Na KHAMIS SHARIF
– ZANZIBAR
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka Kisiwani Pemba, imesema bado wananchi wana uwelewa mdogo wa kupinga udhalilishaji.
Imesema baaadhi ya wananchi huwasilisha barua katika ofisi hiyo za madai ya kuomba kufutwa kesi za jinai zikiwamo za udhaliliushaji.
Mwanasheria wa Ofisi ya DPP, Ali Rajab Ali, alikuwa akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni kwenye maonyesho ya Siku ya Sheria.
Alisema hatua hiyo imekuwa ikiwashangaza hasa kwa jamii kushindwa kuona umuhimu wa mashauri hayo kama yanalinda haki za watu badala ya kutaka kesi zifutwe.
“Kila mwezi tumekuwa tukipokea kati ya maombi 15 hadi 20 kutoka kwa wananchi wakiomba kufutwa kesi zao zikiwamo za udhalilishaji, jambo ambalo huwa linatupa mshangao.
“Baada ya mwananchi kupatwa na masahibu ya kesi za udhalilishaji sisi wakati wote tupo tayari kuona kesi inakwenda mbele lakini baada ya muda huletwa barua za kuomba kufutwa kesi hizo.
“Tena kinachoumiza zaidi ni kesi hizo zipo zile zinazolalamikiwa sana na jamii zikiwamo za udhalilishaji lakini ikifika mahakamani kwa ajili ya ushahidi huwa ngumu,” alisema Ali.
Mwanasheria huyo alisema miongoni mwa sababu ambazo huandikwa na wananchi hao ni kwa mtuhumiwa kufunga ndoa na muathirika wa tukio.
Akizungumzia sababu za nyingine kutaka kufutwa kesi hizo, Ali alisema, ni undugu baina ya mtuhumiwa na aliyefanyiwa kitendo cha udhalilishaji.
“Huwa tunakaa nao nje ya mahakama na kuwaeleza kuwa sheria zetu zinakataza kufutwa kesi yoyote ya jinai, na kuwaomba wafike mahakamani kutoa ushahidi na wapo wanaotii hilo,” alisema.