27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Fidel Castro nyuma ya vurugu Venezuela

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

BAADA ya anguko la Umoja wa Kisovieti (USSR) mwaka 1991, uchumi wa Cuba ulikuwa hoi. Cuba ilijikuta ikihitaji marafiki, ikingatiwa kuwa isingekuwa rahisi kujiendesha bila USSR.

Chini ya Fidel Castro (sasa marehemu) aliyeingia madarakani mwaka 1959 akimng’oa dikteta Fulgencio Batista, uchumi wa Kisiwa hicho ulipoteza ‘sapoti’ kubwa ya Umoja huo wa mataifa ya kijamaa.

Kifo cha USSR kilimfanya Castro aanze kutafuta marafiki wanaoweza kumuinua kiuchumi. Moja kwa moja, safari yake ya kwanza ilikuwa mjini Caracas, Venezuela.

Isingeweza kuwa Marekani kwani taifa hilo lilikuwa likiuunga mkono utawala wa kimabavu wa Batista. Pili, ni kwa kuwa Marekani ilikuwa upande hasimu wa ujamaa, yaani ubepari.

Tatu, ni kutokana na ukweli kwamba Venezuela ilikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya kijeshi aliyofanya Castro dhidi ya dikteta huyo.

Katika namna ambayo haikuwa ikionekana hapo awali, Venezuela ilimpa Castro msaada wa fedha na silaha kufanikisha mpango wake wa kuingia madarakani.

Hivyo basi, Castro alikuwa na kila sababu ya kuanza na Venezuela ndipo kwingine kufuate.

Alipofika kwa majirani zake hao, alikuwa na ombi jingine kwa aliyekuwa Rais wa taifa hilo kipindi hicho, Romulo Betancourt.

Alitaka Venezuela iikopeshe Cuba mafuta yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300, akidai anataka uchumi wa nchi yake usiitegemee Marekani.

Hilo lilipopitishwa na Serikali ya Venezuela licha ya awali Rais Betancourt kuweka ngumu. Meli za mafuta zikaanza kuelekea Cuba kwa makubaliano kwamba wao watakuwa wakiwapatia Venezuela msaada wa madaktari, walimu na wakufunzi wa vyombo vya usalama.

Betancourt alipoondoka madarakani mwaka 1998, ilionekana kuwa unyonyaji huo wa Cuba dhidi ya Venezuela ungefikia ukomo lakini kwa bahati mbaya uliendelezwa na Hugo Chavez aliyeingia Ikulu mwaka 1998.

Kufikia miaka ya 2000, urafiki wa Castro na Venezuela kupitia Chavez ulikuwa umeunufaisha kwa kiasi uchumi wa Cuba kupitia nishati ya mafuta.

Mathalan, ni kipindi hicho ndipo ilipoelezwa kuwa meli kutoka Venezuela zilikuwa zikipeleka takribani mapipa 100,000 kila siku.

Uchumi wa Cuba ya Castro uliimarika maradufu, ikiwamo kulipa madeni ya muda mrefu na kuiinua sekta ya utalii iliyoonekana ‘kufa’ wakati anachukua nchi kwa mapinduzi ya kijeshi.

Ili kunogesha urafiki wao kwa manufaa ya Cuba, Castro alimpa Chavez nyumba ya kifahari iliyokuwa karibu na ile ya balozi wa Korea Kaskazini nchini Cuba.

Wafanyakazi wa viwanda vya mafuta walikuwa wakiingiza fedha nyingi kuliko wengine waliokuwa wakijihusisha na bidhaa zilizokuwa zikizalishwa nchini humo.

Hatimaye, mafuta yakawa ndiyo bidhaa inayosafirishwa zaidi na wananchi wa Cuba.

Wakati huo wote, Castro na Chavez waliendelea kusisitiza kuwa mataifa hayo ni kitu kimoja, ingawa ukweli ni kwamba uchumi wa Venezuela ulikuwa ovyo, tofauti na wa Cuba.

Wakati wananchi wa Cuba wakifurahia maisha, wenzao wa Venezuela walikuwa hoi, ambapo baadhi ya huduma muhimu zilianza kukosekana.

Wananchi wa Venezuela waliokuwa wakifanya kazi Cuba walilazimika kubeba vitu kama sabuni, ambavyo vilikuwa havipatikani kwao kutokana na mdororo wa uchumi.

Hali hiyo ilianza kuibua ukosoaji mkubwa dhidi ya Serikali ya Chavez, akitajwa kuingia kwenye urafiki uliokuwa ukiinufaisha Cuba na si Venezuela.

Wapinzani wake walidai kuwa si tu kiuchumi, bali Cuba ‘imeiweka mkononi’ idara ya usalama wa taifa ya Venezuela.

Bado Castro aliendelea kuwa karibu na Chavez, ikiwamo kumpigia simu na kumshauri arudi madarakani kwa nguvu baada ya kupinduliwa na jeshi.

Chavez alipofariki mwaka 2013 kutokana na ugonjwa hatari wa kansa aliobainika kuwa nao miaka miwili kabla, ilikuwa taarifa mbaya kwa Castro na Cuba kwa ujumla, ambako kwa tatu zilitengwa kwa mapumziko.

Wakati wengi wakiamini kuwa huo ungeweza kuwa mwisho wa urafiki wenye shaka kati ya Cuba na Venezuela, Nicolas Maduro aliyeingia Ikulu kuchukua nafasi ya Chavez naye hakuweza kuepuka kizingiti hicho cha Castro.

Urafiki kati yake na Cuba umeendelea kuwaumiza wananchi wengi wa Venezuela, huku ukikumbana na ukosolewaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa wa upinzani.

Japo si kwa kiwango kile cha utawala wa watangulizi wake, Hadi leo hii, Maduro ameendelea kuwahakikishia Cuba si chini ya mapipa 50,000 ya mafuta kila siku.

“Nasema kwamba, hata kama Cuba itakumbwa na majanga yoyote, bado ina mafuta ya kutosha, yanayoweza kuhudumia kwa siku 35 au 45,” anasema mtaalamu wa nishati ya mafuta wa Cuba, Jorge Pinon.

Wachambuzi wa siasa wanasema Cuba imekuwa ikichukua mafuta Urusi na Algeria lakini mikataba yake na Venezuela imekuwa yenye maslahi mazuri zaidi kwake.

Ni kutokana na hali hiyo ndipo wakosoaji wa Maduro wakiongozwa na Rais wa Bunge, Juan Guaido wameamua kuingilia kati, wakiutaka uhusiano kati ya Cuba na Venezuela usitishwe mara moja.

Kwa upande wao, maofisa wa Cuba wamejibu mapigo wakiweka wazi nia yao ya kutoachana na urafiki wao na Venezuela.

Hivi sasa, kuna shinikizo la kumtaka Maduro aitishe uchaguzi mkuu ambapo mpinzani wake mkubwa, Guaido alijitangaza kuwa Rais wa muda, hivyo kusababisha machafuko.

Tayari vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwa watu zaidi ya 40 wamepoteza maisha kutokana na mvutano uliopo kati ya wafuasi wa Maduro na wale wa Guaido.

Aidha, wegine wapatao 850 wameshikiliwa na polisi tangu Januari 23, mwaka huu, siku Guaido alipochukua uamuzi wa kujitangaza kuwa Rais wa muda wa Venezuela.

Wakati Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya (EU), zikimuunga mkono Guaido, mataifa ya Urusi na China yameendelea kusisitiza kuwa yanamtambua Maduro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles