Na FESTO POLEA, DAR ES SALAAM
JULAI 8 hadi16, mwaka huu, wadau wa filamu kutoka nchi zaidi ya 70 watajumuika pamoja kushuhudia filamu zaidi ya 100 zitakazoonyeshwa kwenye Tamasha la 20 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) kwenye Ukumbi wa Ngome Kongwe, visiwani Zanzibar.
Kati ya filamu hizo, ipo filamu ya makala ya prodyuza na mwigizaji maarufu kutoka Hollywood, Leonardo di Caprio inayoitwa ‘The Ivory Game’.
Filamu nyingine ya makala itakayoonyeshwa ni ya mwanaharakati Winnie Mandela kutoka Afrika Kusini iliyoongozwa na Pascale Lamche na nyingine ni ya Whitney Houston ya ‘Can I Be Me’ iliyotengenezwa na Nick Broomfield.
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Fabrizio Colombo, alisema licha ya ugumu katika uchaguzi wa filamu unaotokana na ubora wa filamu walizopokea, wanaona umuhimu na mchango wa ZIFF katika maboresho ya filamu zilizowasilishwa kwao.
Colombo alisema watengeneza filamu kutoka nchi zaidi ya 70, wametuma filamu zao wakiwamo Tanzania, wengine ni Kenya, Canada, Hispania, Ufaransa, Afrika Kusini, Tanzania, India, Australia, Marekani, Nigeria, Rwanda, Brazil, Ghana, Chad, Uganda, Msumbiji, Hungary, Uingereza na Ethiopia.