England, Nigeria wamgombania Abraham

0
841

LONDON, ENGLAND

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Chelsea, Tammy Abraham, ameweka wazi kuwa, hadi sasa hajafanya maamuzi juu ya kulitumikia taifa gani kwenye michuano mikubwa kati ya England na Nigeria ambapo kila taifa linamuhitaji.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22, amekuwa na mchango mkubwa ndani ya klabu ya Chelsea msimu huu ikiwa mchezo wa juzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Lille akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-1.

Mshambuliaji huyo alizaliwa Camberwell jijini London, lakini ana asili ya nchini Nigeria. Hata hivyo tangu akiwa na umri wa miaka 18 amekuwa akiitumikia timu ya taifa England ya vijana na sasa ni wakati wa kufanya maamuzi ya kuchagua alitumikie taifa gani.

Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate, yupo kwenye mipango ya kumuita mchezaji huyo katika kikosi chake mwezi huu kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya kufuzu Euro 2020 dhidi ya Jamhuri ya Czech na Bulgaria, lakini Abraham amesisitiza kuwa hadi sasa hajafanya maamuzi ya nchi ya kuitumikia.

“Ni jambo la furaha sana kuona nchi zote zinakuhitaji, ukweli ni kwamba ninazipenda nchi zote, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia hilo, ila kikubwa ambacho ninakiangalia ni jinsi gani ninaweza kuisaidia timu yangu ya Chelsea, ila muda utafikia na kila kitu kitakuwa wazi,” alisema mchezaji huyo.

Mchezaji huyo ndani ya klabu ya Chelsea kwa sasa anaanza kufananishwa na nyota wa zamani wa timu hiyo Diddier Drogba kutokana na uwezo wake, hivyo wanaamini atakuwa kuwa na msaada mkubwa kwa kipindi kijacho kutokana na umri wake kuwa mdogo.

Timu ya taifa England itashuka dimbani Oktoba 11 dhidi ya Jamhuri ya Czech kabla ya siku tatu mbele kukutana na Bulgaria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here