26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 2, 2023

Contact us: [email protected]

Elimu afya na barabara kipaumbele bajeti Jiji la Mwanza

Na Clara Matimo, Mwanza

Baraza la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Mwanza limepitisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 142 huku vipaumbele vikiwa ni afya, elimu na barabara ili kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta hizo.

Kwa mujibu wa Naibu Meya wa Jiji hilo, Bhiku Kotecha, katika bajeti hiyo zaidi ya Sh bilioni 114 kutoka Serikali Kuu na Sh bilioni 28.13 mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Mapendekezo hayo yamepitishwa Machi 10, 2023 kwenye kikao maalum cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili na kuidhinisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024. 

Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la mwanza Bhiku Kotecha(kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji hilo, Erick Mvati wakiwa kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilicholenga kujadili na kuidhinisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Bajeti hii imegusa kila eneo lenye changamoto kwa wananchi wa wilaya ya Nyamagana hivyo ni matumaini yetu sisi madiwani wote wa halmashauri ya jiji la Mwanza kwamba mapendekezo ya bajeti tuliyoipitisha ikirudi vizuri tutaenda kutekeleza miradi yote tuliyoianisha ikiwemo ya maendeleo ya jamii.

“Lakini ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi sisi madiwani tunawategemea sana wataalamu wa halmashauri ya jiji letu la Mwanza hivyo nawasihi sana endeleeni kutushauri vizuri ili kwa pamoja tuwaletea wananchi maendeleo tunahitaji ushirikiano na katika kila jambo tunalolifanya tumtangulize Mungu mbele tukifanya hivyo tutaweza kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan mwenye nia ya dhati ya kuwaondolea wananchi changamoto zinazowakabili,”amesema Kotecha.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Erick Mvati alisema  wametenga Sh bilioni moja kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya maabara lengo likiwa ni kuhakikisha shule za sekondari ambazo hazina maabara zinatatuliwa changamoto hiyo.

Diwani wa Kata ya Mkolani Viti Maalum(CCM),Mariam Maftah alisema amefurahishwa na mapendekezo ya bajeti hiyo maana  anaamini endapo itarudi kama walivyoipitisha itasaidia kutatua changamoto za uhaba wa vyumba na vifaa vya maabara katika shule za sekondari kwenye jiji la Mwanza hali itakayowawezesha wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kujifunza kwa vitendo hivyo kuwa na ufaulu mzuri watakapohitimu elimu ya sekondari.

Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakiwa kwenye kikao maalum  kilicholenga kujadili na kuidhinisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kilichofanyika Machi 10,2023.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga aliyehudhuria kikao hicho aliwataka wataalamu na watumishi wa umma ndani ya halmashuri ya jiji la Mwanza kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwatatulia changamoto walizonazo.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka kesho 2024, CCM  inaimani kubwa sana na nyie kwamba mtaendelea kuwahudumia wananchi na kuwatatulia changamoto walizonazo kwa wakati ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kutuamini.

“Hatutaelewani endapo wananchi wakiwa na changamoto ambayo haina majibu lengo na nia ya CCM  ni kutafuta suluhu kwa kila changamoto walizonazo wananchi, ikiwezekana wapate majibu ya kina ili waelewe mipango ya chama tawala yenye dhamira ya kuwanufaisha kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo,”alisema Kavenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,405FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles