24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Fedha za Tasaf sasa kutolewa kwa mtandao

Christina Gauluhanga -Dar es salaam

MKURUGENZI Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), Ladislaus Mwamanga, amesema mfuko huo umeboresha huduma zake ili kuwafikia walengwa wote kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwamanga alisema katika maboresho hayo, kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya malipo ya ruzuku kwa kaya masikini unaotarajiwa kuanza Juni, utafanyika kwa njia ya mtandao.

Mwamanga alisema utekelezaji wa kipindi cha pili awamu ya tatu ya mfuko umeanza kutekelezwa baada ya kuzinduliwa rasmi na Rais Dk. John Magufuli Februari, mwaka huu.

Alisema mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao utawawezesha walengwa kuweka akiba na kuondoa kero waliyokuwa wakiipata awali, huku Serikali ikiweka mikakati kadhaa ikiwamo kuwajengea uwezo wa kiuchumi ambao utawawezesha kuona umuhimu wa kununua simu ili kunufaika na huduma mbalimbali za kimtandao.

“Tunaendelea na maandalizi ya kuanza utekelezaji wa kipindi hiki ambacho kitahudumia takribani kaya za walengwa zipatazo milioni 1.4 katika halmashauri zote za Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tayari kupitia majaribio tuliyoyafanya kwenye baadhi ya halmashauri tumebaini mfumo huu  wa malipo ya ruzuku kwa njia ya mtandao ni bora zaidi kuliko mfumo ule wa awali,” alisema Mwamanga.

Alisema katika kipindi cha kwanza Tasaf ilifikia kaya za walengwa milioni 1.1 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Unguja na Pemba, lakini hata hivyo asilimia 39 za kaya zenye uhitaji ambazo zinakadiriwa kuwa ni 5,900 hazikufikiwa katika kipindi hicho kwa sababu ya upungufu wa fedha.

Mwamanga alisema Tasaf imepanga kaya zote zitakazokidhi vigezo vya umasikini zitaandikishwa ikiwamo wananchi ambao hawakunufaika na huduma za mfuko huo katika kipindi cha kwanza kwa sababu mbalimbali na baada ya hapo watendaji watashirikishwa.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa kipindi cha awamu ya tatu ya Tasaf imepanga kugharimu Sh trilioni 2.032 ambazo zitatumika kutekeleza miradi inayolenga kuboresha miundombinu  kwenye sekta za afya, elimu na maji na kiasi kingine kutumika  kutoa ruzuku kwa kaya zinazoishi katika mazingira duni  ili ziweze kuboresha maisha yao.

Alisema kwa mwaka huu  mkazo maalumu umewekwa katika  kuzihamasisha kaya hizo kutumia sehemu ya ruzuku kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili kujiongezea kipato.

“Kama ambavyo Rais Magufuli alivyosisitiza wakati wa uzinduzi wa kipindi hiki, mkazo maalumu umewekwa kwa kutumia nguvu kazi za walengwa kwenye miradi ya maendeleo itakayolenga moja kwa moja suala la kuondoa kero ya umasikini na kukuza uchumi wa kaya za walengwa na wananchi wengine kwenye maeneo ya mradi,” alisema Mwamanga.

Akielezea kuhusu malipo kwa njia ya mtandao, Mwamanga alisema kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa awamu ya tatu ya Tasaf kimekuwa na mafanikio mengi kwani kaya nyingi za walengwa ambazo ziliingia kwenye mpango zikiwa na hali duni zimeimarika kiuchumi, walengwa wengi  wameboresha makazi yao, wamejiingiza kwenye shughuli za kilimo na ufugaji na pia kuanzisha miradi ya ujasiriamali.

Alisema pia katika kipindi hicho cha kwanza, Tasaf imejifunza mambo mengi ikiwa na namna bora zaidi ya matumizi ya mtandao kwenye kutoa ruzuku kwa walengwa.

Mwamanga alisema Tasaf ilianza utaratibu  wa kulipa ruzuku kwa walengwa kwa njia ya mtandao kwa majaribio Mei mwaka 2017 katika Halmashauri 16 nchini.

Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Arusha, Ilala, Kinondoni, Temeke, Mpanda, Kigoma Manispaa, Bagamoyo, Songea Manispaa, Kisarawe, Kilwa, Muheza, Mkuranga, Bahi, Urambo, Siha na Unguja.

Alisema hadi kufikia Januari mwaka huu jumla ya walengwa 55,539  kati ya 102,299 kwenye halmashauri hizo walianza kupata ruzuku kwa njia ya mtandao na tayari wanufaika walikuwa tayari wamejiunga kupata ruzuku kwa mfumo huo.

Mwamanga alisema walengwa 46,760 ambao ni sawa na asilimia 44 katika halmashauri hizo hawajajiunga kwa njia ya mtandao na wanaendelea kupokea fedha zao taslimu kila kipindi cha malipo kwa utaratibu uliopo.

Alisema  walengwa hawa hawakujiunga kwenye mfumo huo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ukosefu wa simu, kutokuwapo kwa mawakala wa malipo hususan vijijini, watoto, wazee na wasiojua kusoma mtandao haikuwa rafiki kwao hivyo hawakujiandikisha.

Mwamanga alisema baada ya utekelezaji wa miaka miwili ya majaribio, imebainika kwamba mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao una ufanisi mkubwa hasa katika upande wa uendeshaji kwa kupunguza gharama kwa mfuko.

Alisema  kuna changamoto chache ikiwamo baadhi ya walengwa kutokujua kusoma na kuandika sambamba na kusahau namba zao za siri mara kwa mara jambo ambalo wamewataka kila mmoja kubuni namba ambayo ni rahisi kuikumbuka.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles