28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Fasheni ya Chenge yatesa Baraza la Maadili

chengeNa Aziza Masoud, Dar es Salaam
BARAZA la Maadili kwa mara nyingine jana limeshindwa kumhoji Loicy Appollo, ambaye ni Naibu Kamishna Upepelezi wa Kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), anayedaiwa kupata mgawo wa fedha za Escrow, baada ya kutumia mbinu ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ya kukimbilia mahakamani.
Appollo, ambaye anadaiwa kupata mgawo wa Sh milioni 80.8, alikataa kuhojiwa jana kwa kudai kuwa shauri hilo lilishawekewa pingamizi Mahakama Kuu.
Kigogo huyo amekuwa mtuhumiwa wa nne kutoa pingamizi hilo, ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu Chenge, anayedaiwa kupokea mgawo wa Sh bilioni 1.6 kuwa wa kwanza kukimbilia mahakamani.
Juzi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala Ufilisi na Udhamini (Rita), Phillip Saliboko, alikwamisha Baraza hilo kumhoji kwa madai ya kuwa kesi inayohusu miamala ya akaunti hiyo imewekewa zuio la kujadiliwa Mahakama Kuu.
Pingamizi la jana lilitolewa na wakili wa Appollo, Willson Ogunde, mara baada ya kusomewa mashtaka ambayo mteja wake aliyakana.
“Mwanasheria kabla ya kwenda katika hatua ya maelezo ninalo pingamizi la awali la kisheria ambalo naomba kuliwasilisha mbele yako.
“Kwa mujibu wa Mahakama Kuu, shauri namba 51 la mwaka 2014 ambapo uamuzi wa kuzuia kujadili miamala ya akaunti ya Escrow ulitolewa Novemba 5 mwaka 2014, hivyo baraza lako tukufu halina mamlaka ya kusikiliza malalamiko yaliyoletwa mbele yako,” alisema Ogunde.
Alisema anatambua kwamba pingamizi kama hilo lilikwishawasilishwa mbele ya jopo hilo katika kesi kama hizo, zikiwemo ya Chenge, Saliboko na Rugonzibwa na baraza lilisema lina mamlaka ya kusikiliza, licha ya pingamizi la Mahakama Kuu.
Alisema kwa kuwa kesi hiyo ni tofauti na wao wanawasilisha pingamizi hilo kwamba kwa mujibu wa amri hiyo, baraza halina mamlaka ya kusikiliza na wanaomba shauri lisitishwe kwakuwa malalamiko dhidi ya mlalamikiwa yanahusiana na masuala ya miamala ya akaunti Escrow ambayo imeshazuiwa kujadiliwa.
Baada ya kuwasilisha pingamizi hilo, Wakili wa Baraza hilo, Filotheus Manula, alisimama kupinga pingamizi hilo na kudai kuwa shauri hilo ni mwendelezo wa uchunguzi wa awali ulioanza mwaka jana ambapo aliitwa na baraza na kuhojiwa bila kuweka pingamizi.
“Nakubaliana na mwanasheria mwenzangu kwamba baraza lilisitisha suala la Chenge, Saliboko na Rugonzibwa, lakini hapa tunasimamia kuwa huu ni mwendelezo wa uchunguzi ambao mtuhumiwa alikuja kuhojiwa, kesi zilizopita hakuna miongozo iliyotolewa kuonyesha kwamba wata-review (watapitia), baraza lina muda maalumu tofauti na mahakama ambao wao wanasikiliza kesi muda wote,” alisema Manula.
Alisema hukumu iliangalia kifungu cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma iliyotungwa mwaka 1995 na kuanza kutumika Julai.
“Tuki-refer (rejea) taarifa ya Bunge ili tujue nia hasa ya kutunga sheria ile kifungu kinaeleza mtu akishughulikiwa chini ya viongozi wa umma haitakuwa kinga kwake kushughulikiwa na sheria ya maadili, baada ya mwongozo huo naomba shauri hili liendelee kwa kuwa sheria inajieleza suala hili halina kizuizi,” alisema Manula.
Baada ya mvutano huo, Mwenyekiti Baraza la Maadili, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi, alianza kufafanua sheria iliyotungwa na Bunge ambapo alisema baraza halina ukiritimba wa kusikiliza kesi zinazotokana na sheria inayotokana na Bunge.
“Baraza hili halina monopoly (ukiritimba) wa kusikiliza kesi zinazotokana na sheria hii, kesi za utovu wa maadili zinaweza zikasikilizwa na sheria nyingine penal code na nyingine,” alisema Jaji Msumi.
Alisema tafsiri ya sheria inapokuwa na utata ndipo inapopatikana nia ya Bunge ni nini na hadhani kama Bunge lilikuwa na nia hiyo, ambayo anaizungumzia wakili wa mtuhumiwa.
“Baraza lilishakataa hoja iliyotolewa kuhusu kuhusika katika zuio na halina madaraka ya kusikiliza tamko hili kwa sababu haidhani kama ni miongoni mwa waliotajwa.
“Hatuoni kama baraza lina appendix kwamba hawa waliotajwa ni kwamba wasifanye kitendo ambacho kitasababisha suala hili kwenda kujadiliwa na Bunge na sisi hatupo huko, kwa hiyo ombi au pingamizi lako limekataliwa,” alisema Jaji Msumi.
Baada ya kauli hiyo, wakili Ogunde aliomba nakala ya hukumu ili aweze kuipeleka Mahakama Kuu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
“Nafikiri naomba tupewe nakala ya ruling (hukumu) ili mlalamikiwa aweze kuifikisha Mahakama Kuu kwa ufafanuzi zaidi,” alisema Ogunde.
Baada ya Ogunde kutoa kauli hiyo, Jaji Msumi alimtaka kuharakisha kulipeleka Mahakama Kuu shauri hilo ili kuweza kuweka kumbukumbu ambazo zitasaidia katika mashauri mengine.
Mashtaka
Akisoma hati ya mashtaka, Mwanasheria wa Baraza la Maadili, Mwanaharabu Talle, alisema mlalamikiwa, Appollo ambaye ni kiongozi wa umma, kwa mujibu wa fungu namba nne la sheria ya maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995 na kanuni zake.
Alisema mlalamikiwa amekiuka maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa fungu la 12(1)(e),12(2) na fungu la 6(a)(e) na (f) la sheria la maadili ya viongozi wa umma ya mwaka 1995 kwa kuomba fadhila za kiuchumi kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, kiyume na fungu la 6(f) la sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Alisema mnamo Februari 24 mwaka 2014, mlalamikiwa alipokea Sh milioni 80.8 kupitia akaunti ya benki ya Mkombozi namba 00120102684801 tawi la St. Joseph, lililopo Dar es Salaam, kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, ambayo ina uhusiano wa kikazi na TRA kama mlipa kodi.
“Kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo wakati ni kiongozi katika mamlaka hiyo ni ukiukwaji wa fungu namba 6(e) la sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa maslahi,” alisema Talle.
Alisema mlalamikiwa kwakutumia wadhifa wake alijipatia maslahi binafsi ya kifedha kinyume na fungu la 12(e) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Aliongeza kuwa mlalamikiwa hakutamka kwa Ofisa Masuuli (Accounting Officer) mara baada ya kupokea fedha hizo kutoka kwa kampuni hiyo kinyume na kifungu cha 6(f) na fungu la 12(2) la sheria ya viongozi wa umma.
Alibainisha kuwa mlalamikiwa pia hakutamka kwa Kamishma wa Maadili kuhusu umiliki wa hoteli ya ‘Classic Hotel’ iliyopo Kinondoni, yenye thamani ya Sh milioni 150 katika tamko lake la rasilimali na madeni kwa kipindi kilichoishia Desemba 31 mwaka (2010, 2011, 2012, 2013 na 2014) kinyume na matakwa ya kifungu cha 9(1)(c).
Wanasheria ya maadili wachanganya madawa
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo kuhusu sakata la Escrow, Jaji Msumi aliwalaumu wanasheria wa baraza kwa kushindwa kuandaa hati ya mashtaka vizuri kutokana na kuchanganya shtaka la Escrow na lile la mtuhumiwa kumiliki hoteli ya ‘Classic’ na kudai kuwa kufanya hivyo kumesababisha suala hilo kutojadiliwa kwa siku ya jana.
“Sekretarieti mnapaswa muwe makini katika kuandaa hati za mashtaka ili next time (wakati mwingine) tukiandaa malamiko tukumbuke kutenganisha na kama hayahusiani,” alisema Jaji Msumi.
Alisema suala la umiliki wa hoteli halipo katika sakata la Escrow, lakini limeshindwa kujadiliwa kwa sababu zote zilikuwa zimewekwa katika hati moja ya mashtaka, hivyo hawawezi kuendelea nalo.
Alisema walipaswa kuweka utaratibu wa namba katika malalamiko hayo na yangekuwa tofauti na kungekuwa na urahisi wa kujadili umiliki wa hoteli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles