Na Sheila Katikula,Mwanza
Wafanyabiashara wanaosafirisha mafuta ya Petroli kwa njia boti (mashua) kwenda visiwani wametakiwa kuacha kubeba abiria kwenye boti ambayo imebeba bidhaa hiyo ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea.
Akizungumza na Mtanzania Digital kwenye mahojiano maalum juu ya njia bora ya kusafirisha mafuta kwenda visiwani bila kuathiri mazingira ya Ziwa Victoria, Meneja wa Kanda ya ziwa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), George Mhina amesema kila mfanya biashara ambaye anasafirisha mafuta ya petroli kwa usafiri wa boti anawajibu wa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na EWURA.
Mhina amesema wafanyabiashara hao wanawajibu wa kuzingatia sheria na kanuni za usafirishaji wa mafuta zilizowekwa kulinda ubora wa mafuta na mazingira.
“Hakikisheni mnasafirisha mafuta ya petro kwenda visiwani kwa tahadhali zote katika kuhifadhi kwa kutumiwa vyombo vizuri vyenye usalama.
“Vifaa bora vya kusafirisha mafuta hayo ni mapipa ya chuma na siyo ya plastiki kama inavyofanyika hivi sasa kwani yanapitisha mionzi ya jua na inaathiri ubora wa mafuta,” amesema Mhina.
Amesema serikali kupitia bajeti 2022/23 imepitisha sheria na kutenga fedha ili kuwawezesha wananchi waweze kujanga vituo vya mafuta vya bei nafuu hasa maeneo ya vijijini kwani itasaidia kuondoa uchafuzi wa mazingira ikiwemo ziwa victoria.
Amesema kwa mjibu wa sheria, kituo cha mafuta cha bei nafuu kinaweza gharimu Sh milioni 40 tofauti na vya mjini vinaweza kugharimu zaidi ya Sh milioni 200.
“Serikali imetenga karibu Sh bilioni 2 kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kutoa mikopo ya ujenzi wa vituo vya mafuta vya bei nafuu vijijini ili kuepuka uuzaji wa mafuta kiholela kwenye madumu.
“Tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi mara kwa mara ili waache kupanda boti ambazo zinabeba mafuta ya petroli na abiria kwa pamoja ili kuepuka majanga yanayoweza kujitokeza,”amesema Mhina.