Na Ramadhan Hassan, Dodoma
BODI ya Usajili wa Wahandisi nchini (ERB) imetaja vipaumbele vyake kwa mwaka 2022-2023 ikiwemo kuhuisha leseni za wahandisi.
Hayo yameelezwa leo Novemba 10, 2022 jijini Dodoma na Msajili wa Bodi hiyo, Mhandisi Bernard Kavishe wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Bodi ya usajili wa Wahandisi na Vipaumbele vyake kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.
“Ili Mhandisi aendelee kuwa shapu tunampa leseni na leseni ile kila baada ya miaka mitatu anabidi atuthibitishie kwamba anahuisha kwahiyo mwaka huu leseni zote zitakuwa zimefika mwisho wake na Wahandisi wanawajibika kuzihuisha,” amesema Mhandisi Kavishe.
Hata hivyo, amesema wanaendelea kuimarisha Taasisi kwa upande wa sheria zinazoongozwa na taratibu na kanuni mbalimbali.
“Tunaendelea kudumisha nidhamu,kutoa elimu,kudhibiti hisibati katika vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya ufundi sanifu,”amesema.
Vilevile,Kavishe amesema kuwa wanaendelea kupambana na vishoka wanaongilia mifumo na wanaoingilia taaluma.
“Tunaendelea kudhibiti wataalamu wanaotoka nje ya nchi lazima akija aje na ujuzi ambao sisi tunauhitaji lakini tunahakikisha kwamba utaalamu tunaoutaka uje umepita bodi kwahiyo kwajumla tunaimarisha,”amesema Kavishe.
Pia imesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 inatarajia kujenga kituo Kikubwa cha Umahiri eneo la kizota, jijini Dodoma ambapo ni moja ya vipaumbele vyake ili vijana waweze kufanya shughuli zao kwa kuonyesha ubunifu wao.
Amesema kituo hicho kitawafanya waendelee kukua lakini kitawasaidia Wahandisi kufanyakazi mbalimbali za kibunifu kwa umahiri zaidi.
Kavishe amebainisha kuwa Bodi hiyo ina Mpango wa Miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2025 yakiwemo mawili ya kitaifa.
Amesema lengo la kwanza ni kudhibiti maambukizi ya UKIMWI pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza.
“Hilo ni jukumu letu wote ili tuweze kujenga Taifa lazima tuwekeze kwenye afya,”amesema Kavishe.
Ametaja lengo la pili ni kupambana na rushwa ambapo amesema bodi hiyo ipo mstari wa mbele katika kupambana na rushwa maana yake rushwa ni adui wa uhai na kusisitiza kuwa sio tu adui wa haki bali ni adui wa uhai.
Amesema kuwa lengo mahususi la mpango huo ni kuimarisha udhibiti na utendaji kazi ya uhandisi na taaluma ya uhandisi kwasababu uhandisi hauishii shuleni bali mhandisi wanakwenda naye mpaka anapostaafu.
Kavishe ametaja lengo lingine ni kukuza na kuimarisha weledi ambapo amesema wanafanya Uimarishaji wa Taasisi yenyewe ili iweze kutoa huduma vizuri,lazima iwe imara.