Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH) imetoa tuzo kwa Abilis Foundation kutambua mchango wake mkubwa katika kusaidia watu wenye ulemavu, hususan katika maeneo ya Global South.

Tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini juhudi za Abilis Foundation katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 12, 2025 jijini Dodoma, Mratibu wa Abilis Foundation, Winniel Manyanga, alisema kuwa tuzo hiyo ni uthibitisho wa mafanikio ya juhudi zao ndani ya jamii.
“Tunashukuru kwa kutambuliwa, na tunapokea tuzo hii kwa furaha. Kama Abilis Foundation, tutaendelea kushirikiana bega kwa bega na FDH kuhakikisha jamii ya watu wenye ulemavu inapata haki na usawa. Hii ni hatua muhimu katika kuondoa vikwazo vinavyowakabili,” alisema Manyanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, alisema kuwa Abilis Foundation imekuwa mstari wa mbele kufadhili miradi mbalimbali inayosaidia watu wenye ulemavu, hatua ambayo imeleta matokeo chanya kwa jamii.

“Tuzo hii ni ishara ya kuthamini mchango wa Abilis Foundation. Kupitia miradi yao, watu wenye ulemavu wamepata uelewa, elimu na fursa za kujikwamua kiuchumi, lengo likiwa ni kujenga jamii jumuishi,” alisema Salali.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Foundation for Disabilities Hope na Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida, alisisitiza kuwa msaada wa Abilis Foundation umeleta mabadiliko makubwa kwa watu wenye ulemavu, hasa katika sekta za ajira, elimu, uchumi na huduma za afya.
Lulida alihimiza wadau wengine kujitokeza kusaidia juhudi hizo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao na nafasi sawa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Ushirikiano huu ni hatua muhimu katika kuhakikisha ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika nyanja zote za maisha. Ni wajibu wetu kama jamii kushirikiana kuwawezesha na kuondoa changamoto zinazowakabili,” alisema Lulida.