31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ELIMU YA MABADILIKO YA TABIA NCHI ITOLEWE KWA WAKATI

Na Ismail Ngayonga

RIPOTI iliyotolewa na Idara ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, inasema maeneo mengi ya Bara la Afrika kwa mwaka huu yataendelea kusumbuliwa na uhaba wa chakula na hatari ya baa la njaa na ukame.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa ifikapo mwaka 2050 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wastani wa mavuno ya mpunga, ngano na mahindi utashuka kwa asilimia 14, asilimia 22 na asilimia tano, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Katika kipindi kisichopungua miongo mitatu, dunia imekuwa ikikabiliwa na majanga mbalimbali ambayo yamesababisha hasara kubwa ya upotevu wa mali na maisha ya watu.

Kila mwaka takribani watu milioni 200 duniani wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemo, moto na majanga mengine, hivyo kuongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.

Kuwepo kwa majanga haya kunatokana na sababu mbalimbali zitokanazo na kuongezeka kwa shughuli za binadamu zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa ikiwemo ukataji wa miti, uvuvi usiozingatia utaalamu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi.

 

Tanzania pia imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji na milipuko ya mabomu ambapo majanga yote haya yalileta athari kwa wananchi na mali zao.

Katika mwaka 2013/14, ukame ulisababisha upungufu wa chakula kwa watu 828,063 katika wilaya 54 za mikoa 14 nchini na Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya Sh bilioni 2.2 kwa ajili ya kusafirisha chakula hicho kwa walengwa.

Sekta ya Kilimo ni uti wa mgongo kwa wananchi na uchumi wa Tanzania na kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kumechangia kwa kiasi kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na kutotabirika kwa mvua kumeathiri wakulima.

 

Taarifa ya hali ya chakula ya mwaka 2016/17 iliyotolewa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inaonyesha kuwa kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, mikoa 15 na halmashauri 43 zilibainika kuwa na maeneo yenye uhaba wa chakula kutokana na ukame ulioathiri mazao.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa mvua za vuli zinazochangia asilimia 17 hadi 20 ya uzalishaji wa chakula, zilichelewa kuanza na kunyesha chini ya kiwango na kwa mtawanyiko usioridhisha katika maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Hali hiyo inaelezwa kuathiri uingizaji wa mazao ya chakula kwa wingi sokoni hususani mahindi kutokana na wafanyabiashara kukodi mazao hayo wakiwa na matarajio ya kupanda kwa bei.

Mtaalamu wa mazingira katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Theresia Massoy, anasema mpango huo umekusudia kutoa kipaumbele katika  kuboresha matumizi bora ya ardhi na maji katika kilimo, ikiwa ni pamoja na kuwa mbinu mbalimbali za uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua.

Wizara imepanga kushirikiana na wataalamu wa kilimo katika halmashauri nchini kwa kutilia mkazo na kuzijengea uwezo mbinu za kienyeji za uvunaji maji ya mvua kwa kuzingatia utafiti, sera ya umwagiliaji na ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi.

Katika kuongeza kasi ya matumizi ya mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, Serikali iendelee kuzijengea uwezo halmashauri ili ziweze kuhuisha masuala ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi katika mipango, mafunzo na uhamasishaji.

Hali ya hewa duniani inabadilika, hivyo uzalishaji wa chakula na kilimo ni lazima vibadilike ili kwenda sanjari na mabadiliko hayo.

Kuwekeza kwa wakulima wadogo kutasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na umuhimu wa kundi hilo katika kilimo, ndio maana ajenda ya mwaka 2030 inatoa wito wa kutokomeza njaa pamoja na kuchangia kilimo endelevu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles