25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

DPP awafutia mashtaka mahabusu 201

Na Mwandishi wetu -MUSOMA

MKURUGENZI wa Mashtaka   (DPP), Biswalo Maganga, amewafutia kesi mahabusu 201 waliokuwa katika magereza ya wilaya za Musoma, Tarime na Mugumu Serengeti.  

Mganga alifikia uamuzi huo katika ziara aliyofanya kwenye magereza ya Mkoa wa Mara akiwa amefuatana  na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju.

Viongozi hao waliofuatana  na wataalamu wao walifanya ukaguzi ndani ya magereza na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya magereza hayo  kujua changamoto za  sheria zinazowakabili.

Baada ya kuzungumza na mahabusu hao na kupitia majalada yao, Mganga aliwaagiza waendesha mashtaka Mkoa wa Mara kwenda mahakamani na kuzifuta kesi zilizokuwa zikiwakabili mahabusu hao ambao wataachiwa huru baada ya mahakama kupokea nia ya DPP ya kufuta kesi hizo kwa mujibu wa sheria.

Mahabusu   29 wanatoka katika Gereza la Wilaya ya Musoma, 106 wanatoka katika Gereza Tarime na wengine 66 wanatoka katika Gereza Mugumu-Serengeti. Katika mahabusu hao wanawake ni 11, watoto 39, wazee tisa na wanaobakia ni vijana ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi mbalimbali ambazo zilionekana zinaweza kumalizwa nje ya mahakama.

Alisema katika baadhi ya kesi ushahidi ulionekana kuwa hafifu, nyingine ni kesi ndogo ndogo kama kupigana, kutukanana, wizi wa simu na vitu vingine vidogo vidogo, kutishiana kwa maneno, waliokiri kunywa gongo na kuvuta bangi, wengine walionekana kuwa mashahidi wa mashtaka.

Mganga aliwataka wote wanaohusika na kazi ya upelelezi wa kesi mbalimbali zinazowakabili mahabusu hao kuhakikisha wanakamilisha upelelezi wa kesi mbalimbali kwa wakati kuondoa hali ya upelelezi kuchelewa. Alisema kitendo cha kuchelewesha upelelezi kinawafanya watuhumiwa wa makosa ya jinai nchini kukaa magerezani kwa muda mrefu bila kujua hatma yao na hivyo kufanya magereza kuwa na msongamano ambao unaweza kuzuiliwa.

“Wapelelezi mlioko hapa  nadhani mnaelewa ninachokisema hapa, fanyeni kazi haraka kesi za watuhumiwa hawa   ziweze kumalizwa na  wajue moja kama wanafungwa au wanaachiwa huru maana kwa kuendelea kuwa mahabusu hakuna tija kwa taifa.

“Hawa watu humu ndani wanatakiwa wafanye kazi za uzalishaji na hiyo inakuwa sehemu ya urekebishwaji na siyo kukaa bure na kujazana,”

alisema   Mganga Naye Mpanju akizungumza na wafungwa na mahabusu katika nyakati tofauti ndani ya magereza hayo, aliwataka watakaofutiwa mashtaka kubadili mienendo na kuwa raia wema na kuacha kuishi kwa mazoea kwa sababu  kufanya hivyo ni kuvunja sheria na Serikali haitoacha kuwachukulia hatua za  sheria.

“Mmeona kazi kubwa tulioifanya leo hii humu ndani, ni wajibu wenu kuwa raia wema na kubadili mienendo ya maisha yenu. “Muache kuishi kwa mazoea, muangalie mnavyoishi na mkiachiliwa mkaambie na wenzenu kwa sababu  kufanya hivyo ni kuvunja sheria na Serikali haitawaacha lazima hatua za  sheria zichukuliwe,”  alisema   Mpanju.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles