29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

ELIMU BURE ILIVYOSABABISHA WALIMU KUELEMEWA NA WANAFUNZI

*Zamani, mwalimu mmoja wanafunzi 45,

*Sasa hivi, mwalimu mmoja wanafunzi 164


Na ASHA BANI

MWAKA jana Serikali ilitangaza kuanza kutoa elimu ya msingi bila bure. Yaani mwanafunzi anatakiwa kusoma tu bila kulipa ada kama ulivyoainishwa katika waraka wa Elimu namba tano wa mwaka 2015.

Serikali iliahidi kwamba itagharamia utoaji wa elimu ya msingi na wazazi watagharamia nauli, vifaa na sare za shule pamoja na matibabu ya watoto wao.

Mpango huo ni matokeo ya utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambamo suala la utoaji wa elimu bila malipo ni mojawapo ya mambo yaliyoainishwa.

Na kabla ya utekelezaji wa sera hiyo elimu bila malipo wazazi walikuwa wanabeba mzigo mkubwa wa kuchangia elimu na ilisababisha  baadhi yao kushindwa kupata elimu kutokana na gharama mbalimbali.

 Aidha ripoti zilizoonesha kwamba kiwango cha ruzuku  kilichokuwa kinafika  shuleni kilikuwa ni kidogo na hakikuwa kinakidhi mahitaji ya kuendesha shule.

Hata hivyo, mpango huo umeshindwa kufanikiwa kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.

Taasisi ya HakiElimu ilifanya utafiti katika mpango huo na kuonesha mapungufu yake ambapo serikali inatakiwa kuchukua hatua ili kuboresha zaidi na kuleta mafanikio.

Utafiti wa HakiElimu ulielekezwa katika wilaya za Njombe, Mpwapwa, Sumbawanga, Kilosa, Korogwe, Tabora Mjini na Muleba na ilihusisha shule za msingi 28 na sekondari, walihojiwa walimu wakuu, walimu wa kawaida na wazazi.

Katika utafiti huo yalibainika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na changamoto ya fedha za ruzuku ambazo zinapelekwa shuleni bila kuzingatia idadi ya shule ,wanafunzi kama ambavyo inapaswa kuwa.

Kimsingi jumla ya fedha za ruzuku zinazopelekwa shuleni inapaswa kulingana na idadi ya wanafunzi ambapo shule zenye idadi kubwa zinapaswa kupata fedha nyingi zaidi ya shule zenye idadi ndogo.

Akitolea mfano alisema Shule ya Msingi ya Muleba wilayani Muleba yenye wanafunzi 828 ilipokea kiasi cha fedha Sh 3,918,000 ilihali ya Ilolo iliyopo Mpwapwa yenye wanafunzi 874 ilipokea Sh 3,400,000.

Akizindua utafiti huo Mkurugenzi wa taasisi ya HakiElimu John Kalaghe anasema uchambuzi wa matokeo unaonyesha kuwa baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache zinapata fedha zaidi kuliko shule zenye wanafunzi wengi.

Alifafanua kuwa kabla ya utekelezaji wa sera elimu bila malipo shule za msingi zilipaswa kupata kiasi cha Sh 10,000 na sekondari 25,000 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kwa ajili ya uendeshaji wa shule, ununuzi wa vitabu, ununuzi wa vifaa vya mitihani na ukarabati. 

“Asilimia 40  ya ruzuku kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari inapaswa kubaki tawala za mikoa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu, asilimia 60 kwa shule za msingi na asilimia 50 kwa shule za sekondari inayobaki kupelekwa moja kwa moja shuleni kwa jaili ya kugharamia ukarabati, vifaa, mitihani, utawala na michezo.

“Utafiti unaonesha kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Juni mwaka jana ambapo serikali ilipaswa kupeleka kiasi cha shilingi 3,000 kwa shule za msingi iliweza kupeleka wastani wa 2,700 kwa shule za msingi ambayo sawa na asilimia 93 na kupeleka ruzuku kwa sekondari kwa wastani wa asilimia 100,’’ anasema Kalaghe. 

Changamoto nyingine alisema shule zenye wanafunzi wachache kati ya 200-300 zinapata wastani wa shilingi 100,000-150,000 kwa mwezi ambayo haiwezi kutatua matatizo ya msingi kama vile ukarabati ikizingatiwa fedha za ruzuku zinatumwa shuleni kila mwezi huku walimu wakishindwa kutatua changamoto hiyo. 

Anasema ruzuku inayopelekwa shuleni hazikidhi mahitaji ya shule, hii imedhihirika kutoka kwa walimu 95 wakuu wa shule kwamba fedha wanazozipata hazitoshi kukidhi mahitaji mbalimbali. 

Kalaghe anasema hata baada ya kuanza kutekelezwa kwa sera ya elimu bila malipo, wazazi bado waliendelea kubanwa kwa kuchangishwa gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule kwa ajili ya watoto. 

Anasema gharama hizo ni pamoja na zile za kulipa walinzi, kujenga madarasa na kulipa wapishi na hili inategemea na wazazi wenyewe kwani wengine wanachanga na wengine hawachangi.

 

 Anasema hiyo inahusishwa moja kwa moja na matokeo ya utafiti kuhusu uelewa wazazi kwenye namna ya elimu  bila malipo, kwani asilimia 51.3 ya wazazi wanaelewa kuwa elimu bila malipo maana yake wazazi kutochangia gharama  zozote za elimu ya watoto wao katika shule za umma. 

Hata hivyo sera ya elimu bure imesababisha ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza hasa kwa shule za msingi ambapo kulikuwa na ongezeko asilimia 43 na asilimia 10 kwa shule za sekondari.

“Hali ya elimu bure imesababisha pia walimu kuelemewa kwa kuwa awali ilikuwa mwalimu mmoja wanafunzi 45 kwa sasa mwalimu mmoja wanafunzi 164 kwa wastani badala ya 45.

Maoni ya wadau wa elimu 

Mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kijamii, Jenerali Ulimwengu alichangia kwa kusema kutokana na hatua hiyo ndiyo maana huwezi kutenganisha suala la elimu na siasa kwa kuwa chimbuko la elimu bure lilianzia kwenye kampeni za siasa. 

Anasema anashangaa kwa Rais John Magufuli kukataza kuendelea na mikutano ya siasa hadi hapo 2020 wakati ingekuwa muda muafaka kuweza kuendelea kukosoa kutoa mawazo  na kuchangia hilo.0 

Mapendekezo

Utafiti huo ulipendekeza kuwa Serikali inatakiwa kufanya juhudi za makusudi ili kuhakikisha kwamba wadau wanailewa vizuri sera ya elimu bila malipo ili kurahisisha utekelezaji wake.

Anasema wadau wote wanapaswa kuzielewa nyaraka zote na miongozo kuhusiana na sera hiyo ili kila mdau atambue wajibu wake na jinsi anavyopaswa kushiriki katika utekelezaji wa elimu bure.

Anasema Fedha ya ruzuku inayotolewa haikidhi mahitaji ya shule kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Anasema japo sera ya elimu bila malipo imesaidia kuongeka kwa uandikishaji hasa darasa la kwanza, serikali ichukue hatua za makusudi kushughulikia changamoto zinazotokana na elimu bila malipo kama ongezeko la wanafunzi, uhaba wa madarasa, walimu, vitabu na kadhalika.

Pia zoezi la Serikali kupeleka fedha za ruzuku liende sambamba na za serikali kutoa fedha za maendeleo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.

Shule zina changamoto ya miundombinu na hivyo ni muda muafaka kwa serikali kuanza sasa kuzisaidia shule kwa kuzipa fedha za maendeleo kama ambavyo ilifanya wakati wa utekelezaji wa mipango ya MMEM na MMES miaka ya nyuma.

Hivyo basi, kila mdau anatakiwa kuhakikisha anaipigania elimu ya Tanzania kuwa katika kiwango kinachostahili kuwa.

Ripoti ya CAG

Aidha, katika ripoti yake ya mwaka 2015/2016 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, iliyotolewa wiki iliyopita ilibaini uhaba mkubwa wa miundombinu na samani katika shule za msingi na sekondari nchini.

Pamoja na mambo mengine, Profesa Assad ameonya  lengo la kuondoa kiwango cha ujinga katika jamii linaweza lisifikiwe endapo hatua za uboreshaji hazitachukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine.

Anasema uhaba wa miundombinu ya shule na samani, unasababisha kuwapo kwa matokeo mabaya ya wanafunzi katika shule hizo.

CAG anabainisha mahitaji ya madawati katika shule za sekondari ni 64,675, yaliyopo ni 36,043 na upungufu 28,632 sawa na asilimia 44.

Anasema kwa upande wa maabara, mahitaji ni 5,896, zilizopo ni 2,432 upungufu 3,495 sawa na asilimia 59, huku vyoo mahitaji ni 81,173 vilivyopo 20,510, upungufu 60,663 sawa na asilimia 75.

“Nyumba za walimu mahitaji ni 56,000, zilizopo 11,017, upungufu 44,983 sawa na asilimia 80, mabweni mahitaji ni 876, yaliyopo 347, upungufu 529 sawa na asilimia 60, mahitaji ya madarasa ni 209,773, yaliyopo 109,767, upungufu 100,006 sawa na asilimia 48.

“Mahitaji ya madarasa katika shule za msingi ni 44,000 yaliyopo 23,630 upungufu 20,370 asilimia 46, vyoo 90,988 vilivyopo 57,017 upungufu 33,971 asilimia 37.

“Kwa upande wa nyumba za walimu, mahitaji 69,047 zilizopo 19,500 upungufu 49,547 asilimia 72, madawati 397,652 yaliyopo 278,443 upungufu 119,209 sawa na asilimia 30,”anasema Profesa Assad.

Profesa Assad anasema ukaguzi wake, ulibaini uwezo wa wanafunzi wa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kawaida na ile ya ngazi ya juu unapungua kila mwaka.

“Hii inaashiria uhaba wa miundombinu na samani katika shule ni changamoto kubwa inayoikabili sekta ya elimu katika mamlaka za Serikali za mitaa na nchi kwa ujumla,” alisema Profesa Assad.

Anasema kukosekana kwa miundombinu muhimu ya shule kunaweza kuendelea kuathiri ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari. 

Profesa Assad anasema kuna uhaba wa walimu wa sayansi katika shule za sekondari na waliopo wachache kutopangiwa shule kwa uwiano sawa.

“Ukaguzi niliofanya katika Idara ya Elimu ya Sekondari kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa katika mwaka wa fedha 2015/16, umebaini uhaba mkubwa wa walimu wa sayansi 3,438 na wataalamu wa maabara 1,087 kwa ajili ya kufundisha masomo ya sayansi katika shule za sekondari.

“Ukaguzi wangu uligundua zaidi walimu wa sayansi wachache waliopo walisambazwa bila kuwa na uwiano mzuri kwenye shule za sekondari ndani ya halmashauri, hali iliyofanya baadhi ya shule kuwa na idadi kubwa ya walimu wa sayansi na kuacha shule nyingine bila hata kuwa na mwalimu mmoja wa sayansi.

“Katika baadhi ya halmashauri, walimu wa sayansi walipelekwa makao makuu ya halmashauri na kupangiwa majukumu ambayo hayahusiani na ufundishaji. Kwa mfano, walimu wa hisabati na teknolojia ya habari na mawasiliano katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.

“Baadhi ya halmashauri walimu walikuwa hawatumiki kikamilifu mfano mzuri ni Manispaa ya Morogoro ambapo walimu wa sayansi wenye sifa za shahada ya uzamili katika masomo ya sayansi na hisabati, walipelekwa kufundisha katika shule za sekondari za elimu ya kawaida badala ya kuwapanga kufundisha elimu ya juu ya sekondari,” alisema.

Anasema hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa rasilimali watu haitumiki ipasavyo ambapo anazishauri menejimenti za halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuja na mikakati inayotekelezeka ili kumaliza tatizo la walimu wa sayansi kwa kuhamisha walimu wa sayansi ambao ni wahitimu wa shahada.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles