25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

DPP aomba kutaifisha bilioni 16/-

Kulwa Mzee -Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga ameiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutaifisha zaidi ya Sh bilioni 16 kutoka kwa raia wawili wa kigeni wanaotuhumiwa kujihusisha na mchezo haramu wa upatu.

Jamhuri imebaini watu kadhaa, viongozi wa Serikali na viongozi wa dini, walihusika katika mchezo huo wa upatu, ambao waliwekeza mamilioni ya fedha zikiwamo za sadaka ili kujitajirisha na kuhatarisha uchumi wa nchi.

Maombi ya kutaifisha fedha hizo kuwa mali ya Serikali, yaliwasilishwa jana mbele ya Jaji Elinaza Luvanda na DPP Biswalo akisaidiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Shadrack Kimario na Christopher Msigwa.

Kwa mujibu wa maombi hayo, fedha zinaombwa kutaifishwa kutoka kwa Manon Elisabeth Hubenthal, mkazi wa Greven nchini Ujerumani na Frank Robert Riketits, Mkazi wa Blackwats, Uingereza. Wote ni wakurugenzi na wanahisa wa Kampuni ya IMS Marketing Tanzania Limited.

Maombi hayo yaliambatanishwa na hati mbili za viapo zilizowasilishwa na Wakili wa Serikali, Estazia Wilson na Wakili wa upelelezi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Fadhili, wakielezea jinsi washtakiwa hao walivyohusika katika kutenda uhalifu wa kuendesha mpango wa upatu na utakatishaji fedha.

Akiwasilisha maombi hayo, DPP Biswalo alidai amri ya kutaifisha fedha hizo ni muhimu ili kuzuia wahalifu kufaidika na makosa ya jinai waliyotenda.

“Katika hali ya kushangaza tumegundua watu kadhaa, viongozi wa Serikali na viongozi wa dini walihusika katika mchezo wa upatu, waliwekeza mamilioni ya fedha kujitajirisha na kuhatarisha uchumi wa nchi.

“Unaweza kufikiria kiongozi mmoja wa kidini alichukua milioni 100/- za sadaka na kupanda pesa kama hizo kwenye upatu. Tunaamini kama maombi haya yatakubaliwa, viongozi hawa wa Serikali na kidini wataacha kujihusisha na michezo hii michafu. Itawazuia wengine kutenda makosa,” alisema DPP Biswalo.

Wakifafanua zaidi walidai  akaunti mbili za Dola za Marekani 1,351,597.79 na akaunti nyingine ya Euro 5,377,306.56, zote mbili kwa jina la IMS Marketing Tanzania Limited zilifunguliwa na washtakiwa katika Benki ya Afrika (BOA).

DPP pia iliomba mahakama kuiagiza Benki ya BOA Limited kulipa riba kwa kukaa na kiasi hicho kikubwa cha fedha tangu Januari 19, 2018, wakati wakijua fedha hizo si halali.

Baada ya kusikiliza maombi hayo, Jaji Luvanda anatarajia kutoa uamuzi kuhusu shauri hilo Aprili 3.

Mahakama ilielezwa Januari 19, 2014, raia hao walikuja nchini na kusajili IMS Marketing Tanzania Limited, kampuni ambayo ilipewa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni leseni ya kutoa huduma mbalimbali za masoko.

Kwamba ukusanyaji wa fedha kutoka kwa umma na kuendesha upatu kwa ujumla, haikuwa miongoni mwa malengo ya biashara ambayo kampuni ilisajiliwa.

Inadaiwa katika tarehe tofauti, washtakiwa walifungua akaunti tajwa katika Benki ya BOA baada ya kusajili kampuni, ambayo ina uhusiano wa karibu na kampuni nyingine ya IMS International Marketing Services ya Singapore.

Kampuni kama hiyo ya Singapore, inadaiwa ina uhusiano wa karibu na ni sehemu ya operesheni ya Kampuni ya Onecoin Limited, iliyoanzishwa Aprili 2014 huko Gibraltar, ina ofisi nchini Bulgaria na Falme za Kiarabu.

DPP alidai shughuli za Kampuni ya Onecoin Limited na kampuni tanzu katika mamlaka mbalimbali zilisimamishwa na akaunti zao za benki kufungwa kwa sababu ya kujihusisha na utakatishaji fedha uliosababishwa na mchezo haramu wa upatu.

Kutokana na kusimamishwa kwa shughuli hizo, Onecoin Limited ilitangaza kwenye akaunti yake ya facebook na wavuti zake, wanachama wanapaswa kulipa vifurushi na michango yao kupitia akaunti za benki zinazotunzwa katika Benki ya BOA.

Alidai kuwa kwa tarehe tofauti, Sh 16,720,858,579/47 zilipokewa kutoka kwenye akaunti zote tatu za benki. Kiasi hicho kinajumuisha Dola za Marekani 1,351,597.79 katika akaunti mbili za USD na zingine Euro 5,377,306.56 katika akaunti ya Euro.

Kuzingatia ushahidi huo, DPP alifungua kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya raia hao Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa mashtaka matatu ya kula njama ya kutenda kosa, kuendesha upatu na utakatishaji fedha.

Kwa kuwa watuhumiwa walikuwa hawajakamatwa, mwendesha mashtaka aliomba na kupata hati ya kuwakamata,  lakini hawakuweza kujitokeza.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles