Na Allan Vicent, Kigoma
TAASISI ya Enabel ya nchini Ubelgiji imefadhili miradi ya maji yenye thamani ya EURO milioni 8.8 sawa na zaidi ya sh bil 23.6 katika wilaya tano za Mkoa wa Kigoma ili kupunguza tatizo la maji kwa wakazi wa wilaya hizo.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Kigoma Mhandisi Mathias Mwenda, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa Mtanzania Digital aliyetembelea miradi hiyo hivi karibuni.
Amesema miradi hiyo inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Ubelgiji na Tanzania inatarajia kunufaisha wakazi zaidi ya 200,000 katika wilaya za Kigoma Vijijini, Buhigwe, Kibondo, Kakonko na Uvinza.
Amebainisha miradi hiyo kuwa ni Mkongoro (Kigoma vijijini) unaohusisha ujenzi wa chanzo cha maji kipya (intake) katika mto Nyete na matenki ambayo yatahudumia wakazi wa vijiji 7 katika kata za Mkongoro, Bitale na Mwandiga.
Amesema kukamilika kwa chanzo hicho ambacho awali kilijengwa na serikali ya awamu ya kwanza mwaka 1979 kitanufaisha wakazi zaidi ya 40,000 wa vijiji vya Mkongoro, Bitale, Nyamhoza, Nyabigufa, Kizenga, Kiganza na Mkwanga.
Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa skimu ya Mwayaya wilayani Buhigwe ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika na kubainisha kuwa utakapokamilika utanufaisha wakazi zaidi ya 8000 wa kata hiyo ya Mwayaya.
Mwingine kuwa ni wa Kijiji cha Kazuramimba katika wilaya ya Uvinza ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 60 ambapo utakapokamilika utamaliza kero ya maji kwa kiasi kikubwa katika kata hiyo.
Amesema kuwa miradi hiyo mitatu inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu huku miradi mingine ya Kifura (wilayani Kibondo) na Kiziguzigu (wilayani Kakonko) ikitarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba.
Akifafanua kuhusu gharama za utekelezaji miradi hiyo, Mwenda amesema kuwa serikali ya Ubelgiji imechangia EURO mil 8 sawa na sh bil 21.5 na Tanzania imechangia kiasi cha EURO laki 8 sawa na sh bil 2.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Ubalozi wa Ubelgiji hapa nchini Jasmien De Winne alizitaka Kamati za Usimamizi wa miradi ya Maji (CBWSO) Mkoani humo kutunza miradi hiyo vizuri na kuhakikisha inawanufaisha wananchi wote.
Aidha ili miradi hiyo iwe endelevu amewataka kuelimisha jamii umuhimu wa kuchangia kidogo huduma hiyo pindi mradi utakapokamilika.