26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Fao la kujitoa lawapandisha hasira wafanyakazi  

gratian-mukobaHARRIETH MANDARI NA PAULINE KEBAKI (TUDARCO)

CHAMA cha Walimu (CWT) pamoja na jumuiya mbalimbali za wafanyakazi wametoa tamko la kupinga hatua za serikali kutaka kuliondoa fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamiii.

Msimamo wa kupinga hatua hiyo ya serikali umekuja wakati serikali ikijiandaa kupeleka muswada bungeni wa mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ambapo kwa sasa fao la kujitoa litaondolewa na badala yake litaletwa fao la kutokuwa na ajira.

Katika tamko lao la pamoja lililotolewa jana, CWT pamoja na asasi mbalimbali za kiraia, zikiwemo Jumuiya za Wafanyakazi wa Migodini (NUMET), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIK), Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu na Utafiti (RAAW), Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda na Biashara (TUICO), na Chama cha Wafanyakazi wa hoteli, majumbani, huduma za jamii na ushauri (CHODAWU), pamoja na mambo mengine walihoji usiri wa serikali, hasa kutokana na hatua yake ya kushindwa kuwashirikisha wadau juu ya muswada huo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rais wa CWT, Gratian Mukoba, alipinga mchakato huo, akisema haujawashirikisha wadau ambao ni wafanyakazi.

Alisema mchakato wa kubadilisha sheria  za mafao ulipaswa kuwa shirikishi kwa kuwahusisha wenye mifuko wenyewe kupitia vyama vyao vinavyotambuliwa kisheria.

“Kinachoshangaza ni usiri mkubwa katika zoezi hili, hasa lengo la kutaka kupeleka muswada huu kwa hati ya dharura bungeni bila kutoa ushiriki wa wadau kikamilifu,” alihoji.

Alishangaa hatua ya serikali kutaka mfuko wa hifadhi ya jamii umtunze mtu asiyeweza kujitunza, yaani aliyestaafu kwa hiari na kwa mujibu wa sheria, huku ikiacha kuangalia wale wenye miaka 30 walioacha kazi, kuumwa kwa muda mrefu, au kufukuzwa kazi.

“Ina maana serikali mapenzi yake yanaanza wakati mfanyakazi akiishiwa  nguvu na siyo kwamba atalipwa kila mwezi, badala yake wanapatiwa kiasi kile kile ambacho kwa wakati huo thamani ya fedha itakuwa imeshuka,  jambo ambalo ni kumnyonya Mtanzania badala ya kumsaidia,” alisema.

Katika hilo walisema fao la kutokuwa na ajira ni takwa la mikataba ya Shirika la Wafanyakazi Duniani (ILO), hivyo litolewe bila vikwazo na kuitaka serikali isimamie mchakato huo ambao walishauri pia kwamba fao hilo lisiishie kwa wale waliopoteza ajira tu, bali lipelekwe kwa Watanzania wote wenye sifa na haki ya kuajiriwa.

Pamoja na hilo, waliwataka wabunge kusitisha majadiliano ya muswada huo unaotarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza kwenye vikao vinavyoendelea vya Bunge la Nne hadi pale serikali itakaporejesha kipengele cha fao hilo.

Akifafanua juu ya umuhimu wa fao la kujitoa, Mratibu wa kitaifa wa asasi za kutetea haki za binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema fao hilo ni muhimu kwa wafanyakazi, hasa katika asasi za kiraia, mashirika ya kiserikali, migodini, viwandani, majumbani na sekta zote binafsi, kwa kuwa ajira nyingi siyo za kudumu na ni kati ya miaka miwili hadi mitano.

“Watu wengi wanaofanya kazi katika sekta binafsi wanaacha kazi au mikataba kwisha wakiwa na umri mdogo, hivyo kutegemea fao la kujitoa kwa ajili ya kuboresha maisha yao,” alisema.

Zaidi walipendekeza wakisema kwa kuwa fao la kujitoa halitolewi tena kwa sasa, na kwamba sheria bado haijatungwa, wameitaka serikali itoe tamko mara moja la kuruhusu mafao hayo kutolewa kwa wafanyakazi ambao hawako kazini kwa sasa.

Sakata la fao la kujitoa liliibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2012, baada ya Sheria ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kupitishwa bungeni mwezi Aprili na kusainiwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Sheria hiyo, pamoja na mambo mengine, iliondoa fao la kujitoa ambalo lilikuwepo kisheria na kupitisha ile ambayo ilimtaka mfanyakazi kutochukua mafao yake hadi atakapofikisha umri wa kustaafu wa miaka 55 au 60.

Sheria hiyo ilipopitishwa iliibua mjadala kutoka kwa wafanyakazi, hasa wa sekta binafsi na ilisababisha baadhi ya makampuni na mashirika kusitisha shughuli zake na baadhi ya wafanyakazi kupoteza ajira zao.

Baadaye wabunge mbalimbali walipaza sauti zao bungeni kupinga sheria hiyo na  Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Selemani Jafo, kupeleka hoja binafsi katika kikao cha 41 cha Mkutano wa 8 cha Bunge.

Baada ya mjadala mrefu, serikali iliunda kikosi kazi kilichozunguka kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Kikosi kazi hicho baada ya kumaliza kazi yake kilipeleka taarifa yake serikalini ambapo Wizara ya Kazi na Ajira ilitoa kauli ya serikali bungeni kuwa fao hilo litaendelea kutolewa kama ilivyokuwa kabla ya mabadiliko ya sheria na pia serikali iliomba Bunge kuipatia muda ili kuleta muswada mpya wa sheria ya marekebisho ya mifuko ya hifadhi ya jamii itakayokuwa endelevu na itakayojumuisha maslahi ya wadau na kutoa wito kwa wadau kuendelea kutoa maoni yao kwa nia ya kuboresha suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles