ESCROW, MAKINIKIA ZILIVYOFUNIKA MJADALA WA BAJETI

0
421
Na EVANS MAGEGE,

SAKATA la ukwapuaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa BoT ambalo limeibuka kwa mara ya pili kivingine, linatafsirika kusindikiza mjadala wa mchanga wa madini (makinikia) ambao kwa kiasi kikubwa si tu ulitikisa, bali ulifunika mchakato mzima wa kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

Mtazamo wa hoja hiyo unajengwa kwa msingi wa uzito wa mijadala yote mitatu ambayo imefuatana kwa matukio, hasa ya mijadala miwili kati ya hiyo iliingiliana kwa maana ya muda na kusababisha mjadala mmoja kuumeza mwenzake.

Mijadala iliyoingiliana na kusababisha mmoja kuumeza mwingine ni ule wa kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2017/18  na Ripoti ya Pili ya Uchuguzi wa Mchanga wa Madini (makinikia).

Ikumbukwe kuwa, majadiliano ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali bungeni yalianza Juni 12, mwaka huu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani  kuwasilisha mapendekezo yao, lakini nje ya Bunge kusudio hilo likajikuta linaathiriwa kama si kufunikwa kabisa na tukio la uwasilishaji wa ripoti ya pili ya makinikia ambalo ni dhahiri lilionekana si tu kugawa mtazamo wa jamii juu ya mambo hayo mawili, bali uliweza kuteka mjadala wa bajeti, hivyo mjadala mkuu ukahamia kwenye makinikia na kudumu kwa takribani wiki moja.

Wakati mjadala wa makinikia ukiwa bado umetawala miongoni mwa jamii kwa wiki nzima, sakata la Tegeta Escrow nalo likaibuka kivingine na kuibua mjadala mkubwa hadi sasa.

Kuibuliwa kivingine kwa sakata hilo kumetokana na kitendo cha  Serikali kupitia Taasisi yake ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwakamata na kuwafikisha mahakamani mmiliki wa Kampuni ya Pan Afrika Power-PAP, Harbinder Sethi Singh na mfanyabiashara James Rugemalira kwa tuhuma za uhujumu uchumi.

Harbinder na Rugemalira walifikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Jumatatu ya wiki hii ikiwa ni siku moja kabla ya Bunge kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

Hadi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linapitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2017/18 Jumanne wiki hii,  mjadala wa Escrow ulikuwa umetawala sehemu kubwa ya jamii, hivyo suala la bajeti kuu likajikuta  linapita pasipokuteka hisia za watu ukilinganisha na bajeti za nyuma.

Kupitishwa kwa makadirio hayo kunaimarisha msingi wa kiasi cha Sh trilioni 31 cha fedha zinazokadiriwa kukusanywa, kutumiwa na Serikali kwa mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai Mosi, mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa, kuelekea kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali, tayari wabunge wa upinzani, walikuwa wamejiandaa kuikosoa bajeti hiyo katika maeneo mbalimbali, hasa uamuzi wa Serikali kuhamishia ada ya leseni ya magari (Road License) kwenye mafuta, hatua ambayo wanadai itawaongezea mzigo wananchi wa kawaida, huku wengi wao wakiwa hawamiliki magari.

Pamoja na wabunge wa upinzani kujipanga kwa ajili ya mjadala wa bajeti, nguvu ya hoja zao ilijikuta ikimezwa na ukubwa wa mjadala wa ripoti ya pili ya madini, ambayo ilionekana kutawala makundi mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari kwa takribani wiki nzima(Juni 12-17).

Ingawa awali baadhi walidai kwamba ripoti hiyo isingeweza kuathiri mwenendo wa mjadala wa jambo kubwa kama bajeti ambalo linawagusa watu wengi, hata hivyo hoja bado ilikuwa na msingi wa hofu kwa kuangalia jinsi ripoti ya kwanza iliyowasilishwa na Kamati ya Wanasayansi, Mei mwaka huu na kuibua mjadala mkubwa.

Kumbukumbu hiyo ilijengwa kwa hoja si tu kwa sababu kamati ya wanasayansi ilibaini kiwango kikubwa cha madini kilichomo katika mchanga unaosafirishwa nje ya nchi, bali uamuzi mgumu uliofanywa na Rais Magufuli dhidi ya watendaji wa juu kwenye taasisi zinazohusika moja kwa moja na masuala ya madini.

Kwa muktadha wa ripoti ya kwanza, ambayo ilishuhudia Rais Magufuli akiwaondoa madarakani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na baadhi ya viongozi wa Mamlaka ya Kudhibiti Madini Tanzania (TMAA), macho na masikio ya wengi yalijielekeza kusikia nani atasalimika katika safari hii na nani hatasalimika.

Ikumbukwe kuwa, wakati wa mjadala wa taarifa ya kwanza ya uchunguzi wa makinikia, Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, aliandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii uliosomeka; “Tulikosea njia tulipopitisha sheria ya madini ya mwaka 1998 iliyofanya mikataba iwe na nguvu zaidi kuliko sheria, tukajifunga pingu. Nani wa kumlaumu?”

Hoja kama hiyo pia ilizungumzwa na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Tundu Lissu, ambaye amekuwa akihoji matatizo ya mikataba ya madini, ikiwamo sheria ya madini ya mwaka 1998, ambayo Serikali iliipeleka bungeni kwa hati ya dharura na kupitishwa ndani ya siku moja.

Ndani ya mitazamo au hisia za kile kinachoitwa hitilafu za kisheria ambazo zimesababisha taifa kuwa na mikataba mibovu ya madini, majina ya waliokuwa wanasheria wakuu wa Serikali (AG) Andrew Chenge na Jaji Frederick Werema, yamekuwa yakinyooshewa vidole zaidi.

Chenge, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia mwaka 1993 hadi 2005, anatazamwa kuwa na ufahamu au ushuhuda wa mikataba yote mikubwa ya madini ambayo inalalamikiwa kwa sasa ambayo ilisainiwa kati ya mwaka 1994 na 2007.

Wakati Chenge akiwa AG katika kipindi cha utiaji saini mikataba hiyo, chini ya Serikali ya awamu ya tatu ya (1995 – 2005), Jaji Werema alikuwa mtaalamu wa sheria katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jaji Werema alishika nafasi hiyo mwaka 1984 hadi 2007, baadaye akawa Mwanasheria Mkuu mwaka 2009 hadi 2014, akichukua nafasi ya Johnson Mwanyika, aliyestaafu kwa lazima.

Wakati mjadala wa taarifa ya kwanza ya uchunguzi wa makinikia ukiwa bado mkubwa, gazeti la MTANZANIA katika toleo la Aprili 27, lilimkariri Chenge akishangaa kunyooshewa kidole kila mara.

Kwa upande wake, Jaji Werema alisema haoni kama kuna tatizo la kisheria katika mikataba ya madini, isipokuwa kuna watu ambao walikuwa hawafanyi kazi yao sawasawa.

Wakati hayo yakijiri, Kampuni ya Acacia nayo iliipinga taarifa ya kwanza ya kamati ya uchunguzi wa makinikia, ikidai haikuwa sahihi, zaidi ikiomba ufanyike uchunguzi huru ili kupata ukweli.

Hata hivyo siku moja baada ya Rais kukabidhiwa ripoti ya pili ya uchunguzi wa makinikia, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa Kampuni ya Acacia, Prof. John Thornton, alikuja nchini na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.

Katika mazungumzo yao walikubaliana kuwa, kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania, ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.

Siku mbili baada ya viongozi hao kufikia uamuzi huo, Kampuni ya Acacia ilifanya mkutano kwa njia ya simu na wanahisa wake ambapo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Acacia, Brad Gordon, alisema wamejipanga sawasawa kwenye kuunda timu ambayo itakuja kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania.

Gordon alisema mbali na kuunda timu, pia kampuni yao inataka kufahamu mapema timu ambayo itaongozwa na Rais Magufuli katika mazungumzo hayo pamoja na namna mazungumzo yatakavyofanyika.

Katika kuujengea msingi wa kile kinachoitwa kujipanga zaidi, Gordon aliwaambia wanahisa wa kampuni hiyo kuwa anaamini timu itakayoiwakilisha Tanzania kwenye mazungumzo hayo itaongozwa na Rais, Dk. Magufuli, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) pamoja na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Pamoja na Gordon kutoa mtazamo huo kwa wanahisa wa kampuni yake, msingi wa tatizo hilo umeshavuka ngazi moja, kinachosubiriwa kwa sasa ni kukutana kwa timu mbili za mazungumzo ya kumaliza mgogoro uliopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here