Na Mwandishi Wetu, Ludewa
MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amesema kwa muda wa miaka kadhaa sasa baadhi ya vyama vya siasa wilayani Ludewa vimekuwa vikimshawishi atoke kwenye chama chake jambo ambalo amekuwa akilipinga.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kijiji cha Nsele, Kata ya Kilondo wilayani hapa, alisema hata mapokezi aliyoyapata yalikuwa ya vyama vyote, vikiwamo vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), huku baadhi yao wakimshawishi ahamie kwenye vyama vyao.
Filikunjombe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema wapinzani wanamthamini na kuona kazi zake akiwa CCM, hivyo ataendelea kuwajibika kwa wananchi akiwa ndani ya chama hicho.
“Nimekuja hapa nimepokewa na vijana na viongozi wa vyama vyote, hasa vya Chadema, CUF na TLP, na wengine wakati wananibeba walidiriki kuniambia kuwa wana hofu nitakatwa jina kwenye chama changu na kama itakuwa hivyo nijiunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),”alisema Filikunjombe.
Akizungumzia maendeleo ya Kata ya Kilondo, mbunge huyo alisema awali ilikuwa haina huduma za maendeleo ambapo Januari 30, mwaka huu alikwenda na wahandisi wa umeme na kuzindua mradi wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya wilayani humo.
Lakini kutokana na kasi ya utekelezaji wa mradi huo vijiji vyote vya Kata ya Kilondo kabla ya kufikia Desemba mwaka huu vitakuwa vimepata huduma ya umeme ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za maendeleo.
Katika hatua nyingine, wazee wa Kijiji cha Nsele wamemchangia mbunge huyo Sh 100,000 ili aweze kutetea tena kiti chake katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Hatua ya wazee hao imekuja baada ya kile walichodai kuwa katika kipindi cha miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika, kata yao ilishindwa kupata maendeleo ikiwamo ukosefu wa umeme na huduma za afya.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya wazee wenzake, Josephat Mwandesile, alisema kwa kipindi cha miaka michache ya uongozi wa Filikunjombe wamefanikiwa kujengewa zahanati pamoja na kupatiwa huduma ya umeme kwa nguvu ya mbunge huyo.
Hata hivyo, mchango huo umeambatana na masharti kwamba lazima autumie kwa ajili ya kuchukulia fomu za ubunge na si vinginevyo.
Baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Filikunjombe aliahidi kuzitunza na pindi wakati ukifika atafanya kama alivyoelekezwa na wazee hao.