OUAGADOUGOU, BURKINA FASO
WANASAYANSI wamegundua aina ya fangasi inayozalisha sumu ya buibui inayoweza kuua kwa haraka idadi kubwa ya mbu wanaoeneza malaria.
Majaribio yaliyofanywa katika nchi ya Burkina Faso, yameonesha kuwa idadi ya mbu ilitoweka kwa asilimia 99 ndani ya siku 45.
Watafiti walioongoza jaribio hilo walisema lengo lao ni kusaidia kumaliza tatizo la kuenea kwa malaria.
Ugonjwa wa malaria ambao unaenezwa baada ya mbu jike kunyonya damu, unaua zaidi ya watu 400,000 kwa mwaka.
Duniani kote, kuna kesi karibu milioni 219 za malaria kila mwaka.
Wakifanya utafiti huo, watafiti wa Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani na taasisi ya utafiti ya IRSS ya nchini Burkina Faso – kwanza walibaini fangasi inayojulikana kama Metarhizium pingshaense, ambayo kwa kawaida huathiri mbu aina ya Anopheles anayeeneza malaria.
Hatua iliyofuata ilikuwa ni kuingezea nguvu fangasi hiyo.
“Kwa maumbile ni rahisi kuangamizwa kwa njia hiyo,” Profesa Raymond St Leger wa Chuo Kikuu cha Maryland, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza.
“Buibui hutumia midomo yake kushika wadudu na kuchoma sumu, tukabadilisha na Metarhizium,” alieleza Profesa St Leger.
Majaribio ya maabara yameonesha kuwa fangasi iliyoboreshwa kisayansi kutoa sumu ya buibui zinaweza kuua kwa haraka mbu na kwamba inaweza kuchukua mazalia kidogo tu ya fangasi kufanya kazi hiyo.
Baada ya utafiti kufanywa katika eneo la futi za mraba 6,500 lenye mimea, wadudu na maji, vyanzo vya maji na vyakula vya mbu huko Burkina Faso, likiwa limezuiwa na neti mbili mbili kuzuia chochote kisitoke, watafiti hao walisema hatua inayofuata sasa ni kujaribu fangasi hiyo kwenye hali halisi.