Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, amewataka wanasheria kuendelea kutumia Mahakama mbalimbali nchini kudai haki sheria kandamizi ziweze kubadilishwa.
Amesema hali hiyo inatokana na Bunge kushindwa kubadilisha sheria mbalimbali ambazo ni kandamizi hivyo ni vema mawakili watumie mahakama kudai haki hizo ikizingatiwa ndicho chombo pekee kilichobakia kinachoweza kutoa haki kwa wananchi.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa mawakili na wanasheria watetezi wa haki za binadamu kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo kupata mawakili wenye nia ya kwenda mahakamani kuendesha kesi za katiba na za uvunjifu wa haki za binadamu yaliyoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THDRC).
“Kuna sheria mbalimbali kandamizi ambazo mpaka leo (jana), Bunge halitaki kuzibadilisha.
“Kuna sheria kandamizi na uvunjifu wa Katiba bado umeendelea kufanywa kila kukicha hivyo ni wakati mwafaka sasa kwa watu kwenda mahakamani kupinga mambo hayo kufanyika nchini.
“Na ijulikane kwamba Mahakama pekee haiwezi kufanya kazi bila ya kuwa na mawakili kwa kushirikiana na wananchi kupeleka kesi hizo.
“Na kwa kuwa Bunge halitaki kabisa kubadilisha sheria kandamizi na serikali nayo haitaki kupeleka miswada bungeni kubadilisha sheria hizo, kilichobaki watu waende mahakamani tu ndiyo suluhisho,’’ alisema Fatma.
Rais huyo wa TLS alisema anatambua zipo kesi nyingi za katiba ambazo zinapelekwa mahakamani na wanasheria mbalimbali lakini zimekuwa zikigonga mwamba.
Aliwataka kutokata tamaa kwa maana ipo siku haki hiyo inaweza kupatikana.
Akizungumzia watu wanavyowekwa mahabusu kwa muda mrefu, alisema TLS inasikitishwa na hatua hiyo wakati ni haki ya mtuhumiwa kupelekwa mahakamani na uchunguzi kufanyika katika makosa husika ili hukumu itolewe.
Fatma alisema TLS haitaendelea kuvumilia na itajitoa kwa ajili ya kuwatetea wananchi na kupaza sauti dhidi ya baadhi ya viongozi wanaojichukulia sheria mbalimbali zinazovunja Katiba ya nchi.
“TLS haiwezi kuvumilia kuona watu wanawekwa mahabusu bila kuwa na hatia yoyote tena kwa muda mrefu.
“Wananyimwa dhamana ambayo ni haki yao … na kwa sasa hali ni mbaya zaidi ya uvunjifu wa katiba unaoendelea.
“Hapa mahakama ndiyo suluhisho pekee na mafunzo haya yatatoa mwanga jinsi gani ya kuweza kuanza na masuala haya yote,’’ alisema Fatma.
Mratibu wa Mtandao wa THDRC, Onesmo ole Ngurumwa, alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na mawakili waliosajiliwa zaidi ya 5000, lakini wenye uwezo wa kuendesha kesi na kutetea haki za binadamu hawazidi 50.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, ndiyo sababu mafunzo hayo yanatolewa kuwajengea uwezo lengo likiwa ni kufikia 1/10 ya mawakili nchini.
Ukishakuwa mtetezi ni lazima pia ujue sheria zitakazoweza kukusaidia na mawakili pekee ndiyo watu muhimu kuweza kuwasaidia wananchi wasinyanyasike,” alisema.
Mhadhiri wa Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. James Jesse, alisema ili Watanzania waweze kuishi kwa amani, upendo na undugu ni muhimu.
Alisema viongozi pia wanapaswa kuziheshimu na kuzilinda haki za binadamu ambazo baadhi yake ni haki ya uhuru wa kutoa maoni.
Alisema kama Taifa litaminya haki hizo basi watu wake wanaweza kutumia mbinu nyingine za vurugu kuonyesha hisia zao za kukosa fursa ya kueleza mawazo.
Dk. Jesse alisema hali ikifika huko, kujinasua itakuwa ni vigumu kurudi katika hali ya kawaida.
“Ili Taifa liwe na amani ya kudumu ni vema watu wakakumbushwa tu kuwa na amani ni hii inakwenda sambamba na kuheshimu na kulinda haki za binadamu,’’ alisema.
Wakili Warehema Kibaha, alisema mafunzo hayo yatawasaidia lakini huwa wanapata ugumu kwa kuwa kesi hizo mara kadhaa zikisimamiwa na wao wanaonekana ni watu wa kupinga hata kama wanakuwa na haki ya kufanya hivyo.
“Yaani ukiwa wakili na kila siku wewe unatetea haki za binadamu unaonekana kuwa ni tofauti.
“Utasakamwa na utaonekana ni mtu wa kundi fulani kumbe ni hisia tu ambayo imejengeka katika jamii yetu,’’ alisema Wakili Kibaha.