33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

England kumpa Allardyce mikoba ya Hodgson

Sam Allardyce
Sam Allardyce

LONDON, ENGLAND

CHAMA cha Soka nchini England, FA, kinatarajia kumtangaza kocha mpya wa timu hiyo, Sam Allardyce, kuchukua nafasi ya Roy Hodgson.

Allardyce ni kocha wa klabu ya Sunderland ya nchini England, lakini timu hiyo ya Taifa imekuwa ikihangaika kumtafuta mbadala wa Hodgson na inadaiwa kuwa tayari Allardyce amefikia makubaliano ya awali, hivyo muda wowote wanaweza kumtangaza.

Hodgson alijiuzulu kuitumikia timu hiyo baada ya England kutolewa kwenye michuano ya Euro 2016 katika hatua ya 16 bora dhidi ya wapinzani wao, Iceland.

Baada ya bodi ya chama cha soka nchini humo kukaa na kufanya uteuzi wa nafasi hiyo, Allardyce ambaye ni maarufu kwa jina la Big Sam, alikuwa akichuana vikali na kocha wa Hull City, Steve Bruce, ambaye aliwahi kuichezea Manchester United.

Mtendaji Mkuu wa FA, Martin Glenn, alithibitisha kuwa bodi ya watu 12 ya FA itajulishwa rasmi kuhusu mchakato huo unavyoendelea baada ya kila kitu kuwa sawa.

Waliopewa mamlaka ya kupendekeza jina la nani atakuwa mrithi wa Hodgson ni Martin Glenn, Makamu Mwenyekiti wa FA, David Gill, aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Man United, na Mkurugenzi wa Ufundi, Dan Ashworth.

Aliyewahi kuwa kocha wa Man United, Sir Alex Ferguson, aliwaeleza wazi viongozi wa FA kuwa, mtu pekee anayefaa wadhifa wa kuwa kocha wa timu hiyo kwa sasa ni Sam Allardyce na si mtu mwingine.

“Wapo makocha wengi wenye uwezo mkubwa wa kufundisha timu, lakini kwa sasa England inahitaji kocha kama Big Sam, ninaamini yeye ndiye pekee ambaye anaweza kuipeleka timu hiyo sehemu sahihi.

“Kama atapata nafasi ya kuifundisha timu hiyo, basi England itakuwa na mafanikio makubwa baada ya muda mfupi ujao,” alisema Ferguson.

Big Sam ambaye aliwahi kuzifundisha klabu za Newcastle, West Ham, Bolton na Notts, mwenye umri wa miaka 61, ataachana na klabu ya Sunderland baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miezi tisa.

Wiki iliyopita kocha huyo alizungumza na mtandao wa klabu ya Sunderland na kusema kuwa atahakikisha anamalizana na klabu hiyo kwa manufaa ya sehemu zote mbili.

“Ninaamini kuna mashabiki wanahitaji niendelea kuwa hapa na wengine wanaona bora niondoke, lakini kila kitu kitakuwa sawa baada ya muda mfupi na pande zote mbili zitakuwa sawa,” alisema kocha huyo

Kocha huyo alikuwa na timu ya Sunderland juzi katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu nchini England dhidi ya Hartlepool, ambapo Sunderland ilifanikiwa kushinda mabao 3-0.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles