27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Facebook yapigwa faini ya Dola bilioni 5

NEWYORK- MAREKANI

TUME ya Shirikisho la Biashara ya Marekani ambayo inashughulikia maslahi ya wateja FTC, imeipiga faini ya Dola bilioni 5 kampuni ya Facebook kwa kushindwa kulinda taarifa za watumiaji wake.

FTC ilikuwa ikichunguza tuhuma kwamba kampuni ya ushauri ya Cambridge Analytica ilipata kinyume taarifa za watu milioni 87 za watumiaji wa Facebook.

Si hilo tu pia kampuni ya Facebook ilikiri kuyapatia makampuni ya Amazon na Yahoo taarifa za watumiaji wake.

Hiyo itakuwa faini kubwa kuwahi kutolewa na tume hiyo inayoshughulikia maslahi ya wateja japo wakosoaji wanasema ni ndogo.

Kiasi hicho kinatajwa kuwa ni robo ya faida inayotengenezwa na kampuni ya Facebook kwa mwaka.

Ripoti za vyombo vya habari zinasema, faini hiyo iliungwa mkono na chama cha  Republican na kupingwa na Democrats kwa kura 3-2.

Kutokana na uamuzi huo  bei ya hisa za Facebook ilishuka kwa asilimia 1.8 juzi.

Facebook  na FTC  waliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba hawana cha kusema juu ya ripoti hizo.

Mapema mwaka huu, Facebook ilisema kuwa ilitenga dola bilioni 3 kwa ajili ya kesi zinazohusiana na ‘data’ za watumiaji na kwamba inatarajia kulipa hadi dola bilioni tano.

UAMUZI WA FTC

Tume hiyo FTC, ilianza kuichunguza Facebook Machi 2018 baada ya kuwapo kwa ripoti kwamba Cambridge Analytica  imechukua taarifa na mamilioni ya watumiaji wake.

Uchunguzi huo ulijikita kuangalia iwapo Facebook ilikiuka makubaliano ya 2011 ambayo yanataka watumiaji wajulishwe kama wanaweza kutoa idhini ya kushirikisha wengine taarifa zao.

Gazeti la The New York Times liliripoti kuwa chama cha Democrats walitaka kampuni hiyo ipewe onyo kali wakati wana Democrat wengine  walikosoa faini hiyo wakisema ilikuwa ni ndogo.

“FTC ikiwa haiwezi au haitaki kufikia mahali pa kuhakikisha faragha na taarifa zinalindwa, ni muda wa Bunge kuchukua hatua,” alisema Seneta  Mark Warner.

Faini hiyo iliyoidhinishwa na FTC inatakiwa kupitishwa na Idara ya Sheria inayoshughulikia masuala ya ndani na haijulikani ni muda gani hatua hiyo itachukua.

Pamoja na kwamba faini hiyo inatajwa kuwa ni kubwa imefikia kwenye makadirio yale yale ambayo Facebook iliyaona mapema mwaka huu  ambapo ilikaririwa ikisema inatarajia kupigwa faini inayofikia dola bilioni 5.

Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa uamuzi huo utaifanya Facebook kuchukua hatua zaidi kama kuongeza ulinzi kwenye taarifa za watumiaji wake.

KASHFA YA CAMBRIDGE ANALYTICA

Cambridge Analytica ilikuwa ni kampuni ya  Uingereza inayotoa ushauri wa kisiasa ambayo ilichukua taarifa za mamilioni ya watumiaji wa Facebook.

Baadhi ya taarifa hizo zilidaiwa kutumika kisaikolojia kuwaelezea wapiga kura wa Marekani  na kuwalenga kusaidia kampeni za urais wa Donald Trump mwaka 2016.

Taarifa za watumiaji wa Facebook zilichukuliwa kupitia chemshabongo ambayo iliwaalika watumiaji kujua hali yao ya utu.

Kama ilivyokuwa kawaida kwa ‘Application’ na michezo mingine ya wakati huo, chemshabongo hiyo iliundwa kwa ajili ya kuvuna taarifa si tu za watumiaji hao bali pia za marafiki zao.

Facebook iliwahi kusema kuwa inaamini taarifa za watumiaji wake karibu milioni 87 zilichukuliwa kinyume  na kampuni hiyo.

Kashfa hiyo ilisababisha chunguzi nyingi kufanyika duniani.

Oktoba, Facebook ilitozwa faini ya Euro 500,000  na taasisi ya Uingereza inayolinda taarifa za watumiaji.

Taasisi hiyo ilisema kuwa Facebook iliacha uvujaji mkubwa wa taarifa kinyume na sheria zake.

Taasisi kama hiyo ya nchini Canada mapema mwaka huu nayo iliinyooshea kidole Facebook ikisema ilifanya makosa makubwa  kwa sheria zake za faragha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles