
BARCELONA, HISPANIA
KOCHA wa timu ya Barcelona, Luis Enrique, amesema hatolaumu kiwango cha wachezaji wake baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa timu iliyopanda daraja msimu huu, Deportivo Alaves katika Uwanja wa Nou Camp, Barcelona.
Enrique alibainisha kuwa uwezo wa wapinzani wao ulikuwa wa hali ya juu kutokana na kutumia mbinu iliyowabana na kushindwa kupata bao.
Hata hivyo, Enrique alisema alipata mshtuko baada ya timu hiyo iliyopanda daraja kuwafunga mabao hayo wakiwa uwanjani humo.
Katika mchezo huo, kocha huyo aliwaweka benchi wachezaji wake mahiri, Lionel Messi na Luis Suarez wakisubiri mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya timu ya Celtic utakaochezwa wiki ijayo.
Kocha huyo alimwanzisha Neymar Jr ambaye alirejea katika michuano ya Olimpiki yaliofanyika jijini Rio de Jeneiro, Brazil.
Mbali na Mbrazili huyo, Enrique alikuwa akitambulisha wachezaji wapya akiwamo Ibai Gomez ambaye hakuwa na mafanikio mazuri katika mchezo huo.
Enrique alithibitisha kwamba kocha wa timu ya Deportivo Alaves, Mauricio Pellegrino, alifanikiwa kimbinu.
“ Tunastahili lawama lakini kwa upande wetu tulikuwa hatuna namna ya kupata ushindi kutokana na ubora wa wapinzani wetu.
“Katika suala zima la ushindi inategemea na kiwango cha wachezaji tegemezi , lakini baada ya kufungwa anayelaumiwa ni kocha,” alisema.
Kocha huyo alidai kwamba anastahili lawama zote na kuahidi kurekebisha makosa yaliyojitokeza baada ya kushuhudia timu yake ikipata kipigo hicho.
“Mimi ni kiongozi wa kilichotokea, mabadiliko yaliyofanyika ndio chanzo cha kupata matokeo mabovu, hata hivyo nitajitahidi kukiboresha kikosi changu,” alisema Enrique.