FEDHA ZA MELINI ZILIVYOWAPELEKA PUTA VIJANA 1985

0
436

HAKUNA aliyefahamu kwa nini vijana wengi waliokuwa wakisota na maisha magumu, jijini Dar es Salaam na kisha kupata zali la kazi ya ubaharia na kwenda kuishi nje ya nchi walirejea kwa wingi nchini ili kusherehekea Sikukuu ya Krismas na mwaka mpya wa 1985.

Ilikuwa kama ni ndoto vile, kwani vijana wa maeneo ya Keko, Magomeni, Mwananyamala, Msasani, Ilala na sehemu nyingine walirejea wakiwa katika hali bora ya kimaisha.

Wengi wao walitokea nchini Italia walikobahatika kupata kazi ya ubaharia, wachache walitokea katika nchi ya Ugiriki na baadhi katika nchi za Bara Hindi.

Dar es Salaam ilionekana kuingiliwa na vijana hao ambao haikuwa kazi sana kuwafahamu kutokana na mavazi yao ya kisasa, utumiaji wa fedha lakini pia magari yao ya fahari ambayo mengi yalikuwa aina ya 504 enzi hizo yakiitwa Guruwe.

Ukipishana na kijana wa aina hiyo hupati tabu kumjua hata kwa kusikia harufu ya manukato yake, wengi walipendeza na kuonekana kunawiri tofauti na wenzao waliokuwa wakiendelea kusota.

Wapambe nao hawakuwa nyuma, maana waliwajua kabisa wageni hao ambao mara nyingi walionekana wakati wa kuingia tu lakini kutoka ilikuwa siri ya kila mmoja wao, wenyewe waliamini ukiaga unaweza kukutana na mikosi ikakufanya uendelee kusota Bongo.

Kwa bahati mabaharia wengi waliondoka nchini wakiwa mashabiki wa bendi mbalimbali za muziki wa dansi, lakini waliporejea wakaachana kabisa na muziki huo badala yake wakajitosa katika ushabiki wa muziki wa disko.

Kwa maana hiyo maeneo waliyokwenda kucheza muziki ilikuwa ni katika hoteli zilizokuwa zikipiga muziki wa aina hiyo kama vile YMCA pale Posta Mpya, Mbowe Hotel pale ilipokuwa Bilcanas na kando yake kidogo paliitwa Ushirika Club au 900 Vision.

Vilevile kandokando ya bahati kulikuwa na kumbi kama Rungwe Oceanic, Kunduchi Beach Hotel na Mwananyamala kulikuwa na ukumbi maarufu wa Villa.

Lakini baada ya kujirusha sana katika siku hizo za mwisho wa mwaka na kisha kuikaribisha Januari ya mwaka 1985, mabaharia hao waliamua kutafuta siku moja kwenda kuagana katika ukumbi utakaokuwa Uswahilini.

Siku hiyo watacheza muziki wa dansi wa bendi yoyote, ilimradi iwe inapiga katika ukumbi waliokubaliana kukutana.

Bahati ikaangukia Ukumbi wa Omax Bar uliokuwepo Keko sehemu ambayo kwa sasa ni maarufu kwa utengenezaji wa fenicha.

Magari ya kifahari yalitapakaa nje ya ukumbi huo, na mabahari na wapambe wao walioneka kuingia kila baada ya dakika na haikuchukua muda mrefu ukumbi ule ukatapika.

Kwa bahati nzuri siku hiyo ilikuwa Jumamosi, Januari 12, 1985 Bendi ya Orchestra King Kikii Double O ndiyo iliyokuwa ikifanya onyesho katika ukumbi huo.

Kwa bahati nzuri tena bendi hiyo ilikuwa na wanamuziki waliokomaa kwa kupiga muziki wa aina mbalimbali, akiwemo Tabia Mwanjelwa, ambaye kwa sasa anaishi nchini Ujerumani, Rizy, na King Kikii sambamba na kina Kapelembe Kokoo na wengine.

Walipogundua kwamba siku hiyo ugeni waliokuwa nao haukuwa wa kawaida, basi wanamuziki wa bendi hiyo walianza kutumbuiza kwa nyimbo mbalimbali na mapigo ya aina Afrika Magharibi na vilevile magoma ya Ulaya, hali iliyowafanya mabaharia wachanganyikiwe na kuanza kucheza na pia kuhoji kama wanamuziki hao walikuwa wapo miaka yote.

Wapo walioondoka wakimuacha King Kikii akiwa na OSS lakini ufanisi ule jukwaani uliwachengua kiasi cha jioni ilipohamishwa onyesho na kwenda Bahari Beach Hotel walisomba na mabaharia wote wakaenda kumalizia furaha yao katika ukumbi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here