NA RATIFA BARANYIKWA,
DALILI zinaonyesha kuwa, wanasiasa wameanza kuchokwa na jamii katika mataifa mbalimbali duniani.
Ushindi wa hivi karibuni kabisa wa Adama Barrow, huko Gambia uliotanguliwa na ule wa Donald Trump kule Marekani, ni uthibitisho tosha kwamba uvumilivu na imani ya jamii kwa wanasiasa inaelekea ukingoni.
Wakati Wamarekani wengi wakiwa bado hawaamini kile kilichotokea, baada ya mfanyabiashara Trump asiye na rekodi yoyote katika historia ya siasa za nchi hiyo kushinda kiti cha urais, ushindi wa Barrow wa Gambia nao umetoa taswira inayolandana na hiyo.
Ushindi wa Barrow umeleta mshtuko katika Bara la Afrika na pengine kuandika historia mpya ya siasa katika bara hilo.
Barrow hajawahi kuwa mwanasiasa, zaidi ya kuwa meneja mauzo katika Taasisi ya Alhagie Musa & Sons, kabla hajaelekea nchini Uingereza miaka ya 2000 kwenda kuchukua shahada ya majengo, akijilipia ada kwa kazi ya ulinzi.
Siasa haijawahi kuwa sehemu ya maisha yake, kwani hata aliporejea Gambia baada ya kumaliza masomo yake mwaka 2006 alianzisha kampuni yake ya Majum Real Estate, yeye mwenyewe akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO).
Mwaka huu alipochaguliwa na umoja wa vyama saba vya upinzani kuwa mgombea wao wa urais, siasa zake zilijikita zaidi kwenye mitandao kama facebook, Instagram nk.
Afrika na pengine dunia nzima hakuna aliyeamini kwamba Barrow, asiye na mbinu wala asiyejua fitna za siasa anaweza kuhitimisha utawala wa miaka 22 wa Yahya Jammeh.
Si hivyo tu, wengi pia walidhani ni vigumu kwake kuleta mabadiliko kupitia uchaguzi dhidi ya mbabe wa kijeshi, Jammeh na hivyo kuandika historia mpya ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru wake kutoka kwa Waingereza mwaka 1965.
Watu wanaofahamu vimbwanga vya Jammeh, wakati mwingine akijifanya ni mganga wa kienyeji ambaye mwaka 1994 akiwa kijana mdogo tena Ofisa wa Jeshi mwenye cheo cha Luteni akiingia madarakani kwa mapinduzi na mwaka 1996 akichaguliwa kuwa rais, akichaguliwa tena 2001, 2006 na 2011, hawaamini kilichotokea kwa Barrow, ambaye si mbabe wa kijeshi wala hana uzoefu katika siasa za nchi hiyo.
Wafuatiliaji wa siasa si tu za Gambia bali za dunia nzima wanasema, kilichomfika Jammeh ni matokeo ya kuacha sera na kuanza kutumia silaha za ubabe na uongo na kucheza na hisia za wananchi.
Wanasema akina Jammeh wapo wengi Afrika na habari mbaya kwao ni kwamba, wananchi wameanza kuwatambua, wametia doa siasa, wamewafanya wanasiasa wasiaminike tena.
Kwa sababu ya matendo ya wanasiasa waliowaamini kuwaangusha kwenye serikali na Bunge, wanasema wameona dalili ya wananchi kupoteza imani nao.
Wanasema ishara ya wananchi kuwa wapo tayari kumuamini mtu mwingine yeyote isipokuwa ‘mwanasiasa’ imeanza kuonekana.
Jammeh, licha ya kuuaminisha umma kwamba anaipeleka nchi katika siasa za kidemokrasia na hata kuunda chama chake cha siasa ulipofanyika uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1996, kwa sababu ya ubabe wake wananchi walionekana kukubali yaishe. Waangalizi wa kimataifa hawakuwa na imani kama uchaguzi huo ulikuwa huru na haki.
Hata katika uchaguzi wa Oktoba 18, 2001 aliposhinda kwa asilimia 53 ya kura; bado waangalizi walionya juu ya kuwapo kwa vitisho vya serikali dhidi ya wapigakura, lakini pia kuchezea matokeo ili kuulinda utawala uliokuwa madarakani.
Vitisho vya Jammeh, uongo na staili yake ya kucheza na hisia za wananchi akijidai tabibu wa Ukimwi  si tu viliwachosha wananchi, bali hata wanajeshi ambao Machi 21, 2006 walifanya jaribio la kumpindua wakati huo akiwa safarini Mauritania, ambapo alilazimika kurejea haraka nyumbani.
Mkuu wa Jeshi, Kanali Ndure Cham, ambaye alituhumiwa kuongoza mapinduzi hayo, aliripotiwa kukimbilia nchi jirani ya Senegal, wakati wengine wakikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa makosa ya uhaini.
Licha ya uchaguzi uliofuata wa mwaka 2006 kushinda kwa asilimia 67.3 na ule wa mwaka 2011 kushinda kwa asilimia 72, na mwaka huu kuwafunga gerezani viongozi wa upinzani, akiwamo wa chama cha United Democratic, Ousainou Darboe, ubabe na nguvu zake za dola haukuweza tena kushinda uamuzi wa wananchi kwenye sanduku la kura.
Silaha nyingine ya Jammeh ambayo alikuwa akiitumia kama turufu ya kushinda uchaguzi wa mwaka huu ya kutaja jina la Mungu, kuwapaka matope wapinzani wake kama ni watu wasiolitakia mema Taifa hilo kwamba wametumwa na mataifa ya Magharibi, haikuweza kamwe kubadilisha uamuzi wa wananchi walioonekana kuchoshwa na uongo, ubabe na maisha duni.
Nilipata kuandika siku za hivi karibuni kuwa, Wamarekani walikuwa tayari kusamehe dhambi zote za Trump kwa sababu alikuwa yu radhi kuusema ukweli mchungu wa yale yaliyowagusa Wamarekani.
Licha ya kuonekana hajajipanga wakati fulani, akisababisha mparanganyiko mkubwa na kuuacha mkutano mkuu wa chama chake cha Republican katika hali ya sintofahamu, wananchi hawakujali hayo yote, waliamini mfanyabiashara huyo anaweza kuleta mageuzi makubwa yaliyowashinda wanasiasa.