31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Dunia kushuhudia ‘Iron Ladies’ wakishika dola?

Margaret Thatcher
Margaret Thatcher

NA LEAH MWAINYEKULE,

JANUARI 19, 1976, Mwanamama Margaret Thatcher ambaye alikuwa ametoka kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Conservative nchini Uingereza, alitoa hotuba iliyoitwa “British Awake” akiwa jijini London.  Katika hotuba hiyo, Thatcher aliwashutumu Warusi kwamba wanataka kuitawala dunia na wanafanya kila wawezalo ili kuwa taifa kubwa zaidi lililowahi kutokea duniani.

Januari 24 ya mwaka uliofuata, gazeti la kijeshi la Kisovieti, Red Star, lilichapisha majibu kwa hotua ya Bi. Thatcher, kupitia Mwandishi wake Kapteni Yuri Gavrilov.  Katika makala yake, Kapteni Gavrilov aliandika kichwa cha habari “The ‘Iron Lady’ Sounds the Alarm” akimtaja Bi. Thatcher kama mwanamke wa chuma.  Makala ile ilichapishwa tena kwenye gazeti la Sunday Times la Uingereza wiki iliyofuata.

Tangu wakati huo, jina la ‘Iron Lady’ lilimkaa Bi. Thatcher, hasa kutokana na misimamo yake isiyoyumba.  Lilimjengea jina kubwa na hata akawa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke wa Uingereza na pia Waziri Mkuu wa Uingereza aliyeongoza kwa muda mrefu, kuanzia mwaka 1979 hadi 1990.  Uongozi wake na uimara wake ulimfanikisha kushinda chaguzi tatu mfululizo.

Margret Thatcher alikuwa ni mfano mmoja wa wanawake wa chuma ambao wanaweza kukumbukwa duniani kwa kuongoza mataifa makubwa na kufanya maamuzi makubwa yaliyowekwa katika vitabu vya historia.

Ukiachilia mbali maamuzi aliyokuwa akiyafanya ambayo yaliathiri moja kwa moja raia wenzake, Bi. Thatcher anakumbukwa kwa kuongoza vita ya Visiwa vya Falkland ambavyo vilivamiwa na Argentina mwaka 1982.  Hakusita kupeleka vikosi vya kijeshi kupambana na vikosi vya Argentina, na aliishinda vita hiyo ambayo ilisababisha pia vifo vya askari 655 wa Argentina, 255 wa Uingereza na raia watatu wa Falkland.

Kwa sasa, inadhaniwa kwamba huenda nchi mbili zenye nguvu duniani,  Uingereza na Marekani – zikaongozwa na wanawake wengine wa chuma.  Kwa Uingereza, uhakika uliopo ni kwamba Waziri Mkuu atakayefuata atakuwa mwanamke.  Leo hii, Jumatano, David Cameron anatarajiwa kuachia nafasi yake ya uwaziri Mkuu, na uongozi utachukuliwa na Theresa May.  May anachukua nafasi hiyo baada ya kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Conservative ambacho ndicho kinachoshika dola ya Uingereza kwa sasa.  Ushindi wa mwanamama huyu uliwezekana baada ya mgombea mwenzake, Andrea Leadsom, kujitoa katika kinyang’anyiro cha kuwania kuwa kiongozi wa chama chao.

Kwa upande mwingine, Uchaguzi Mkuu nchini Marekani unatarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu na Rais mteule kuapishwa ifikapo Januari mwakani.  Mfanyabiashara Donald Trump ndiye atakayekuwa akigombea kiti cha Urais kwa tiketi ya chama cha Republican, huku Mwanamama Hilary Clinton akitarajiwa kugombea kupitia chama cha Democrat.

Endapo Hilary atashinda katika uchaguzi huo, basi ataungana na Theresa May katika orodha ya wanawake waliofanikiwa kushika dola.

Swali ambalo wengi huenda wakawa nalo kwa sasa, ni kwamba endapo wanawake hawa watapewa uongozi katika nchi zao, wataweza kuweka historia na kuwa na nguvu ile ile kama ilivyo kwa wanawake wengine kama vile Margaret Thatcher?  Watakuwa wanawake wa chuma?

Dunia imekwishashuhudia wanawake wengine wenye nguvu katika uongozi.  Yupo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Ellen Johnson Sirleaf ambaye ni Rais wa 24 wa Liberia, aliyeingia madarakani miaka kumi iliyopita na kupewa uongozi wa nchi iliyokuwa na majeraha na changamoto kubwa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Wengine ni Cory Aquino aliyekuwa Rais wa Ufilipino kwenye miaka ya 1980 na Golda Meir aliyekuwa Waziri Mkuu wa nne wa Israeli na kuiongoza nchi yake katika vita na amani kutoka mwaka 1966 hadi 1974.

Alikuwapo pia Benazir Bhutto wa Pakistan ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo mwaka 1988, nchi ambayo inashutumiwa kwa kutojali haki za wanawake na huenda angekuwa Waziri Mkuu kwa mara nyingine endapo asingeuawa mwaka 2007 na mtu aliyejilipua kwa bomu.

Alikuwapo pia Indira Gandhi ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa tatu wa India kutoka mwaka 1966 hadi 1984.  Yeye pia aliuawa.  Hata Iceland, nchi yenye watu 330,000 tu na ambayo baadhi ya watu wameisikia kwa mara ya kwanza wakati wa michuano ya Euro iliyomalizika Jumapili iliyopita, nayo ina Waziri Mkuu mwanamke, Jóhanna Sigurðardóttir.

Ukweli ni kwamba kinachoonekana hivi sasa ni imani ya wapiga kura katika kuwapa uongozi wanawake, licha ya kwamba katika miaka ya nyuma, uongozi ulikuwa ukidhaniwa kuwa kwa ajili ya wanaume tu.

Na wakati nchi zingine duniani zimedhihirisha kuamini kuwapa wanawake kuongoza nchi, Marekani, nchi ambayo inapenda sana kuwanyooshea wengine kidole kwa “kukiuka haki za binadamu” haijawahi kuwa na Rais mwanamke.  Endapo Hilary Clinton atashinda, basi ataingia katika vitabu vya kumbukumbu vya Guinness.

Tukumbuke kuwa licha ya kwamba Hilary aliwahi kuwa ‘First lady’ wa Marekani kutokana na kuwa Mke wa Rais wa 42 wa Marekani, William Jefferson (Bill) Clinton, si mara yake ya kwanza kugombea uongozi na kufikia hatua ya juu.

Hilary Clinton
Hilary Clinton

Mwaka 2008 Hilary alikuwa mmoja wa wanachama wa Democrat waliokuwa wakiomba ridhaa ya chama chao kuwa wagombea wa kiti cha Urais wa Marekani.  Alifika hatua za mwisho kwa kubaki yeye na Barack Obama, lakini mwisho wa siku Obama alimshinda na kuwa chaguo la chama.  Safari hii Hilary ameshampita kwa mbali mwanachama mwenzake Bernie Sanders na kuwa na uhakika wa kupambana na Donald Trump katika kuusaka Urais wa Marekani.

Hilary pia alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati wa kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Obama, kazi ambayo ni ngumu na inamhitaji mtu makini sana katika kuifanya kutokana na kuwa na changamoto nyingi za kidunia, kama vile kukabiliana na uhasama uliopo kati ya Israel na Palestina.

Hilary pia anakumbukwa kwa ujasiri aliouonyesha wakati wa sakata la mumewe, wakati huo akiwa Rais wa Marekani, kuwa na uhusiano wa kingono na mwanadada Monica Lewinsky.  Alisimama kwa ujasiri na kuamua kuwa upande wa mume wake, licha ya kuwapo kwa harakati zilizokuwa zikifanywa za kutaka kumuondoa madarakani.  Alidhihirisha kuwa ‘Iron Lady.’

Kwa upande wa Uingereza, Waziri Mkuu aliyekuwa anatakiwa ni yule ambaye jukumu lake kubwa litakuwa ni kuhakikisha kwamba Uingereza inatoka kabisa katika Jumuiya ya Ulaya.  David Cameron alishaeleza kwamba yeye hataweza kulifanya hilo na ndiyo maana alijiuzulu ili nchi ipate nahodha mwingine atakayeweza kuivusha na kuendana na mabadiliko ambayo Waingereza wengi waliyapigia kura.

Wachambuzi wa siasa nchini Uingereza walishampa nafasi kubwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Theresa May, aliyeungwa mkono na watu wanaotaka Uingereza ijitoe kwenye Jumuiya ya Ulaya.  Yeye mwenyewe amekuwa akisisitiza kwamba Uingereza inahitaji mtu shupavu wa kuivusha katika hatua hiyo na kwamba yupo tayari kabisa kuitekeleza.  Waingereza walio wengi wanaamini kwamba anaiweza hiyo kazi vilivyo na wanaamini pia kwamba katika yeye, huenda wakawa wamepata ‘Iron Lady’ mwingine.

Ni mwaka ambao tunasubiri kwa hamu kuona mwisho wake.  Ni mwaka ambao dunia inataka idhihirishe kwamba zama za wanawake kuambiwa hawawezi kutawala, zinafutika.  Ni mwaka ambao hata Kansela Angela Merkel atapata faraja ya kinamama wawili kuungana naye katika lile kundi zito la G7 na kuondoa miaka mingi ya yeye kuwa mwanamke pekee kwenye kundi hilo.

Ni mwaka ambao dunia inatarajia kupata ‘Iron Ladies’ wengine.

                                                                                                 [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles