Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
“Nililazimika kuzima simu yangu kwa siku mbili baada ya kitendo kile, sababu kila mtu alikuwa akinipigia simu wengine wakinitumia meseji za kuniambia kwamba ndio ukome. Nilifikiria hata kujitoa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuona wengi wakitoa maoni hasi juu yangu, lakini nikashauriwa kuachana na mpango huo,” amesema Mtangazaji wa Clouds Media Group, Prisca Kishamba.
Prisca ametoa ushuhuda huo Agosti 10, 2021 kwenye Mjadala wa Unyanyasaji wa Kijinsia katika vyombo vya habari ulioratibiwa na Internews Tanzania kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ukihusisha Wahariri na wadau mbalimbali akiwamo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul.
Prisca ametoa ushuhuda huo kufuatia kukumbana na unyanyasaji wakati akitimiza majukumu yake, ambapo alitishiwa kudharirishwa na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, ambaye alisema kuwa: “Tena wewe nyamaza kabisa wewe, nitakudhalilisha, ninazo picha zako…” alinukuliwa Manara akimtolea maneno mwanahabari huyo baada ya kuulizwa swali kuhusu mwenendo wa timu yake hiyo.
Awali, Mjumbe wa Bodi ya Jukwaa la Wahariri (TEF), Neville Meena akiwasilisha mada kwenye mjadala huo alisema bado inahitajika elimu na mafunzo mahususi juu ya kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyumba vya habari.
“Hii ni wazi kuwa kujengewa uwezo ikiwamo elimu na mafunzi kwa wanahabari itakuwa ndiyo mwarobaini wa kukabiliana na changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye vyumba vya habari na katika utekelezaji wa majukumu kwa ujumla.
“Pamoja na hayo, kuwepo na taratibu za kiutendaji ambazo hazitoi mwanya wa unyanyasaji wa kingono ikiwamo pia mfumo wa kuripoti unyanyasaji wa aina hiyo na hatua za kuchukuliwa. Mafunzo mahsusi yanayolenga kukabili changamoto za usalama wa wanawake ndani ya vyombo vya habari.
“Kuwalinda waandishi wa habari wanawake wanapokuwa maeneo hatarishi au wanapotoka usiku kazini ikiwmo kuanzishwa madawati ya jinsia, ili kuwashirikisha wanawake katika misingi ya usawa,”amesema Meena.
Ametaja mbinu nyingine ya kukabiliana na changamoto hiyo kuwa ni kuwa na siku za hamasa kwa kundi la wanawake mfano kuwapa fursa ya kuonyesha umahiri wao kama ilivyo kwa siku ya wanawake.
“Kuandika ukweli juu ya mwanaume au mwanamke aliyefanyiwa ukatili kwa ushahidi toka vyanzo visivyo na upendeleo na vya kuaminika, kutoa haki na usawa kwa wote, kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika katika kuripoti masuala ya siasa, uongozi, uchumi au vita,” amesema Meena na kuongeza kuwa:
“Kuuhisha sera za jinsia na kutunga mpya, Serikali, MOAT, TEF, MCT na TAMWA wachukue hatua pia nafasi ya waandishi wenyewe katika kuchukua hatua za kukataa unynyasaji na katili.
“Iwapo hayo yatafanyika basi kutakuwa na faida kubwa ikiwamo kujenga amani ndani ya vyumba vya habari, waandishi wa habari kujiamini na kufanya kazi kwa ufanisi na kunufaika na maarifa na tija kutoka kwa waandishi, ikiwamo kuboresha sera kwani hizi za sasa haizitumiki ipasavyo, hivyo vyombo vya habari visiwe matanuru ya kuchomea watu,” amesema Meena..
Upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake(TAMWA), Joyce Shebe amesema kwenye vyumba vya habari bado kuna changamoto nyingi ambapo kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na taasisi ya WANIFRA AFRICA REPORT” Women in News umehusisha nchi nane ikiwamo Tanzania.
Umeonysha kuwa Tanzania ina zaidi ya asilimia 50 ya vitendo vya ukatili wa maneno huku ukatili wa vitendo ukiwa ni zaidi ya asilimia 40.
“Utafiti huo unaeleza kuwa asilimia 47 ya wanawake katika nchi hizo nane wamefanyiwa ukatili huku ukionyesha kuwa kiwango cha utakatili kwa wanawake ni mara mbili ikilinganishwa na wanaume.
“Changamoto hii inasababishwa zaidi na uelewa mdogo, kuhusu ukatili w akijinsia, ukimya, uwezo mdogo wa kunadika habari, kutokuwepo kwa mifumo ya kushughulikia ukatili, uoga, kipato kidogo, kujipeleka mwenyewe kwa mwanaume (boss) kitu unaweza kufanya lakini unajibebisha,” amesema Joyce.
Aidha, amefafanua kuwa suluhisho ni kwa waandishi kuwa na elimu ya kutosha kuhusu ukatili wa kijinsia pia kujena utamaduni wa kujiendeleza mara kwa mara, waandishi wa kike kujiamini, taasisi kuwa na mifumo ya kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, kuachana na ubaguzi kwa kuwaona wanawake ni daraja la chini kwenye kazi jambo ambalo si sahihi.
Naye, Naibu Waziri Wa Habari, Utaamduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, amesema kuwa jambo la msingi ni vijana kujengewa uwezo mzuri wa kielimu na kwamba iwapo mtu atakuwa na elimu basi hatakuwa na haja ya kufanyakazi kwa wasiswasi.
“Kama mtu atakuwa na elimu na maarifa ya kutosha yanayohitajika kwenye taaluma husika basi hakuna mtu atakayekunyanyasa, haijalishi ni mwanamke au mwanaume, hivyo jambo la msingi ni kuhimiza ujuzi kwa watu wetu ili kuwajengea uwezo.
“Lakini pia kuwepo kwa madawati ya jinsia kwenye vyumba vyetu vya habari, kwani hii itasaidia kuonda changamoto hizi za unyanyasaji wa kijinsia,” amesema Gekul.
Awali akifungua mjadala huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa ili kuwa na vyumba vya habari vilivyosalama ambavyo watu wanafanyakazi wakiwa huru basi ni wajibu wa kila mmoja kueleza changamoto zilizoko kwenye vyumba vya habari na kueleza namna bora ya kukabiliana nazo.