DAVAO, PHILIPPINES
KATIKA mlolongo wa kauli zake tata kuhusu mashambulizi ya kingono, Rais Rodrigo Duterte ameripotiwa akisema atawapongeza wabakaji wakitenda jinai itakayowahukumu kifo.
Akizungumza na wanadiplomasia wa Ufilipino Ijumaa iliyopita katika mji wa nyumbani wa Davao, ambako alihudumu kama meya kwa zaidi ya miongo miwili, Duterte alizungumzia masuala ya uhalifu unaotokana na mihadarati, ikiwamo ubakaji.
“Kile nisichopenda ni watoto kubakwa. Mnaweza kubaka pengine mrembo wa Miss Universe. Hapo naweza kukupongeza kwa ujasiri wa kumbaka mtu ukifahamu kuwa utaishia kunyongwa,” Duterte anadaiwa kusema.
Duterte (72), aliukwaa urais mwishoni mwa Juni 2016, na kipindi kisichozidi mwaka mmoja baadaye, alilaaniwa duniani kwa vita dhidi ya unga, ambayo imesababisha maelfu ya mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu.
Wakati akiendesha kampeni za urais Aprili 2016, Duterte alitoa kauli za kutisha kuhusu mmisionari wa Australia, ambaye alibakwa na kundi la watu na kuuawa wakati wa uasi gerezani mwaka 1989 mjini Davao, wakati akiwa meya.
“Niliona uso wake na kujiwa na wazo: Wapumbavu, wamembaka kwa zamu, walipanga foleni. Nilikasirika kuwa alibakwa, lakini alikuwa mrembo. Nilidhani kama meya nilipaswa kuwa wa kwanza,” alisema.
Baadaye aliwaambia wakosoaji wake maneno hayo hayakuwa utani na aligoma kuomba radhi.
Mei mwaka huu, Rais Duterte aliwaambia askari wake angewaruhusu kubaka wanawake watatu kila mmoja.
“Fanyeni kazi yenu. Mengine niachieni. Nitaenda jela kwa ajili yenu. Iwapo mtabaka watatu, nitaikubali,” alisema.
Na wakati binti yake mwenyewe alipotangaza kuwa mwathirika wa ubakaji, Rais Duterte anaripotiwa kupuuza madai yake akimwita ‘malkia wa maigizo.’
Tangu aukwae urais, ametoa kila aina ya kauli tata kuanzia kumtusi Rais Barack Obama hadi kudai ameua wahalifu kwa mkono wake na kuwala nyama.