29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

FARU MPYA AWEKA REKODI NGORONGORO

Na MASYAGA MATINYI – DAR ES SALAAM


 

faruMNYAMAPORI aina ya faru anayesadikiwa kuwa na umri mkubwa kuliko faru wote duniani, anaishi katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Faru Fausta mwenye umri wa miaka 54, ni miongoni mwa faru weusi ambao asili yao ni kusini mwa Afrika na kutokana na umri mkubwa, kwa sasa amepoteza uwezo wa kuona.

Tofauti na faru wengine wenye umri mkubwa duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Fausta anaishi katika mazingira ya asili, lakini wengine katika nchi tofauti duniani, ikiwamo Kenya wanaishi katika mazizi maalumu (zoo) au maeneo yaliyotengwa kwa faru yajulikanayo kama “Rhino Sanctuary”.

Akizungumza na MTANZANIA, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk. Fred Manongi, alisema kwa sasa Fausta amehifadhiwa katika banda maalumu, baada ya kujeruhiwa na kundi la fisi.

Alisema wataalamu wa wanyamapori na uhifadhi walikuwa wanatafakari kumwachia kutoka katika banda hilo, ili arejee na kuishi kwenye mazingira yake ya asili baada ya afya yake kuimarika.

“Huyu faru amekaa katika banda kwa takribani mwezi mmoja sasa, tunaangalia uwezekano wa kumwachia aendelee kuishi kwenye mazingira yake ya asili baada ya majeraha yake kuanza kupona,” alisema.

Mhifadhi huyo, alisema Fausta ambaye ni miongoni mwa faru zaidi ya 50 wanaoishi Ngorongoro, hakuwahi kuzaa katika maisha yake yote.

“Fisi waliomjeruhi walifanikiwa kufanya hivyo kutokana na udhaifu alionao unaotokana na umri mkubwa, lakini tumejipanga kuhakikisha anaishi miaka mingi zaidi, na kuacha historia ya kipekee,” alisema Mhifadhi bingwa wa faru wa NCAA, Cuthbert Lemanya.

Matukio mawili yaliyotokea Desemba, mwaka jana nchini Tanzania na Kenya, yaliibua mijadala mizito na kuwafanya faru kutawala mijadala kadha wa kadha.

Nchini Tanzania, ziliibuka taarifa zilizodai kupotea kwa faru maarufu kwa jina la John, aliyekuwa akiishi Ngorongoro, ambaye awali ilidaiwa aliuzwa kwa mwekezaji Kampuni ya Grumeti.

Lakini baadae ilibainika kuwa John hakuuzwa, bali alihamishwa baada ya taratibu zote kufuatwa kutoka Ngorongoro na kupelekwa eneo la Sasakwa, Grumeti, ambako Agosti 21, mwaka jana alifariki dunia kutokana na maradhi na umri. Kwa kawaida umri wa faru kuishi ni miaka 35 hadi 38.

Kwa upande nchi jirani ya Kenya, Desemba 5, mwaka jana, faru mzee kuliko wote nchini humo aliyejulikana kwa jina la Solio (42), alifariki dunia.

Solio alikuwa amehifadhiwa eneo maalumu la uhifadhi (wildlife conservancy), liitwalo Lewa, ambalo linatajwa kuwa hifadhi kubwa maalumu (si ya asili) ya faru barani Afrika. Katika hifadhi hiyo kuna faru weusi 84 na weupe 72.

Faru ni miongoni mwa wanyamapori ambao wapo katika tishio la kutoweka duniani, kutokana na majangili kuwaua kisha kuuza pembe zao kwa bei kubwa, soko kubwa likiwa Mashariki ya Mbali.

Tangu mwaka 1998, Tanzania imekuwa na mpango mkakati maalumu wa kuongeza idadi ya faru, ili kuwa na zaidi ya faru 100 ifikapo 2018.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Save the Rhino ya nchini Uingereza, kulikuwa na faru 500,000 barani Afrika na Asia mwanzoni mwa karne ya 20, lakini kwa sasa wanakadiriwa kusalia 29,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles