31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

EU yaipa miezi minne Kenya iishawishi Tanzania

Balozi wa EU nchini Kenya, Stephano A Dejack.
Balozi wa EU nchini Kenya, Stephano A Dejack.

NAIROBI, KENYA

BUNGE la Ulaya (EU) limesogeza kwa miezi minne hadi Februari 2, 2017 kwa Kenya kuendelea kuuza bidhaa zake Ulaya bila ushuru ili izishawishi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hasa Tanzania kusaini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kibiashara (EPA).

Hatua hiyo, inatokana na kile lilichoeleza dhamira iliyooneshwa na Kenya kuhakikisha makubaliano hayo baina ya Umoja wa Ulaya (EU) na EAC yanasainiwa baada ya taifa hilo na Rwanda kutangulia kuyasaini mjini Brussels, Ubelgiji mwezi uliopita.

Licha ya kuwa Kenya na Rwanda zilishasaini, mkataba huo sharti usainiwe na mataifa yote ya EAC ili Kenya iendelee kunufaika na soko hilo.

Wakati Uganda ikionesha nia ya kusaini, Tanzania kupitia kikao cha hivi karibuni cha wakuu wa mataifa ya EAC kilichofanyika mjini Dar es Salaam iligoma ikitaka muda zaidi kupitia makubaliano hadi Januari 2017 kutokana na wasiwasi wa kuathiri mapato na kuvuruga mpango wake wa kuwa taifa la uchumi wa viwanda.

Mkataba huo ambao pamoja na mambo mengine ungeruhusu bidhaa kutoka EU kuingia soko la EAC bila kizuizi, uligomewa pia na Burundi kutokana na vikwazo ilivyowekewa na EU.

Kufuatia mgomo wa Tanzania na Burundi, bidhaa za Kenya kama taifa linalohesabiwa kuwa la uchumi wa kati zilikuwa zianze kutozwa ushuru ifikapo Oktoba Mosi mwaka huu, kitu ambacho kingezipunguzia ushindani na kuathiri uchumi wake.

Kati ya nchi sita wanachama wa EAC ni Kenya, ambayo haiko kwenye kundi la mataifa yenye maendeleo duni na hivyo ni pekee, ambayo ingetozwa ushuru kufikia kipindi hicho.

Balozi wa EU nchini Kenya, Stephano A Dejack alikiri Umoja huo umeipa nafasi Kenya hadi Januari 2017 badala ya Oktoba Mosi kuhakikisha EPA imesainiwa na nchi zote.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Bunge la Ulaya walisema Kenya imepewa hadi Februari 2, 2017 kuzishawishi nchi wanachama wa EAC kusaini EPA ili iendelee kuuza bidhaa zake bila ushuru.

Kenya ina soko kubwa Ulaya hasa kwa bidhaa za maua, samaki, nguo, kahawa, chai na njegere.

Hata hivyo, kutokana na hofu kuwa huenda Tanzania ikaendeleza msimamo wake kipindi cha miezi minne ijayo, Kenya imeanza kujadili uwezekano wa kuruhusu nchi wanachama kusaini mkataba kwa nyakati tofauti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles