26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

DUDE LA IPTL LAAMSHWA

 

 

Na EVANS MAGEGE, Dar es Salaam

DUDE limeamshwa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kuwasilisha ombi la kutaka kuongezewa muda wa leseni ya uuzaji wa umeme nchini huku hofu ya kukwama ikitawala.

Hiyo inatokana na jinsi IPTL ilivyoibua mjadala mzito kiasi cha kusababisha baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne kuwajibishwa kwa tuhuma za kupokea mamilioni ya fedha kutoka kwa kampuni hiyo, kinyume cha sheria.

Kwa miaka mingi IPTL  imekuwa ikiiuzia umeme  Tanesco huku  utata wa bei ya umeme huo ukitawala, jambo lililosababisha Bunge la 10 kuazimia  ifukuzwe nchini na kunyang’anywa mitambo.

Hata hivyo, jana   Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilitoa tangazo katika magazeti ikisema imepokea maombi ya IPTL ya kutaka iongezewe muda leseni yake ya kuuza umeme nchini.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi  wakiwamo wanasiasa wamehoji ukomo wa mkataba wa  TANESCO na IPTL huku wengine wakitaka maelezo ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge la 10 kuhusu utata wa mkataba wa kuuzwa hisa za kampuni hiyo kwa mfanyabiashara, Harbinder Singh Seth.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila aliliambia MTANZANIA  jana kuwa  ameandaa pingamizi dhidi ya maombi ya leseni ya IPTL.

Kafulila alisema kwa mujibu wa uamuzi wa Bunge la 10 uliopitishwa mwaka 2014 umiliki wa IPTL unaowakilishwa na Kampuni ya PAP siyo halali.

Pia alisema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG )ya ukaguzi maalumu wa mihamala ya Tegeta Escrow, mmiliki wa sasa wa  IPTL  (Harbinder Singh Seth) siyo halali kwa sababu alitumia nyaraka za kughushi.  

Alisema hoja yake nyingine ya kupinga ombi hilo la IPTL ni kwamba Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia migogoro ya uwekezaji, Februari mwaka 2014 na Septemba mwaka 2016, ilitanabaisha wazi mfanyabiashara hiyo si mmiliki halali wa IPTL.

“Siyo hayo tu hata ukienda kwa Wakala wa Msajili wa Makampuni na Biashara (RELA) mmiliki wa sasa wa IPTL siyo halali kwa sababu hana hati ya umiliki wa kampuni hiyo. “Yaani hapa ni sawa na mtu anajidai anamiliki nyumba wakati hana hiyo hati ya nyumba. Kwa hiyo lazima nipeleke pingamizi kwa sababu hatuwezi kuhalalisha haramu,” alisema Kafulila.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliandika katika ukarasa wake wa mtandao wa  jamii wa Twitter  ujumbe mfupi uliosomeka kwamba ‘leseni ya IPTL kuongezwa na Serikali inayopambana na rushwa’ na baada ya ujumbe huo akaweka picha ya nakala ya tangazo la EWURA.

Katika kutafuta ufafanuzi au majibu ya hoja hizo, gazeti hili lilimtafuta Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Tito Mwinuka lakini  hakupokea simu  kila ilipopigwa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi    hakuujibu.

Tangazo hilo la EWURA la jana lilitanabaisha kwamba inakusudia  kuongeza muda wa leseni ya IPTL kwa mujibu wa mkataba wa mauziano ya umeme kati ya  Tanesco  na mwombaji.

Taarifa hiyo ilifafanua vipengele vya maombi ya leseni kuwa ni kuzalisha umeme, kuongeza muda wa leseni ya kuzalisha umeme kwa mujibu wa Mkataba wa Mauziano ya Umeme baina  ya mwombaji na Tanesco unaoisha Januari 2022.

Vipengele vingine ni mtambo wa kuzalisha umeme wa megawati 110 kwa kutumia mafuta mazito,  muda wa leseni utakuwa ni miezi 55 kwa maana ya kuanza kutekelezwa Julai 16 mwaka huu hadi Januari 15 mwaka 2022.

“Maoni au pingamizi lolote kuhusiana na maombi tajwa hapo juu yawasilishwe kwa maandishi kupitia anuani ya EWURA kabla ya saa 11 jioni  Juni 30 mwaka huu.

Gazeti hili lilimuuliza Meneja wa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo  ambaye alisema shirika litapitia maombi hayo ya IPTL.

Alipoulizwa ikiwa  pingamizi za wananchi zitakuwa nyingi   uamuzi  utatolewa kwa kuzingatia ya walio wengi.

Kaguo alisema kwamba kama  pingamizi zitakuwa nyingi shirika lina uwezo wa kuzuia utekelezaji wake.

Hata hivyo, alisema  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na Wizara ya Nishati na Madini zinaweza kufanya uamuzi zinaoona unafaa.

Baadaye Kaguo alituma taarifa nyingine inayothibitisha kuwa EWURA imepokea maombi ya IPTL ya kuongeza muda wa leseni kwa miezi 55.

“Naomba ieleweke kwamba leseni ya kuzalisha umeme hutolewa na EWURA,   pamoja na mambo mengine,  kwa kuzingatia Mkataba wa Kuuziana Umeme yaani Power Purchase  Agreement (PPA) kati ya Tanesco na wazalishaji wa umeme.

“PPA ya IPTL na Tanesco ilisainiwa  mwaka 1995 kwa miaka 20(from Commercial Operation Date(COD). Leseni ya sasa ya IPTL ilitolewa na Wizara ya Nishati na Madini mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka 21.

“COD ya mradi wa IPTL ilifikiwa mwaka 2002 na kuanzia hapo ndiyo miaka 20 ya PPA ikaanza kuhesabiwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema  maombi yaliyotolewa na IPTL ni kuongeza muda wa leseni uweze kuendana na mkataba wa mauziano ya umeme.

Ilisema maombi yaliyoko EWURA  kwa sasa siyo ya kuidhinisha PPA bali kuhakikisha uzalishaji wa umeme ambao unafanywa na IPTL unafanyika kwa mujibu wa sheria kwa kupata leseni kutoka EWURA.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Umeme na Sheria ya EWURA, MEM, AG na Tanesco ni wadau ambao wameombwa na EWURA kutoa maoni yao kuhusu maombi haya.

“Wananchi pia wameombwa maoni yao kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya EWURA na kifungu cha 8 cha Sheria ya umeme. Kwa hiyo ni vema Watanzania wakatoa maoni yao katika kipindi hiki  kusaidia EWURA kufanya uamuzi sahihi.

“Kutokana na mijadala mingi ambayo imeendelea kwa miaka kadhaa kuhusu mradi huu, maoni ya MEM, AG na wadau wengine yanahitajika sana   kufikia uamuzi sahihi.

“Kwa sasa  kila Mtanzania mwenye maoni au taarifa za kupinga ama kuunga mkono ombi la IPTL anaombwa kuwasilisha EWURA kama tangazo linavyosema,” ilifafanua taarifa hiyo.

Kampuni ya IPTL imekuwa ikitazamwa kwa hisia hasi tangu ilipoibuliwa kashfa ya ukwapuaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.

Suala hilo   lilichochewa na mgogoro wa wanahisa wawili wa IPTL ambao waliamua  kugawana zaidi ya Sh  bilioni 300 zilizokuwa zinahifadhiwa katika akaunti maalumu ya Escrow iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

 Viongozi mbalimbali wa Serikali walichotewa mamilioni ya fedha akiwamo aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye uteuzi wake ulifutwa na Rais Jakaya Kikwete.

Profesa Tibaijuka alipewa mamilioni hayo na aliyekuwa mmoja wa wamiliki wa IPTL, kampuni ya VIP Engineering.

Mbali na hiyo pia suala hilo lilisababisha kuvunjwa kwa bodi ya Tanesco  huku aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akilazimika kujiuzulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles