NA ELIAS MSUYA, ZANZIBAR
KIKAO cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoketi jana mjini Unguja, Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, kilitawaliwa na mjadala wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, imeelezwa.
Akizungumza jana jioni baada ya kikao hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na Akaunti ya Tegeta Escrow, maadili ya viongozi na uchaguzi ndani ya chama hicho.
“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imekuwa na kikao chake cha siku moja hapa Kisiwandui chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, kama mlivyoona kimekuwa kikao kirefu na kimezungumza mambo mengi ambayo mengi yalikuwa yakitarajiwa likiwamo la Escrow, ratiba ya uchaguzi ya chama chetu na hali ya kisiasa,” alisema Nape.
Hata hivyo, alisema leo atatoa ufafanuzi wa kina wa kile kilichojadiliwa katika kikao hicho.
“Yapo mambo mengi, nadhani nikae chini niandike ripoti na nitaeleza kesho (leo) saa tatu asubuhi… ajenda ya hali ya kisiasa ilichukua muda mrefu karibu saa 8, kwa sababu ilibeba mambo yanayotokea nchini yakiwamo hayo ya Escrow, mambo ya viongozi na yanayohusu wananchi,” alisema Nape.
Kikao hicho kilichodumu kwa saa nane, kilianza saa 6 mchana, baada ya Rais Kikwete kuingia katika ofisi ya Kisiwandui na kupokewa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Vuai, Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Asha-Rose Migiro na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape.
Awali akimkaribisha Rais Kikwete, Kinana alisema kikao hicho kilipaswa kuwa na wajumbe 34, lakini wawili ambao ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Sophia Simba hawakuhudhuria.
Profesa Tibaijuka, alivuliwa wadhifa wake wa uwaziri kutokana na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya kukiri kupokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemarila.
Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 22, 2014, Rais Kikwete alisema amemwondoa Tibaikuka katika wadhifa wake na atatafuta mtu mwingine wa kumrithi.
Hata hivyo, Rais Kikwete alimweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, huku akisema watendaji wengine wa Serikali watawajibishwa na mamlaka husika.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alijiuzulu mapema kabla ya kuwajibishwa, huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi akisimamishwa kazi na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.
Awali kulikuwa na taarifa za kuwawajibisha baadhi ya makada wa chama hicho waliokiuka kanuni za kuwania urais.
Miongoni mwa waliotajwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa huku wengi wakibashiri kuenguliwa kwa jina lake katika kinyang’anyiro hicho.
Taarifa pia zilieleza kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Shein ndiye anayetajwa kupitishwa kugombea urais wa Muungano ili kukata mzizi wa fitina wa makundi ya wagombea urais.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM ilitoa pongezi kwa Katibu Mkuu, Kinana kwa utendaji wake na ziara zake za kuimarisha chama.
“Kamati Kuu imepongeza ushindi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, pia imeipongeza Kamati Maalumu ya Maadili chini ya (Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara, Philip) Mangula kwa kuwabana na kuwarekebisha wagombea watarajiwa wa urais.
“Pamoja na hilo, pia imesifu na kupongeza mwenendo wa wahusika kwa sasa na kuwaona wanafuata taratibu za chama. Hakukuwa na mjadala mkali kama ilivyotarajiwa,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema katika kashfa ya Escrow ambayo imewang’oa baadhi ya watendaji wa Serikali, Kamati Kuu ilimpongeza Rais Kikwete kwa hatua zake za kushughulikia suala hilo na anavyoendelea nalo.
Pamoja na hilo, Kamati Kuu imeiagiza Sekretarieti ya CCM kufanya maandalizi kabambe ya kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu kwa kutoa ripoti mara kwa mara juu ya mikakati inayoendelea.
“Haya ndiyo makubwa, kikao hakikuwa na mjadala mkali, kilitawaliwa na busara,” kimesema chanzo hicho.