31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

FAIDA ZA MAFUTA YA SAMAKI, WANAOPASWA KUTUMIA

SAMAKI ni moja ya chakula ambacho katika ulaji wa kila siku tumekuwa tukitumia kama mboga, lakini pia kama sehemu ya mchanganyiko katika kuandaa vyakula vya aina nyingine.

Kama sehemu ya matibabu ya magonjwa na hali mbalimbali ambazo ni matatizo ya kiafya, madaktari katika vituo vya kutolea huduma za afya wamekuwa wakiwashauri wagonjwa/wateja wao juu ya matumizi ya mafuta ya samaki.

Swali: Je, haya mafuta ya samaki yana nini hasa ambacho huyafanya yawe sehemu ya matibabu au dawa?

Siku zote tumekuwa tukifahamishwa ya kuwa ulaji wa samaki una faida nyingi za kiafya, faida hizo zimekuwa ni pamoja na kuuwezesha mwili kupata madini pamoja na virutubisho ambavyo husaidia katika kuimarisha afya zetu.

Mwili wa samaki pamoja na aina nyingine za virutubisho na madini, pia ana kiasi kikubwa cha vitamin ambazo sifa zake ni tofauti na vitamin nyingine hususani kwa namna ambayo vitamin hizi huyeyuka na kuingia mwilini mwa mlaji.

Aina ya vitamin ambazo hupatikana katika samaki ni pamoja na Vitamini A, Vitamini D pamoja na Vitamini E. Aina hii ya vitamini ni ile ambayo huyeyuka katika mazingira au kimiminika chenye asili ya mafuta.

Kutoka katika mwili wa samaki ni rahisi kupata aina hii ya vitamin pamoja na kuandaa matumizi yake ili kuja kutumika kama kinga pamoja na dawa kwa matatizo mbalimbali ya kiafya.

Jina mafuta ya samaki kwa maana halisi ni aina hii ya vitamin ambazo huyeyuka katika mafuta na katika uandaaji wake kwa matumizi hujumuisha mafuta yatokanayo na samaki.

Katika matumizi ya kinga pamoja na dawa je, mafuta haya yana umuhimu gani kwa afya yako, na ni kundi lipi la watu hupaswa kutumia mafuta haya ya samaki?

Mafuta ya samaki kwa maana ya vitamin ambazo zinapatikana katika mafuta haya (Vitamini A, D na E) husaidia kurekebisha matatizo mengi ya kiafya ambayo ni pamoja na:-

Kwa matumizi ya vitamin A, husaidia katika kuimarisha uwezo wa macho kuona ikiwa ni pamoja na nyakati za giza au usiku. Hii husaidia katika matibabu ya ugonjwa wa macho ambao huitwa ‘Ukavu macho’. Husaidia katika kuimarisha kinga ya mwili ambapo huujengea uwezo wa kupambana na magonjwa na homa ambazo huweza kumpata mtoto au mtu yeyote.

Vitamini D katika mafuta ya samaki husaidia katika kuimarisha mifupa ikiwa ni kwa kuwezesha ukusanyaji na usafirishaji wa madini ya calcium mwilini na kuijenga mifupa iliyo imara. Hii husaidia katika kuepukana na tatizo la miguu kuwa na matege na mifupa ambayo si imara.

Vitamini E husaidia katika kuimarisha afya ya ngozi, huifanya ngozi kuwa na afya imara, husaidia katika afya ya uzazi hususani kwa wanawake ambapo mafuta haya ya samaki (Vitamin E) husaidia kuimarisha ukuaji wa mimba na mtoto tumboni. Hivyo, kusaidia kuondokana na tatizo la mimba kuharibika na kutoka kabla ya kufikia umri sahihi wa mjamzito kujifungua.

Kutokana na aina hizi ya vitamin ambazo hupatikana katika mafuta ya samaki, unayafanya mafuta ya samaki yawe na matumizi ya kuukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali, kutibu magonjwa na kuuwezesha mwili kujijenga imara kiakili.

Mafuta ya samaki yanapatikana katika maumbile tofauti tofauti ya dawa kama vile vidonge laini (Capsules) pamoja na kimiminika.

Matumizi ya mafuta ya samaki hayana mipaka katika kundi au umri wa mtumiaji, watu wa rika zote kulingana na mahitaji ya kiafya wanashauriwa kutumia mafuta ya samaki ili kuweza kuimarisha afya zao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles