FAMILIA YARIDHIA MSITU WA MWALIMU NYERERE KUHIFADHIWA

0
918
UHIFADHI: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, akiwa na viongozi wa Wilaya ya Musoma akipanda Mlima Mukendo juzi ili kujionea namna ya kuuhifadhi ikiwa ni miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa na Baraza la Madiwani la Manispaa ya Musoma kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

Na Mwandishi Wetu – Mara


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema Serikali iko tayari kutangaza katika gazeti la Serikali, kwamba msitu wa Mwalimu Nyerere uliopo Wilaya ya Butiama kuwa eneo lindwa kimazingira kutokana na ahadi iliyotolewa mwaka jana wakati wa kilele cha Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika mkoani hapa.

Kauli hiyo aliitoa mkoani hapa juzi baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na mwakilishi wa familia ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Madaraka Nyerere.

Kwa upande wake, Madaraka alisema familia itafurahi kama litatangazwa ni eneo lindwa pamoja na kuweka taratibu za matumizi sahihi ya uvunaji wa rasilimali ndani ya msitu huo na kutoa zuio kwa baadhi ya shughuli za kibinadamu isipokuwa kwa kibali maalumu.

Pia akiwa katika mwendelezo wa ziara ya kukagua masuala ya usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, January alisema lengo la kuhifadhi baadhi ya maeneo nchini ni kuhakikisha yanakuwa na usimamizi endelevu kwa manufaa ya wote.

Awali akiwa katika Manispaa ya Musoma, January alitembelea Mlima Mukendo uliopo Mtaa wa Nyerere, Kata ya Mukendo na kuridhia ombi wa Baraza la Madiwani la kuomba msitu huo uhifadhiwe kwa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004.

“Nawapongeza uongozi wa Mkoa wa Mara, wao wameenda mbali zaidi kwa kupitisha azimio hili katika Baraza la Madiwani, hii inatupa sisi msukumo wa kufanya jambo hili kwa haraka zaidi, sisi kama Serikali tutaleta rasimu ya tangazo la gazeti mapema iwezekanavyo ili tukubaliane masharti na vigezo tutakavyoweka kabla ya kulitangaza rasmi katika gazeti la Serikali,” alisema.

Katika hatua nyingine, alitoa rai kwa uongozi wa Mara haraka iwezekanavyo kupendekeza majina ya maofisa wanaofaa kuteuliwa kuwa wakaguzi wa mazingira na kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ndani ya mwezi mmoja kutoa mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira walioteuliwa na watakaoteuliwa ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Mratibu wa Mazingira Kanda ya Ziwa, isipite tarehe 30 mwezi huu kabla ya wakaguzi hawa kupatiwa mafunzo na vitambulisho,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alisema wanakusudia kutekeleza kwa vitendo kampeni ya kuufanya mkoa huo kuwa wa kijani na mikakati waliyojiwekea ni pamoja na kupanda miti milioni 10 ndani ya miaka miwili.

Katika kuunga mkono jitihada hizo, January aliahidi kutoa viriba milioni moja vyenye thamani ya Sh milioni 5.5.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here