27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Droni zawapa changamoto kubwa waongoza ndege

NA SABINA WANDIBA – Dar es Salaam

KUWEPO kwa ndege nyuki (droni) imetajwa ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo waongoza ndege nchini kutokana na teknolojia ya mawasiliano ya vifaa hivyo kutoonekana wakati vinaporushwa angani.

Hayo yalisemwa jana na Rais wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TACC), Shukuru Nziku wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya waongoza ndege duniani.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Dar es Salaam jana, Nziku alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto nyingi katika utendaji kazi wao, uwepo wa droni umeonekana kuwa na changamoto kubwa, hivyo kuhatarisha usalama wa ndege angani.

Alisema kifaa hicho kinachotumika kurahisisha kazi kama ujenzi wa miundombinu na upigaji picha za kawaida katika maeneo mbalimbali nchini, wanashindwa kukifuatilia kutokana na kutoonekana kikiwa angani.

“Hii ni changamoto kubwa kwa hizi ndege ambazo hazina rubani ndani, kwakuwa waongoza ndege hawazioni katika satellite, japokuwa sheria ya mwaka 2018 inazuia kifaa hicho kurushwa angani na endapo zitaruka basi kuwepo na mawasiliano ya redio na waongoza ndege, hii ni ngumu kwakuwa hiki kifaa hakina rubani, kinaongozwa na mtu aliyepo chini,” alisema Nziku.

Alisema hivi sasa droni ni nyingi na zinatumiwa kwa shughuli mbalimbali, lakini ni hatari zinapokuwa angani kutokana na kuweza kugongana na ndege kwa kuwa nyingine zinatakiwa kuruka juu zaidi ili kuona eneo kubwa.

Nziku alisema  nchi kama Australia kifaa hicho kimesababisha majanga kwa ndege, hivyo wanafanya jitihada ya kutafuta namna ya kuzifanya zitumike pasipokuleta madhara kwa ndege zinapokuwa angani.

“Japokuwa ni nzuri na zinarahisisha kazi katika uchukuaji wa picha, pia zinapunguza gharama ambazo zingeweza kutumika kwa kutumia ndege ndogo kupiga picha angani, tatizo hazina teknolojia ya kuziongoza, ni vyema watengenezaji wa hiki kifaa waje na mfumo wa mawasiliano na wa kuwezesha kuonekana kwenye mifumo ya kuonekana (Trucking system) kama ilivyo kwa nchi nyingine,” alisema Nziku.

Meneja wa TACC wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mwanajumaa Kombo, alisema mamlaka inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti ambapo kwa sasa mabadiliko ya teknolojia yanawataka waongoza ndege kupata mafunzo mara kwa mara ili kuendana na teknolojia.

“Inatakiwa hawa waongoza ndege wapate mafunzo mara kwa mara, lakini tunashindwa kutokana na bajeti kuwa ndogo, haitoshelezi japokuwa tunajitahidi kuwapa mafunzo kwa uchache,” alisema Mwanajumaa.

Katika kuadhimisha siku hiyo, chama hicho kimetoa msaada wa cherehani tano kwa wafungwa wa gereza la Ukonga zenye thamani ya Sh milioni 1.7 ili kuwasaidia katika shughuli za ushonaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles