JUMA lililopita tulijadili suala la watoto na usalama wao kama lilivyojitokeza katika taarifa ya mwaka ya Haki za Binadamu inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu. Baada ya watu kusoma makala ile wapo waliohoji kazi za kituo na wakidhani kuwa kituo hakijafanya vya kutosha katika utetezi wa haki za watoto ila kimejikita katika masuala ya kisiasa zaidi.
Huu ulikuwa mrejesho mzuri kwani kazi kubwa ya Kituo cha Sheria tangu kianzishwe imekuwa ni kukuza uelewa wa haki za binadamu na sheria zinazohusu haki hizo kwa jamii ya Watanzania. Tunaposema jamii tunamaanisha raia ambao ndio wamiliki wa haki hizo pamoja na dola ambayo ndio msimamizi wa haki hizo. Kazi nyingine zilizotokana na elimu hiyo ni kazi za msaada wa sheria ili kupambanua hali halisi ya upatikanaji wa haki hapa nchini. Vile vile ipo kazi iliyoibuka kutokana na kutoa elimu ambayo ni ufuatiliaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu hapa nchini.
Katika kujaribu kutafakari mrejesho huu na mingine ambayo tumewahi kuipata inaonekana kuwa suala la uelewa wa haki za binadamu pamoja na kuwa tumejitahidi sana lakini bado ipo kazi kubwa sana mbele yetu. Hili la watoto ilikuwa ni kuhoji kazi tunazozifanya pamoja na kuwa tupo kazini kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Lakini wengine wamehoji yale tunayoyafanya kama kweli ni haki au si haki. Maswali kama hayo yamezidi kudhihirisha kuwa suala la haki za binadamu si rahisi kama ambavyo tungedhania. Tulipoanza kutoa elimu kwa jamii zinazokeketa watoto wa kike wanajamii walituambia kuwa wanafurahia sana tukitetea masuala ya ardhi lakini haya ya watoto kukeketwa tusiyaguse maana hayahusiani na haki. Haya ni mila zao waachwe wafanye watakavyo. Hata baba mmoja ambaye ilibidi afunguliwe kesi ya jinai alishangaa sana kuwa iweje watoto wake mwenyewe asiruhusiwe kufanya atakavyo?
Hili pia linaoana na lile la wazazi na walimu kuchapa watoto na kudhani kuwa mradi ni watoto wanaweza tu kuchapwa na wakati mwingine si kuchapwa bali ni kupigwa kiasi cha watoto hao kudhurika na wengine hata kufa. Hawa wengi nao wamekuwa wakihoji suala hilo linahusiana vipi na haki kama sio kuharibu watoto. Wao husema kuwa watoto wasipopigwa hawawezi kuwa watu na ndio wengi wanavyodhania. Huu bado ni mjadala mrefu na hapa elimu inahitajika sana na inahitaji kuchukuliwa taratibu na kwa mifano dhahiri kwani wengi hudhani haya ni mambo ya kigeni.
Jambo jingine ambalo baadhi ya watu bado hawajaelewa ni pale tunaposema kuwa haki ya kuishi ndio haki ya msingi kwa hiyo pasiwe na sababu yoyote ya mtu kuuawa. Hapa tumekuwa tukijaribu kuelezea adhabu ya kifo na jinsi ambavyo si sahihi kutolewa hata kwa mtu aliyeua. Hapa wengi hawaelewi kabisa kwani wanauliza, iweje mtu yeye aue tena kinyama kabisa halafu yeye asiuawe? Hamuoni mnatetea wauaji? Jibu rahisi ni kuwa mtu aliyeua amekosa kosa kubwa sana na Serikali kupitia adhabu ya kifo ikimuua mtu huyu ni kwamba inakubaliana naye kuwa uhai unaweza tu kuondolewa. Kumsaidia mtu wa aina hii ingefaa kumpa nafasi ajue kiasi gani amekosa na apewe adhabu ambayo itamsaidia kujutia kosa lake kama vile adhabu ya kufungwa maisha au miaka mingi. Hili nalo bado liko katika mijadala wapo wanaoelewa lakini wapo ambao bado wanaona ni sawa tu kulipiza kisasi na kumuua aliyeua.
Jambo jingine ambalo limewapa watu shida wakati tukilizungumzia ni pale madaktari walipogoma karibu mara mbili kwenye mwaka 2006 na 2012. Kama Kituo tuliitaka Serikali iwasikilize madaktari na kuwapa nafasi ya kuelewana ili waweze kurejea kazini, kwani wasipofanya hivyo wanaoumia ni wananchi hasa wasio na uwezo wa kwenda kwenye hospitali za kulipia.
Watu wengi hawakuelewa wakatulaumu sana kuwa tunatetea madaktari hatuna utu, watu wanakufa nakadhalika. Kikubwa tulichokuwa tunaonyesha ni kuwa haki walizonazo madaktari kama waajiriwa ni muhimu kama haki walizonazo wagonjwa.
Na ili wagonjwa waweze kutibiwa vyema ni muhimu hao wanaowahudumia wawe katika hali ya kuridhika na wawe na moyo mweupe. Hapa pia ikumbukwe kuwa madaktari waligoma baada ya mijadala na ahadi nyingi zilizokuwa hazijatekelezwa. Vinginevyo itakuwa kama walivyofanyiwa walimu kulazimishwa kurudi shuleni matokeo yake kukawa na mgomo baridi ambao ulikuja kugundulika baadaye sana tulipoanza kuona watoto wanaingia shule na kutoka bila kujua kusoma wala kuandika.
Haki za binadamu ni stahili zinazotegemeana ukijaribu kuzitenganisha lazima kutakuwa na mushkeli katika kuzifaidi. Hapa bado tunahitaji kuelimishana zaidi maana wapo ambao hawaelewi, ndio maana kuna aliyetuambia kuwa ‘mnazungumzia haki zipi wakati watu wanakufa? Ili watu wapate haki yao hii mazingira lazima yawe mazuri kwa wanaowapatia huduma na kwa huduma yenyewe.
Katika taarifa zetu za haki za binadamu tumekuwa tukizungumzia masuala ya watu kujichukulia sheria mkononi na kuua watu wanaowatuhumu na pia masuala ya ufisadi na rushwa. Wapo waliowahi kutuuliza haya nayo yanawahusu nini? Suala la ufisadi na rushwa yanagusa sana suala la watu kufaidi haki zao. Ufisadi unaofanyika huweza kufanya watu wakose haki zao za msingi.
Nchi imeingia kwenye wimbi la umasikini kutokana na wachache kuiba mali za umma na kujitajirisha wakati wengi wakiwa masikini. Elimu, afya, miundombinu vyote vinaathirika kutokana na ufisadi. Wanaochukua sheria mkononi wamewahi kuua watu ambao wala hawahusiki na kosa lolote bali kuwashuku tu.
Tumewahi kufuatilia shauri lililokuwa dhidi ya Serikali yetu wakati ilipovunja mkataba na shirika lililokuwa likisambaza maji jijini Dar es Salaam. Tuliweza kushirikiana na mashirika mengine kuomba kuwa marafiki wa Mahakama ya Kimataifa iliyokuwa inasikiliza shauri hilo dhidi ya Serikali yetu.
Kwa kufanya hivyo tulitoa hoja zetu zilizokuwa zinaiunga mkono Serikali yetu na hoja zile zilitumika na Serikali yetu ikapata ushindi vinginevyo ingepigwa faini kama ilivyokuwa katika shauri lile la DOWANS. Kwa upande wetu tuliona kiasi gani ambavyo kama raia tungeumizwa iwapo Serikali yetu ingetakiwa kulipa mabilioni kwa shauri ambalo lilitokana na huduma mbovu iliyoathiri hasa haki yetu ya kupata maji safi na salama.
Katika taarifa yetu huwa tunajiangaliza pia masuala ya utawala bora kwani utawala usipokuwa bora huweza kuminya haki za biandamu. Kwa nchi kama hii ya kwetu bado tunajibidiisha kufikia demokrasia. Msingi mmojawapo mkuu wa demokrasia ni utawala wa sheria. Hivi karibuni tumekuwa tukivutiwa sana na jinsi Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoanza kwa kasi nzuri ya kupambana na rushwa, ufisadi na kutotimiza wajibu kwa watumishi wa Serikali.
Pamoja na kuwa watu wengi wamefurahishwa sana nasi tukiwamo, kwani kilio chetu kwa miaka mingi ni hali mbovu iliyokuwapo, lakini ilibidi tutoe tahadhari ya njia ya kutekeleza kasi hiyo. Tuliona wapo ambao pia hawakutuelewa kabisa. Kwa mfano kuna waliohoji wanaotetea wanaotumbuliwa, Je, wanalitakia mema Taifa?
Pia tumeona katuni iliyochorwa ikimuonyesha kiongozi aliyeshika rungu akitaka kumkabili fisadi halafu mguuni kafungiwa kitanzi chenye jiwe kubwa lililoitwa wanaharakati. Swali kama hilo na pia katuni ile inaonyesha kutokuelewa kwa yale yaliyokuwa yanatahadharishwa. Hoja haikuwa kuwatetea wanaotumbuliwa bali ni kutahadharisha njia zinazotumika. Hata ingekuwa ni utetezi nao pia ni haki.
Watu hudhani kuwa mtu akishatuhumiwa basi hana haki ya kutetewa. Mfano mzuri wa haki hii ni pale mtu anapojaribu kuipindua Serikali iliyopo madarakani hapa huwa anashitakiwa kwa kosa la uhaini. Pia mtu aliyetuhumiwa kwa kuua kwa kukusudia hawa pamoja na kuwa wanatuhumiwa kwa makosa makubwa sana bado Serikali huwawekea mawakili wa kuwatetea kwa mujibu wa sheria ili kesi zao ziweze kufanyika kwa haki. Wasije wakatiwa hatiani kwa kuwa tu hawana utetezi wa kisheria.
Maana yake iko katika Katiba ya nchi ya mwaka 1977 ambayo katika ibara ya 13 inatoa haki ya usawa mbele ya sheria lakini pia inatoa maelekezo ya njia ya kushughulikia watu walioshtakiwa kijinai au watu wanaoshukiwa kuwa wakosaji.Kwa vile Katiba tunayo na ndio mwongozo wetu ni lazima ifuatwe.
Jambo ambalo tunaendelea kujifunza ni kuwa suala la haki za binadamu ni pana sana na linahitaji upeo kuweza kulielewa vya kutosha. Hii inatoa fursa ya kuendeleza elimu hii ili tuelewane pale haki zinapozungumziwa.