33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Elimu duni, umasikini vyachangia ongezeko utumikishwaji watoto

Na Allan Vicent, Tabora

Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa vitendo vya utumikishwaji watoto miongoni mwa jamii kunachangiwa na elimu duni ya kutokujua haki za watoto na umaskini uliokithiri kwa wakazi wa vijijini na mjini.

Hayo yamebainishwa leo Juni 14, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Abel Busalama alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa kijiji cha Igagala no.5 katika kata ya Igagala kwenye maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji watoto.

Amesema tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa vyanzo vikubwa vya vitendo vya utumikishwaji watoto katika shughuli za kijamii na kiuchumi ni ukosefu wa elimu ya kujua haki za watoto na umaskini uliokithiri.

Amesema watoto wengi wanatumikishwa katika shughuli za kilimo cha tumbaku, migodi, ufugaji, uvuvi, kazi za nyumbani na shughuli nyinginezo ambazo hupelekea kuwakosesha elimu, kupata mimba katika umri mdogo au kupata madhara ya kiafya, kisaikolojia na kimakuzi.   

DC Busalama amebainisha kuwa licha ya kutumikishwa kwenye kazi hizo kwa ujira mdogo bado ujira wenyewe hupokelewa na wazazi au walezi huku mtoto akiambulia chakula na nguo zilizochakaa kutoka katika familia au kampuni husika.

Amesisitiza kuwa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali, mashirika, makampuni na asasi zisizo za kiserikali katika kukabiliana na vitendo hivyo tatizo hilo bado ni kubwa hapa nchini hasa katika mkoa wa Tabora.

Alifafanua kuwa takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa kati ya watoto 3 wenye umri wa miaka 5-17 mtoto 1 anafanya kazi zilizo hatarishi kwa maisha yake kiafya, jambo ambalo lingeweza kuepukika kama jamii ingekuwa na elimu ya kutosha.

“Matokeo yanaonesha kuwa watoto wasiosoma shule wanatumikishwa zaidi kuliko  wanaosoma na maeneo ya vijijini watoto hutumikishwa zaidi kuliko maeneo ya mjini, elimu ya haki ya mtoto na uwezeshaji jamii kiuchumi ni muhimu,” amesema amesema.

Ameponeza juhudi zinazofanywa na Mradi wa Msaada wa Biashara Vijijini  (PROSPER RESET) katika kupambana na vitendo vya utumikishwaji watoto nchini na kuwataka kutumia mfumo wa serikali wa MTAKUWWA kukomesha vitendo hivyo.

Naye Meneja wa Mradi wa PROSPER RESET, Fredrick Malaso alisema mradi huo unaotekelezwa na asasi ya TDFT unafadhiliwa na Shirika la Eliminating Child Labor in Tobacco growing Area (ECLT) la nchini Marekani.

Aliongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miaka 3 katika wilaya 3 za Mkoa wa Tabora (Kaliua, Urambo na Sikonge), wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na wilaya ya Songwe Mkoani Songwe kwa lengo la kutokomeza utumikishwaji watoto na kuinua jamii kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles