ISTANBUL, UTURUKI
RAIS wa Uturuki, Recep Erdogan, ameibuka mshindi katika kura ya maoni ya kihistoria iliyofanyika juzi, ambayo inamwongezea mamlaka zaidi.
Matokeo hayo yameiacha nchi hiyo ikigawanyika na upinzani kulalamikia udanganyifu na umejipanga kuyapinga.
Mabadiliko hayo makubwa ya Katiba yaliyoidhinishwa kupitia kura hiyo yataongeza madaraka zaidi kwa Rais Erdogan kuliko kiongozi yeyote tangu mwasisi wa Taifa, Mustafa Kemal Ataturk na mrithi wake Ismet Inonu.
Kambi ya ‘ndio’ ilishinda kwa asilimia 51.4 ya kura dhidi ya asilimia 48.6 ya ‘hapana’, Tume ya Uchaguzi ilisema katika taarifa zilizonukuliwa na shirika la habari la Anadolu.
Wakati kura hizo zikitokana na asilimia 99.5 ya masanduku yaliyohesabiwa, mwitikio wa wapiga kura ulikuwa asilimia 85.
Lakini wapinzani katika wilaya zinazompinga Erdogan za mjini hapa walionesha hasira kupinga matokeo hayo.
Mamia ya watu pia waliingia mitaani katika maeneo ya Besiktas na Kadikoy.
Kura hiyo ya maoni ilifanyika chini ya amri ya hali ya hatari ambayo imeshuhudia watu 47,000 wakikamatwa kufuatia jaribio lililoshindwa la mapinduzi dhidi ya Erdogan Julai mwaka jana.