28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Escrow ngoma bado mbichi

Barack-ObamaNa Elias Msuya
SERIKALI ya Marekani imeendelea kuichunguza Tanzania kama inakidhi vigezo vya kupewa msaada wa Shirika la Msaada wa Maendeleo la Marekani (Millennium Challenge Corporation- MCC) unaofikia Dola za Marekani milioni 700, sawa na Sh trilioni 1.3.
Tathmini hiyo imeendelea kufanyika wakati nchi ya Ghana ikiwa tayari imeshapata msaada wake, huku Tanzania ikikabiliwa na harufu ya ufisadi unaokwamisha kupitishwa kwa msaada huo.
Taarifa hizi mpya zimepatikana baada ya kikao kilichofanyika Washington DC Februari 27, mwaka huu, kati ya Makamu wa Rais wa MCC, Kamran Khan na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Liberata Mulamula, ambapo pamoja na masuala mengine, imeamriwa kuwa Bodi ya MCC itakutana kwa mara ya mwisho Septemba, ili kuamua kama Tanzania ipewe msaada au isipewe.
“Kikao cha bodi cha mwezi Machi hakiwezi kuwa cha kufanya uamuzi wa kuipatia Tanzania msaada mpaka kile cha mwezi Septemba 2015, ambacho kitafanya tathmini,” linaeleza andishi lililotunza kumbukumbu ya kikao kati ya Khan na Liberata.
Khan alisema kuwa kikao hicho kilikuwa ni muhimu ili kufanya tathmini sahihi ya yale ambayo walikubaliana na Tanzania, hasa katika masuala yanayohusu ufisadi kabla ya kikao cha bodi cha Machi, mwaka huu.
Ni katika mwenendo huo huo wa kuifuatilia Tanzania, hivi karibuni Makamu wa Rais wa MCC, Kamran Khan na Makamu Rais wa Sera na Tathmini, Beth Tritter, walifanya ziara nchini kwa lengo la kutathmini kama Tanzania imekidhi vigezo vya kupewa awamu ya pili ya msaada wa MCC.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo ambayo MTANZANIA Jumamosi imeiona, Khan na Tritter waliwasili nchini Machi 1. Khan na Tritter ambao kesho yake baada ya kuwasili (Machi 2) walikutana na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress na msaidizi wake, Virginia Blaser, kabla ya kupata taarifa ya mradi wa ‘Power Team Africa’, inaelezwa baada ya kupata maelezo kuhusiana na uchunguzi unaoendelea kuhusiana na kashfa za ufisadi, ikiwemo suala la uchotwaji fedha katika akaunti ya Escrow, bado wameonekana kutoridhishwa na hatua ambazo serikali imezichukua.
Imebainika kuwa katika ziara hiyo ambayo pia ilikuwa na lengo la kupata picha juu ya kile ambacho kitafanyika kuhusiana na mchakato wa maoni ya Katiba mpya pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, viongozi hao walikutana na mjumbe wa MCC na Balozi Childress.
Pia walikutana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, Mkurugenzi wa Tanesco, Felichesmi Mramba, Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Felix Ngamlagosi, Mratibu wa Taifa wa Akaunti ya Maendeleo ya Milenia (MCA) na wengineo.
Siku hiyo pia Khan na Tritter walitembelea makao makuu ya MCA katika jengo la Shirika la Maendeleo (NDC), kabla ya kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, kwa lengo la kusikia vipaumbele vya kamati hiyo, hasa katika gesi asilia. Baadaye walimaliza ratiba ya siku kwa kufanya mkutano na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Ikulu.
Ratiba yao inaonyesha kuwa Machi 3 walikutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ili kupata taarifa za sakata la IPTL na Akaunti ya Escrow kwa ujumla na baadaye walipata chakula cha mchana na wawakilishi wa Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo ya Sweden (Sida), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na wawakilishi wa Norway ili kusikia mikakati yao katika sekta ya nishati.
MCC inafadhili miradi mbalimbali, ikiwemo ya maji, barabara na nishati.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alipoulizwa na gazeti hili alikiri kukutana na Khan na Tritter kwa lengo la kutathimi vigezo vya Tanzania kupata msaada wa awamu ya pili wa MCC ambazo ni kiasi cha Dola za Marekani 700 milioni (Sh 1.3 trilioni).
“Ni kweli Khan alikuja na tumezungumza na mapendekezo yetu ameyapeleka kwenye Bodi ya MCC,” alisema Mkuya.
Alipoulizwa kama MCC wameridhishwa na hatua za Serikali katika utawala bora na hasa kashfa ya Escrow, Mkuya alisema:
“Hayo sasa ni yako, ila mimi najua wameridhishwa na hatua za Serikali hata katika hilo suala la Escrow. Hizi ni hatua za kawaida tu katika kupata huo msaada. Tunategemea utakuwa tayari ifikapo Septemba,” alisema Mkuya.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sumve ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, alikiri kukutana na Khan.
“Nani kakupa hizo taarifa?” alihoji Ndassa, akionyesha kushtuka, kisha akaendelea: “Niambie chanzo chako ili nikusaidie… La msingi walitaka kujua maendeleo ya awamu ya kwanza msaada wa MCC kwa kuwa tunakwenda kwenye awamu ya pili (MCC Compact 2) hasa kwa upande wa umeme,” alisema Ndassa na kuongeza:
“Walituuliza wabunge kama tumeridhishwa na msaada wa MCC na jinsi Serikali inavyochukua hatua. Tumesema tumeridhika kwa kuwa Bunge limechukua hatua… si unajua yalitolewa mapendekezo? Utawala nao umechukua hatua ya kuwasimamisha mawaziri na watendaji wa Serikali na Mahakama nayo inafanya kazi; kwa sasa unaona Baraza la Maadili linaendelea kuwahoji wahusika.”
Escrow bado mbichi
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alisema bado Tanzania haijakidhi vigezo vya kupewa msaada wa MCC.
Katika ujumbe wake mfupi wa simu, Kafulila, aliyeibua sakata la Escrow bungeni mwaka jana, alisema kipengele kilichoguswa katika sakata hilo kinahusu watu waliopewa fedha na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemarila.
“Tanzania bado haijakidhi vigezo vya MCC, Ghana wenzetu wameshaanza kupata fedha hizo. Kikubwa kichozuia bodi ya MCC kuamua ni namna ambavyo Serikali inavuta miguu kuchukua hatua kuhusu ufisadi wa Escrow,” alisema Kafulila na kuongeza:
“Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa ni kwa watu waliohusishwa na Rugemarila (James) ambaye alifaidi asilimia 30 tu. Bado waliofaidi kupitia Harbinder Singh Sethi (Mwenyekiti Mtendaji wa Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP) aliyepata asilimia 70 ya fedha zote.”
Kafulila alisema nchi za Ulaya zinajua kwa kina suala hilo kuliko Watanzania.
“Bila shaka majasusi wa Ulaya na Marekani wanajua hata kilichomo ndani ya ripoti ya PCCB (Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa,” alisema na kuongeza:
“Hili huenda likaigharimu nchi nchi kwa miaka mingi kama ufisadi wa Goldenberg ulivyovunja uhusiano wa Kenya na nchi za Magharibi.”
Desemba 2014, Bodi ya Wakurugenzi ya MCC ilionyesha wasiwasi wao kuhusu kukithiri kwa rushwa nchini, hasa kesi ya hivi karibuni ya IPTL.
“Kwa miaka saba iliyopita, Bodi imegundua Tanzania imeshindwa kudhibiti rushwa (rushwa inaongezeka) kwa mujibu wa vipimo vya jitihada ya kupambana na Rushwa,” ilisema taarifa ya bodi hiyo na kuongeza:
“Wakati Bodi imekubali kuiruhusu Tanzania iendelee kuandaa mapendekezo yake, ila ni muhimu Serikali ya Tanzania ionyeshe kuchukua hatua suala la rushwa kabla ya fedha kutolewa.”
Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, hakuwa tayari kuzungumzia ripoti ya taasisi yake, hasa kwa asilimia 70 za mwamala ulioihusisha kampuni ya PAP.
“Siwezi kuzungumzia suala hilo… niko msibani, siwezi kuzungumzia masuala ya kazi,” alisema Dk. Hosea na kukata simu yake.
Mbali na Marekani, hivi karibuni nchi wahisani wanaofadhili bajeti walisema hawajaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kashfa ya akaunti ya Escrow.
Nchi hizo zilitoa Sh 25.8 bilioni kati ya Sh 959 bilioni wanazopaswa kutoa kwa kile walichosema bado hawajaridhishwa na hatua za Serikali katika utawala bora.
Hatua za Serikali
Sakata la akaunti ya Escrow liliibuliwa bungeni mwaka jana na baada ya kujadiliwa kwa urefu, Bunge lilitoa mapendekezo ya kuwawajibisha mawaziri na watendaji wa Serikali.
Waliowajibika ni pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, huku Rais Jakaya Kikwete akimfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na baadaye aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa amemweka kiporo.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Kwa upande wa Mahakama, baadhi ya watendaji wa Serikali wamefikishwa mahakamani, akiwemo Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Julius Angelo, Ofisa Mwandamizi wa TANESCO, Steve Urassa na Leonard Lutabingwa wa TRA.
Mbali na mahakamani, Baraza la Maadili ya Watumishi wa Umma chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Hamisi Msumi, limewahoji watumishi wa Serikali waliopokea fedha kutoka kampuni ya VIP Engineering. Waliohojiwa ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko na Mnikulu, Shaaban Gurumo.
Baadhi ya wabunge walihusishwa na kashfa hiyo, akiwemo Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, aliyekata rufaa Mahakama Kuu akipinga kuhojiwa.
Wengine ni Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Hivi karibuni CCM imetangaza kuwatema wabunge hao kushiriki kwenye vikao vya maamuzi, yaani Halmashauri Kuu na Kamati Kuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles