Na Ramadhan Hassan, Dodoma
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeteja mipango ya muda mfupi wa kati na mrefu kuhakikisha Mkoa wa Dodoma unakuwa na maji ya kutosha.
Mipango hiyo imetajwa leo Julai 28,2023 na Mkurugenzi Duwasa, Aron Joseph wakati akiwasilisha taarifa ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2023-2024 kwa Waandishi wa Habari.
Amesema Mpango wa muda mfupi ni kufanya utafiti, kuchimba na kuendeleza visima maeneo ya pembezoni mwa mji.
Aidha, amesema lengo la mpango huo ni kupunguza adha kwa wakazi katika maeneo hayo, na kupunguza utegemezi wa chanzo kikubwa cha Mzakwe.
“Hii ni wakati tunasubiri uwekezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati jijini Dodoma,”amesema Joseph.
Aidha, amesema katika mpango wa muda wa kati, DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji inaendelea kufuatilia hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa bwawa la Farkwa lililopo wilaya ya Chemba – Dodoma.
Amesema katika mpango wa muda mrefu, DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji inaendelea kufuatilia hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji ziwa Victoria kuja Dodoma.