32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

FAIDA NA HASARA ZA KUNYWA CHAI

chai

Na MWANDISHI WETU,


 

CHAI ni kinywaji cha pili kikuu na mashuhuri duniani baada ya maji. Chai huwa na ladha za aina mbalimbali na mara nyingi hunyweka ikiwa ya moto na hata inapopoa.

Chai hulimwa zaidi katika mashamba makubwa barani Asia. Majani ya chai yanalimwa na kuchumwa katika jamii moja ya mmea, Camellia sinensis. Kisha yanakaushwa, yanafikichwa na kusagwa, au tuseme yanachakatwa ili kupata chai mbalimbali zinazotofautiana rangi na ladha.

Hizo ni pamoja na chai ya kijani (green tea), chai nyeupe (white tea) na chai nyeusi (black tea).
Inasemekana kuwa chai imetengenezwa ili kukabiliana na magonjwa ya aina zote ikiwa ni pamoja na saratani na moyo. Kiambato cha kwanza ambacho hutujia kichwani pale tunapoiwazia chai ni kile kinachotufanya tuwe macho na kutuletea uchangamfu – caffeine.
Hivyo basi, chai zote isipokuwa zile zilizoondolewa caffeine zina kiwango fulani cha caffeine ndani yake. Kwa kulinganisha na kahawa, caffeine iliyomo kwenye chai ni ndogo. Kikombe kimoja cha chai kina takribani miligramu 40 za caffeine wakati kikombe kimoja cha kahawa nyeusi kina takribani miligramu 90 za caffeine.

Kiasi kingi mno cha caffeine kinaweza kusababisha kiyangayanga (nervousness), maumivu ya kichwa, matatizo ya uyeyushaji wa chakula mwilini, na matatizo ya kurukwa na usingizi (disturbed sleep patterns).
Kiasi cha wastani cha caffeine huchangamsha ubongo wako na hupandisha presha, lakini hakisababishi zile dalili za magonjwa yatokanayo na kiasi kingi cha caffeine.
Hata hivyo, inategemea mtu na mtu, kile ambacho kwa mwingine kinaweza kuonekana cha wastani, kwako wewe kinaweza kuwa kingi mno. Ni juu yako mwenyewe kutambua uwezo wako wa kuhimili caffeine.
Majani ya chai, kwa asili pia huwa na virutubisho viitwavyo flavenoids na catechines. Virutubisho hivi inasemekana husaidia kupambana na aina zote za maradhi yanayosababishwa na vitu hatarishi vilivyo nje ya uwezo wetu kama vile saratani.
Kiasi cha virutubisho katika majani ya chai kinategemeana na kiasi cha uchakataji wa majani ya chai yanayoingia katika uzalishaji. Ndiyo sababu chai ya kijani huaminika kuwa ndio chai bora zaidi kiafya kuliko nyeusi kwa vile majani ya chai ya kijani hukusanyika haraka na huchakatika kwa kiwango kidogo kuliko majani ya chai meusi.
Kwa kifupi, kuna madai kwamba anuai vitabuni yanayohusiana na manufaa ya unywaji wa chai. Hii ni pamoja na kuboresha afya ya moyo, kuchangamsha akili (hii yamkini ikihusiana na caffeine), na hata kupunguza uzito wa mwili (hasa kwa chai ya kijani).
Tafiti zinazoonesha matokeo hayo yamefanyika maabara kwa kutumia wanyama na yapo matokeo machache mno ya tafiti zilizofanyika kwa binadamu.
Wataalamu wanashauri kuwa chai inyweke kwa kiwango cha wastani kikiwa kama kinywaji cha kalori ya kiwango cha chini ambacho kina manufaa zaidi kuliko madhara.

Chai za mizizi/mitishamba nazo huweza kutumika kwa malengo ya tiba.
Mathalani, chai ya chamonile inaweza kutumika kutuliza tumbo lililotibuka. Ila uwe makini na chai hizi za mitishamba kwani wakati mwingine unaweza usizijue zile zenye madhara ambazo zinaweza kutatiza afya nzima ya mwili. Hatuwezi kupuuzia madhara ya kijamii na kisaikolojia ya unywaji wa kinywaji ambacho ni cha halijoto na cha ladha tamu. Ni utamaduni kuwa sehemu kubwa ya watu ulimwenguni hunywa aina fulani ya chai. Chai hunyweka sanjari na maongezi, pia hunyweka pamoja na chakula cha usiku.
Katika ulimwengu wa leo chai hunyweka miongoni mwa matabaka yote ya jamii, wapo wenye kunywea kwenye migahawa, mahoteli, majumbani na hata misikitini.

Kuchanganyika na watu katika makundi ya watu wema kumethibitika kitabibu kuwa ni tiba ya kukuongezea afya ya nafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles