FIGISUFIGISU ZISIWEPO UCHAGUZI MKUU TFF

0
575

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),  uliopangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mkoani Dodoma, mchakato wake umesitishwa jana, kwa kile kilichoelezwa kutokuwapo kwa maelewano kwa wajumbe wa kamati ya uchaguzi ya Shirikisho hilo

Tayari kamati ya uchaguzi ya Shirikisho hilo ilifikia kufanya usaili kwa watu waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, huku wakishindwa kuwasaili wengine ambao wanakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Watu wanaokabiliwa na kesi ni Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, aliyehitaji kutetea nafasi yake na Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliyeomba kuwania nafasi ya makamu wa rais.

Kwa pamoja wawili hao walikuwa katika mikono ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), wakikabiliwa na tuhuma ya matumizi mabaya ya madaraka na baadaye kufikishwa katika mahakama hiyo.

Kutokana na Malinzi na Kaburu kuwapo rumande ya mahakama ya kawaida ya sheria, tumeelezwa kwamba, kumekuwa na mabishano makubwa ndani ya kamati ya uchaguzi, huku wengine wakitaka nao wapitishwe kwenye kinyang’anyiro hicho.

Sababu hiyo imeifanya kamati kugawanyika katika hilo na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi TFF, Revocatus Kuuli, kufikia uamuzi wa kusitisha mchakato wa uchaguzi huo, ambapo sasa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo itakutana kesho kujadili suala hilo.

Tumesikia kabla ya kusitisha mchakato wa uchaguzi huo kulikuwa na mabishano makali ya kimtazamo kiasi cha baadhi ya wajumbe kutishia kuachia nafasi zao

Kuna baadhi ya wajumbe wa kamati aliona kwa sasa hakuna haja ya watu wanaokabiliwa na mashtaka kuendelea kuwapo katika uchaguzi huo, lakini wengine wakiona kwa kufanya hivyo watakuwa hawajawatendea haki kwa sababu hawajatiwa hatiani.

MTANZANIA tunaona  kuwa Kamati ya Utendaji ya TFF inatakiwa kuja na jibu moja ambalo litawezesha mchakato ya uchaguzi kuendelea na kuachana na figisufigisu ambazo zinaweza kuathiri mchakato mzima wa kupata viongozi wa soka.

Tunahitaji kuona busara zaidi zitawale katika kikao cha kamati ya utendaji kitakachofanyika kesho, kwani wao ni mhimili mkubwa wa kuongoza soka nchini, lakini ni chombo chenye mamlaka ya kutoa uamuzi.

MTANZANIA tunasema kwamba mawazo ya  kila mwana kamati  yatasaidia kujenga uelewano ndani ya kamati ya uchaguzi na baadaye mchakato kuendelea kama kawaida.

Matarajio ya Watanzania wengi ni kushuhudia uongozi mpya ndani ya Shirikisho hilo ukipatikana, bila kuhusisha upendeleo wa upande mmoja.

Malengo ni kusongesha mbele gurudumu la michezo ili kuiwezesha Tanzania kupiga hatua na kuendelea kuwa miongoni mwa mataifa yanayoweza kunufaika kupitia michezo.

Tunarudia kwa kusema, kamati ya utendaji inatakiwa kutenda haki na kutoa muafaka wa jambo hili, ambalo tayari lilianza kusonga mbele na kufikia katika hatua nzuri ya kupatikana kwa uongozi mpya ndani ya shirikisho hilo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here