25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Fahari mbioni kuanzisha shule ya msingi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo iliyopo Kata ya Gongolamboto inatarajia kuanzisha shule ya msingi ili kusaidia jamii kupata elimu bora yenye malezi mema kwa watoto.

Kwa sasa taasisi hiyo inaendesha kituo cha malezi ya watoto na shule ya awali ambayo ilianzishwa mwaka 2014.

Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Daycare Mkoa wa Dar es Salaam, Josephine Rutashobya, akizungumza wakati wa mahafali ya nane ya Kituo cha Fahari kilichopo Gongolamboto. Wapili Kulia ni Mkurugenzi wa kituo hicho, Neema Mchau na Kushoto ni Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Gongolamboto, Asumpter Nkwera.

Akizungumza juzi wakati wa mahafali ya nane ya kituo hicho, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Neema Mchau, amesema wamepata eneo Kata ya Msongola na mchakato wa ujenzi unaendelea.

“Kituo kimefikia malengo kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufungua matawi mawili ya ‘Daycare’ yaliyopo Bangulo Kata ya Pugu Stesheni na Yongwe Kata ya Chanika, na muda sio mrefu tunategemea kuwa na shule ya msingi,” amesema Mchau.

Aidha amesema kitaaluma kituo hicho kimefanikiwa kutoa elimu bora kwani wameweza kufaulisha watoto kwa kiwango cha juu na hata wanapokwenda kufanya usaili kwenye shule mbalimbali wamekuwa wakipata ufaulu wa daraja A na B.

Hata hivyo amesema wana changamoto za baadhi ya wazazi kushindwa kukamilisha michango mbalimbali kwa wakati na kusababisha kituo kutofikia malengo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo changamoto nyingine ni uelewa mdogo juu ya elimu ya awali kwa wazazi na kusababisha baadhi ya wazazi kushindwa kufahamu hatua za mtoto huku wengine wakilazimisha kupelekwa madarasa ya kati au ya juu wakati mtoto husika hana uwezo wa kusoma madarasa hayo.

Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Daycare mkoani Dar es Salaam, Josephine Rutashobya, amewataka wazazi na walezi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao ili kupunguza vitendo vya ukatili dhidi yao.

“Tunatakiwa tuongee na watoto wetu, kinamama tumekuwa ‘busy’ lakini niwaombe mpate muda wa kuongea na watoto…tupunguze ule ukali wa kuchoka watoto wetu wanaharibikiwa,” amesema Rutashobya.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Gongolamboto ambaye alikuwa mgeni maalumu, Asumpter Nkwera, amewataka wazazi kuwa makini na kuhakikisha katika kipindi hiki cha likizo watoto wanakuwa salama.

“Kila mzazi atambue wajibu wake na nafasi yake ya malezi kwa mtoto wake, ahakikishe mtoto anakuwa salama maana ulinzi na usalama wa mtoto unaanzia katika ngazi ya familia,” amesema Nkwera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles