24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DUDE LA IPTL LAZIDI KUPINGWA

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM


KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimepinga kusudio la Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura) la kuipa leseni Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Limited (IPTL).

LHRC imetangaza kuweka kusudio la kupinga IPTL kupewa leseni ya kuendelea kuliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku wakihoji usafi na makandokando dhidi ya kampuni hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisema kwa sasa wanamalizia kuandaa pingamizi lao la kisheria ambalo wataliwasilisha Ewura.

Henga alisema IPTL haina sifa tena ya kuendelea kuuza umeme nchini, hasa baada ya kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha kupitia Akaunti ya Tegeta Escrow.

Alisema mwaka 2014 Bunge kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilitoa mapendekezo mbalimbali juu ya umiliki wa mitambo ya IPTL.

“Suala hili tumekuwa tukilifuatilia tangu zamani na tuna ushahidi kwamba IPTL haipaswi kupata tenda hii kwa kuwa  mapendekezo yaliyotolewa na Bunge kuhusu kampuni hii bado hayajatekelezwa.

“Tutapeleka maoni yetu Ewura, tutawaandikia jinsi tunavyoona, lakini kwa hali ya kawaida kwa IPTL hawakuhitaji hata kuomba maoni ya wananchi katika kufanya uamuzi kwa kuwa sifa mojawapo ya kupatiwa leseni ni uadilifu wa muhusika,” alisema Henga.

Alisema moja ya mapendekezo yaliyotolewa na iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Bunge la 10, hadi sasa hayakutekelezwa, ikiwamo kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), kufanya uchunguzi juu ya umiliki na uwepo wa rushwa katika utendaji kazi wa IPTL na wabia wake.

Henga alisema hadi sasa bado hakuna taarifa sahihi juu ya upotevu wa fedha za Watanzania katika akaunti ya Escrow.

“Je, Ewura inatuaminisha kuwa hatuna tatizo na IPTL je, IPTL wapo peke yao walioomba, hakuna kampuni nyingine ya kuwapa? Na kama hamna, wanaweza kutoa sababu za kuwapa IPTL waendelee na leseni hiyo?” alihoji Henga.

Pia alishangazwa na hatua ya uwazi wa kuhitaji maoni kwa kampuni hiyo, hali ya kuwa mikataba inaingiwa kwa siri baina ya wadau hao na Serikali.

 “Tumeshangazwa na kitendo cha Ewura kutaka maoni ya wadau, huku ikiwa inafahamu fika kuwa mikataba kati ya Serikali na IPTL ni siri na hivyo wadau hawana sababu ya kimkataba za kutoa pingamizi au maoni,” alisema Henga.

Alisema kutokana na sababu hizo zinazoendana na misingi ya uwajibikaji, LHRC inapendekeza na kuishauri Ewura kusitisha mara moja kusudio la kukusanya maoni ya kuongezea muda kampuni hiyo hadi Serikali itakapotekeleza mapendekezo ya Bunge.

LHRC imeitaka Ewura kuomba radhi Watanzania na wabunge kwa kujaribu kuirudisha IPTL kwa jamii, huku ikitambua wazi kuwa miaka mitatu iliyopita ilikuwa katika kashfa na mtafaruku ndani na nje ya Tanzania.

Kituo hicho kimeitaka jamii na Watanzania kwa ujumla, wakiwamo wabunge, viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi wa kawaida kuungana kwa masilahi ya umma kwa kuwasilisha mapingamizi kwa wingi ili kugomea mpango wa IPTL kupewa leseni ya kuuza umeme.

Hata hivyo Kampuni hiyo huenda ikakosa leseni kutokana na msimamo wa Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa kupinga mikataba mibovu ya kinyonyaji kwa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles