26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

ELIMU YA MZAZI HAIHUSIANI NA MALEZI YA WATOTO

Na CHRISTIAN BWAYA,

IMEJENGEKA dhana kwamba kiwango kikubwa cha elimu anachokuwa nacho mzazi kinamaanisha ubora na ufanisi wa malezi. Katika nchi za ki-Magharibi kwa mfano; ubora wa malezi kwa maana ya uelewa wa mahitaji ya kisaikolojia ya mtoto umekuwa ukihusishwa na elimu ya wazazi inayokwenda sambamba na uwajibikaji wa kimalezi.

Hali inaonekana kuwa tofauti katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. 

Tafiti zilizofanywa kwa nyakati tofauti katika nchi za Tanzania, Botswana, Naijeria na Lesotho zinaonesha kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya elimu, kipato, mafanikio ya kimaisha ya wazazi na ubora wa malezi ya watoto. Badala yake, katika hali ya kushangaza, wazazi wasio na elimu na wenye kazi zisizo na hadhi ndio wanaoonekana kuwajibika zaidi kuliko wenzao wenye elimu ya kuanzia Shahada na kuendelea.

Kwa upande mwingine, wazazi wasio na elimu wala kazi zenye hadhi, wameonekana kuwa na uhusiano na watoto, wakitumia muda mwingi kuwafunza watoto tabia zinazokubalika katika jamii zao.Aidha, tafiti hizo zinaonesha kuwa wakati wazazi wenye elimu kubwa hawapati/hawana muda wa kukaa na kuwasiliana na watoto wao ipasavyo, bado angalau hujitahidi kuweka mazingira ya kujifunzia nyumbani kwa maana ya vitabu, televisheni, na vifaa vingine vya michezo kwa watoto.

Hata hivyo, wazazi hawa wameonekana kushindwa kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia majumbani kwao kama wenzao wenye elimu.

Mazingira ya nyumbani

Watafiti karibu wote niliowataja mwisho wa makala haya wanakubaliana kwamba bila kuzingatia elimu wala kipato cha mzazi, mazingira ya nyumbani pamoja na mitazamo ya wazazi ndiyo hasa huathiri makuzi na malezi ya watoto. Wakati mazingira ya nyumbani yakimaanisha hali ya upendo unaooneshwa na wazazi kwa watoto, uhusiano wa wazazi wenyewe, mienendo ya wazazi, muda wanaoutumia wazazi nyumbani na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia; mitazamo ya wazazi kwa upande mwingine ni matarajio ya wazazi kwa watoto wao, jitihada za kuelewa na kujibu mahitaji ya kihisia ya mtoto, namna ya kuwapa moyo na hata kuwaadhibu. 

Hata hivyo, matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kwamba wazazi wengi wa Afrika huanza kujali, kufuatilia, kuelekeza na kuingilia shughuli za watoto wao wanapofikia kipindi cha kubalehe. Sababu kubwa inayotajwa ni kwamba katika kipindi hiki ndipo watoto huanza kuonesha tabia zisizowapendeza wazazi, ambazo kimsingi huwa ni matokeo ya kupuuzwa kwa mahitaji ya kihisia tangu awali. Kabla ya hapo, wazazi bila kujali elimu huamini hapana haja kubwa ya kuweka nguvu katika kujenga tabia ya mtoto.

Maana ya matokeo haya kwa wazazi

Barani Afrika, elimu ya darasani haimsaidii mtu kuwa mzazi bora wala kutokuwa nayo hakumfanyi mzazi kutimiza wajibu wake. Kinachoonekana ni kwamba ongozeko la elimu linaenda sambamba na ongezeko la majukumu mengine ambayo wazazi hujikuta wakiyapa uzito kuliko malezi. Kwa upande mwingine, kutokuwa na majukumu hayo huwa faida kwa mtoto ingawa changamoto inabaki kuwa uelewa sahihi wa mahitaji ya mtoto.

Inavyoonekana, mabadiliko ya kijamii na kiuchumi tunayoyashuhudia, yanaleta changamoto mpya katika malezi. Wakati mzazi msomi akiathirika kwa kutoa muda wake katika kukabiliana na changamoto hizi nje ya familia, mzazi asiye na msomi naye anapambana nazo hapo hapo nyumbani kwa namna yake.  Kwa namna moja au nyingine, aina za kazi wanazofanya wazazi, mitazamo yao na changamoto nyinginezo huathiri namna wanavyojishughulisha na makuzi ya mtoto kihisia. 

Kiungo cha tafiti na watafitiwa

Zimefanyika tafiti nyingi kuhusu mahitaji na matatizo ya watoto barani Afrika. Kwanini tafiti hizi haziwafikii walengwa? Sababu moja kubwa ni kwamba tafiti nyingi hulenga kukuza maarifa ya kitaaluma pekee. Hufanywa kwa minajili ya watafiti kuwasiliana wao kwa wao na si kutumika moja kwa moja katika kutatua matatizo halisi.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vitabu vya watafiti wafuatao: A. Blair, I. Omari, T, Mwamwenda, D. Mbilinyi, A. Mbise, A. Oyewole na C.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles