Na Mohammed Hamad, Kiteto
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara imerejesha eneo la ekari 27 lililoporwa kwa miaka 10 Mali ya, Imbori Hando (72) mkazi wa Kibaya wilayani humo.
Makabidhiano ya eneo hilo yalifanyika Kijiji cha Ndaleta, chini ya Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Kiteto, Venance Sangawe aliyesimamia kupatikana haki hiyo.
Sangawe amesema walipokea lalamiko hilo na kulifanyia kazi na kubaini kuwa baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali walipotosha ukweli wa suala hilo kwa muda mrefu.
“Haikuwa rahisi Kikongwe huyu kupata haki yake…hata baadhi ya viongozi wa serikali walichangia kuchelewesha haki ya mama huyu, kila tulipotaka kujua ukweli ulipindishwa,” amesema Sangawe.
Leo tumemkabidhi shamba lake ekari 27 mbele ya viongozi wa Kijiji Kata na Tarafa, baada ya kubaini ukweli wa jambo hili ambapo viongozi wengi Kiteto waliamua kuachana nalo.
Mama Imbori amesema: “Nilipuuzwa kila kona, pamoja na kushinda kesi baraza la ardhi la kata na kukaza hukumu baadhi ya watumishi wa serikali walishindwa kunisaidia huku nikidaiwa kuwa mimi nimechanganyikiwa kutaka kupotosha ukweli,” amesema Imbori.