NYOTA wa zamani wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o, ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa klabu ya Antalyaspor ambayo inashiriki ligi ya nchini Uturuki.
Nyota huyo alijiunga na klabu hiyo Juni, mwaka huu, akiwa kama mchezaji wa kawaida, lakini kwa sasa amepewa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa muda akichukua nafasi ya kocha Yusuf Simsek.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye aliwahi kukipiga katika klabu ya Chelsea, alisaini mkataba wa miaka mitatu kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo kama mchezaji tangu Juni mwaka huu, lakini baada ya kocha mkuu, Simsek kuondoka, klabu hiyo imeamua kumpa jukumu mchezaji huyo kuwa kocha mkuu.
Rais wa klabu hiyo, Gultekin Gencer, aliliambia gazeti la DHA la nchini humo kwamba, wamekaa na Eto’o na kumpa jukumu hilo na wamekubaliana.
“Tulikaa pamoja na Eto’o na mkurugenzi wa ufundi Mehmet Ugurlu na kukubaliana kwamba wachukue majukumu ya kuifundisha timu kwa kipindi hiki hadi pale atakapopatikana kocha mpya na tumekubaliana hivyo.
Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Cameroon, Patrick M’Boma, amesema Eto’o alikuwa na nia ya kuja kuwa kocha mara baada ya kustaafu soka, hivyo atakuwa na furaha kubwa kuanza kupata uzoefu.
“Najua kwamba alikuwa na wazo hilo tangu zamani kuja kuwa kocha, aliwahi kuniambia hivyo miaka mingi iliyopita, lakini kwa sasa amepata nafasi hiyo huku akiwa hana uzoefu wa kufundisha, inawezekana akaja kuwa kocha mzuri lakini sina uhakika.
“Ana mwonekano wa kuwa kocha na ana uelewa, lakini sina uhakika kama atafanya vile ambavyo watu wanatarajia kuona, kikubwa ni kuangalia mapungufu yaliyopo katika klabu hiyo na kuyatendea kazi, hapo atakuwa anafanikiwa,” alisema M’boma.