31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

Fahari waadhimisha siku ya matendo mema kwa kuwafariji wanafunzi Bangulo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo iliyopo Kata ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam imetoa msaada wa vifaa vya masomo na chakula kwa wanafunzi 50 waishio kwenye mazingira magumu wanaosoma katika Shule ya Msingi Bangulo.

Msaada huo unaojumuisha unga wa ugali, viatu, madaftari, sare, kalamu na penseli umetolewa na taasisi hiyo kama sehemu ya kusherehekea siku ya matendo mema duniani ambayo huadhimishwa Machi na Aprili kila mwaka.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Bangulo wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo baada ya kupatiwa misaada mbalimbali na taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo jana shuleni hapo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, amesema wanajivunia kufanya matendo mema kwa wengine kama kumbukizi ya siku hiyo.

“Tuligundua tuna majirani zetu ambao bado wana uhitaji ndiyo maana tulichagua Shule ya Msingi Bangulo kuja kuwafariji, watu wengi wana uhitaji hivyo tuguswe kuwasaidia ili jamii yetu iendelee kuwa mbele,” amesema Mchau.

Naye Katibu wa taasisi hiyo Tausi Mfaume, amesema wamekuwa wakitumia rasilimali zao wenyewe bila kutegemea wahisani na kwamba mwaka 2020 waliadhimisha siku hiyo kwa kutoa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Uviko na mwaka 2021 walishiriki kwa kupanda miti katika taasisi mbalimbali za Serikali kama vile shule, zahanati na shule za msingi.

Kwa mujibu wa katibu huyo misaada iliyokabidhiwa kwa wanafunzi hao inajumuisha viatu jozi 31, mashati ya shule 21, unga wa ugali kilo 90 uliogawiwa kwa watoto 18 huku kila mtoto akipata madaftari, peni, penseli na mikebe.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Bangulo, Catherine Chikawe, ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo na kuziomba taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mwalimu Chikawe amesema shule hiyo yenye wanafunzi takribani 3,000 ina watoto zaidi ya 100 wanaoishi kwenye mazingira magumu.

Mmoja wa wanafunzi waliofaidika na msaada huo Elisha Julius anayesoma darasa la sita amesema; “Naishukuru sana taasisi ya Fahari Mungu awabariki, nilikuwa sina viatu nakuja na yeboyebo kama unavyoniona lakini kuanzia Jumatatu na mimi nitaanza kupendeza kama wanafunzi wenzangu.

Siku ya Matendo Mema ilizinduliwa rasmi hapa nchini mwaka 2018 na tangu wakati huo imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka ikilenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii katika masuala mbalimbali kama vile umaskini, njaa, elimu, afya, mabadiliko ya tabia nchi, mazingira na nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles