31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

EPZA KINU CHA AJIRA TANZANIA

Na Ferdnanda Mbamila


AJIRA ni changamoto inayoikabili Serikali kutokana na kuwapo kwa ongezeko kubwa la wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu hususan vyuo vikuu na vyuo vinavyotoa stashahada nchini ambao wengi wao wanatamani kuajiriwa katika sekta rasmi.

Hata hivyo, Serikali inakabiliana na changamoto hii kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwamo ya kuwajengea uwezo wananchi wake kujiajiri na kuondosha dhana ya wahitimu kutegemea kuajiriwa.

Mamlaka ya EPZ ni mmoja wa wachangiaji wakubwa katika kutatua kero ya ajira kwa Watanzania kutokana na shuguhuli za uwekezaji na biashara zinazosimamiwa na EPZA kwa sababu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, imetoa ajira za kudumu 52,698 kwa Watanzania wanaofanyakazi kwenye kampuni zilizopo nchini ambazo zinamilikiwa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi, zilizopo kwenye mpango wa mamlaka hiyo.

Pamoja na kutoa ajira za kudumu na muda, EPZA imekuwa chungu cha kupika vijana wa Tanzania kwa kufundisha stadi za uzalishaji wa viwandani. Ujuzi huu huutumia kama waajiriwa wa viwandani au kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo kulingana na fani iliyojengewa uwezo.

Tofauti na shule ama vyuo vingine vya stadi za kazi na uzalishaji ambako mwanafunzi anatakiwa kulipa ada, Watanzania wanaopata nafasi ya kujifunza kwenye programu zilizopo chini ya EPZA hufundishwa bure stadi za uzalishaji na kuruhusiwa kwenda kuzalisha au kufanya ujasiriamali.

Mbali ya wanafunzi kujengewa uwezo, baadhi ya viwanda mathalani; kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku Garment huwalipa posho ya nauli na chakula wanafunzi wanapokuwa mafunzoni takribani Sh 90,000 kwa mwezi hadi wanapofuzu kushona na kuwaajiri.

Hii ni hatua kubwa inayolenga kuharakisha ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini miongoni mwa Watanzania kwa sababu vijana wengi hushindwa kuajiriwa au kujiajiri katika uzalishaji kutokana na kukosa ada ya masomo hayo. Hivyo, mamlaka hiyo inapotoa elimu hiyo bure ni msaada mkubwa kwa Watanzania wenye nia ya kushiriki katika sekta hiyo lakini hawana uwezo wa kulipia gharama za mafunzo.

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Kanali Mstaafu, Joseph Simbakalia katika mahojiano na gazeti hili anasema ajira hizo zinatokana na uwekezaji na ujenzi wa viwanda, uzalishaji viwandani, uchukuzi wa bidhaa na malighafi pamoja na shughuli  zinazoendana na viwanda (kilimo, biashara na huduma za kifedha).

Anatoa mgawanyo kampuni ambazo zinatoa ajira kisekta kuwa ni;

Kampuni 54 (38%) zimewekeza katika usindikaji mazao ya kilimo (Agro Processing); 29 (21%) zimewekeza katika uzalishaji wa nguo (Textiles); 14 (10%) zimewekeza katika usindikaji madini (Mineral Processing) na kampuni 43 (31%) zimewekeza katika uhandisi (Light Assembly & Engineering).

Anasema kati ya kampuni hizo, 59 sawa na asilimia 42% ni za kigeni, 19 sawa na asilimia 14 ni za ubia na 62 sawa na asilimia 47 ni za Kitanzania.

Bidhaa zinazozalishwa na kampuni au viwanda hivi ni mahususi kwa mauzo ya nje ambapo asilimia 80 na zaidi ya bidhaa zinazozalishwa lazima ziuzwe nje ya nchi na hivyo kuimarisha biashara ya kimataifa na nchi jirani, pamoja kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Anasema EPZA ilianzishwa Februari, 2006 na majukumu yake ni pamoja na kubainisha sekta za kipaumbele katika maeneo ya EPZ (Export Processing Zones) na SEZ (Special Economic Zones).

Majukumu mengine ni kutafuta na kumiliki ardhi ya serikali kwa ajili ya uwekezaji za EPZ na SEZ, kutenga maeneo ya biashara na uwekezaji na kujenga miundombinu ya msingi, kuhamasisha uwekezaji na kujenga miundombinu ya msingi.

Anatayataja majukumu mengine kuwa ni kutoa leseni kwa wawekezaji wa EPZ na SEZ, kusimamia uwekezaji katika maeneo maalumu ya EPZ na SEZ, kutoa huduma ya mahala pamoja kwa wawekezaji wa EPZ na SEZ.

Anasema miradi inayoendelezwa na EPZA imesambaa katika mikoa kadha wa kadha ya Tanzania ikiwamo Dar es Salaam, Kigoma, Pwani, Mtwara, Ruvuma, Mara, Singida na Tanga kwa kuitaja michache na athari za manufaa ya kichumi zitawafikia Watanzania wengi kwa wakati mmoja ili malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yawafikie walio wengi.

Kutokana na mchango mkubwa wa EPZA katika kutoa ajira na kuimarisha biashara ya kitaifa ni budi kuijengea uwezo na kuimarishwa kama taasisi ili kuweza kutekeleza majukumu  yake ambayo yatachangia  kuliwezesha  Taifa kufikia azma na malengo yake ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi endelevu wa viwanda.

Uendelezwaji wa sekta ya viwanda ambavyo vinaendana na biashara utafungua fursa nyingi za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuendeleza matumizi ya bandari na reli kwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika nchi za maziwa makuu na Afrika kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles