakini umevuka mipaka ya heshima ya uhuru wa utu wangu,” alisema.
Profesa Kabudi aliongeza kuwa mjadala wa Katiba uruhusiwe kujadiliwa ili taifa liwe katika mjadala ambao watu wake hawatashupaa.
“Na ndiyo maana nimewahi kusema hata kwenye semina niliyoitwa kwenye Bunge wakati wa kujadili mswaada wa sheria mara ya kwanza, niliwaambia kwamba mpumbavu hushupaa, lakini mjinga huduwaa,” alisema.
Alitoa wito kwa Watanzania kujadili Katiba kwa nia ya kuitafutia muafaka na maelewano, huku kukiwa na tahadhari kubwa kutokana na ukweli kwamba nchi inapita katika kipindi kigumu, inahitaji kila mwananchi awe makini.
Alisema Watanzania wanatakiwa kutambua kwamba taifa ni kubwa kuliko jambo lolote, hivyo, linahitaji uvumilivu wa hali ya juu na unyenyekevu, na katika hilo wasitumie muda mwingi wa kutafuta mshindi au mshindwa.
Alisema Watanzania wanatakiwa kujifunza kupitia busara ya Mwalimu Nyerere aliyewahi kuwasaidia Waafrika Kusini kupata Katiba bora.
“Rais Thabo Mbeki alithibitisha hilo wakati alipokuwa akimkaribisha Rais mstaafu Benjamin Mkapa kutoa mdahalo wa Siku ya Thabo Mbeki, mwaka 2011, ambako alisema chama cha kupigania uhuru cha Afrika Kusini (ANC) kilikuwa kimeandika waraka wa mchakato wa Katiba mpya, baada ya kutoka kwenye utawala wa ubaguzi ambapo waliandika waraka wa mchakato huo ambao ulitaka kuanza kwa kuchagua Bunge Maalumu kama ilivyo hapa kwetu.
“Baada ya kumuonyesha Nyerere waraka ule, aliwashauri wabadili mfumo huo, wakamuuliza kwanini wabadili wakati walifuata misingi ya demokrasia ambayo inaamuliwa na walio wengi. Akawaambia kwamba ANC mpo wengi hivyo mkiita Bunge la Katiba mtajaa ninyi, hivyo ikipatikana katiba italalamikiwa kuwa ya ANC, hivyo kabla ya kupitisha mnatakiwa kuita makundi yote bila kujali wingi wao, ndipo mtafanikiwa kutengeneza Katiba ya kitaifa. Busara hiyo sisi watoto na wajukuu wa Mwalimu tuitafakari na tuitumie kupata Katiba bora,” alisema.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mtu aliyelalamikiwa na wajumbe wa Bunge la Katiba, Joseph Butiku, alisema hana la kusema na hataki kujiingiza katika mgogoro kwenye suala hilo.
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipotafutwa alisema hataki kuchangia lolote kuhusu mjadala huo.
Julius Mtatiro
Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro, alisema Bunge la Katiba halitafika popote kama hakutakuwa na maridhiano kutoka kwa wajumbe wanaopingana.
Alisema nguvu inayotumiwa na Sitta ya kulazimisha kuendelea kufanya kazi katika siku 84 zijazo haitafua dafu kama maridhiano hayatapatikana.
“Hakuna haja ya kuendelea na mchakato feki wa Katiba na kuendelea kutafuna fedha za umma kwa jambo ambalo haliwezekani, ni wendawazimu mkubwa na hilo ndilo linasababisha Bunge liogope kupigia kura sura ya kwanza na ya sita kwa kuhofia kuumbuka kukosa theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar,” alisema.
Mukajanga
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, alisema vyombo vya habari vinatakiwa kupongezwa kwa juhudi wanazozifanya katika kuripoti na kuandaa mijadala ya mchakato wa katiba kwakuwa wanatoa nafasi kwa wananchi kushiriki na kujadili Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mukajanga alisema vyombo vya habari vina jukumu maalumu katika mchakato huo kwa kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki na kujadili wakiwa kama wahusika wakuu kwa kuwa mchakato huo si wa vyama vya siasa wala makundi.
“Kuandika au kujadili kwa kuonyesha masuala yanayohusiana na Katiba kwa vyombo vya habari ni kutimiza jukumu lao, vinapaswa kupongezwa, sio kukatishwa tamaa kwa kutishiwa kufungiwa kwani bila vyombo hivyo tungepata wapi kujua maoni ya wananchi?
“Tukisema watu wakae kimya kuanzia sasa bila kurusha masuala ya Katiba watafurahi?” alihoji Mukajanga.
Taarifa hii, imeandaliwa na Shabani Matutu, Aziza Masoud na Victor Mrutu (TUDARCO)
Mwenyekiti wa bunge la katiba,kufikiria kuzuiwa kwa upashwaji wa habari kuhusu mchakato mzima wa bunge la katiba,yeye pamoja na wajumbe wake ni kuashiria nia ovu kwa wananchi.kimsingi watambuee sisi wanachi ndio tutakao amua ni katiba ipi itakayotufaa kwa mfumo wa kupiga kura.
kuendelea kujadiliwa kwa rasimu ya katiba,pasipo maafikiano na maridhiano kati ya pande zote mbili ni ubatili mtupu,na itambulike ya kwamba wale wote walio diriki kushiriki ktk dhambi hiyo,hili khali wakiwa wanajua ya kwamba ni chukizo mbele za mungu.Dhambi hiyo itawafuna wao pamoja na vizazi vyao.
Kama maandikomatakaifu yanavyosema” Ni ubatili mtupu”, kuendelea kujadili katiba mpya katika mazingira ya sasa ni ubatili. Na Mungu hatakubali ubatili huu, mwisho ya wote wananchi wanakwenda Kuikataa kwa kura ya “HAPANA”. Mjadala ulioongozwa na Taasisi ya Mwl. JK Nyerree imewapa wananch nguvu ya kufahamau nini kinaendelea Bungeni ambacho ni upotoshwaji na uchakachuaji, na Hivi watu wapo tayari KUpiga kura ya “Hapana, Hapana, Hapana.” Wabunge wanaokaa bungeni Dodoma na kupoteza pesa za wananchi waoijue hilo, dhambi hiyo itawafuata wao na vizazi vyao. Hii si demokrasia, bali ni ubabe, na katiba haipatikani kwa ubabe. Watanzania sasa ni muda wa kuungana na kuionyesha CCM kwanza, haiwezi kuwaandikia wananchi katiba ili baadaye katiba hiyo hiyo iendelee kuwachagulia viongozi mwaka 2015, hili halikubaliki. Dawa ni watanzania wote kusema “sasa kuburuzwa na CCM basi.” Dawa ni kusimama wote kwa pamoja na kupasa sauti hadi mbingu isikie, na Mungu atajibu tu.
Kitendo cha Bunge la katiba kuendelea na vikao vyake si sahihi kwani Tanzania inahitaji katiba iliyoandaliwa na watanzania na CCM. Lazima ifike wakati watanzania tutambue kwamba kinachoendelea sasa bungeni ni ubabe na si democrasia. kitendo cha kuzuia vyombo vya habari kurusha mijadala mbalimbali ihusuyo katiba mpya ni ukiukwaji wa haki ya kikatiba ya kutoa maoni (Ibara ya 18, katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania 1977).
Maamuzi yanayofanywa na CCM ya kulazimisha mambo ambayo hayana maslahi na taifa hili, mwisho wake unalipeleka taifa letu katika wakati mgumu. Na kama watanzania tutaendelea kuwa na uongozi wa chama hiki ambacho kinaamini katika mabavu na udikteta. MBELENI TUTAUMIA.